Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

UTAFITI: Jinsi shinikizo la Moyo linavyoathiri Ubongo wako

Your Second Brain Is In Your Heart UTAFITI: Jinsi shinikizo la Moyo linavyoathiri Ubongo wako

Mon, 15 Nov 2021 Chanzo: Habarileo

UTAFITI kuhusu athari za shinikizo la damu kwa ubongo uliofanywa na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) umebaini wanaougua ugonjwa huo wapo hatarini kuathirika ubongo.

Utafiti huo ulioanza Machi mwaka jana hadi Februari mwaka huu ulihusisha wagonjwa 1,201.

Mmoja wa washiriki wa utafiti huo kutoka JKCI, Dk Pedro Pallangyo, alisema matokeo ya utafiti huo yalionesha kuwa shinikizo la damu linaathiri kumbukumbu na uwezo wa umakini.

Alisema asilimia 43.6 sawa na wagonjwa 524 walikutwa na mabadailiko hasi.

“Tulifanya utafiti huu uliolenga kuangalia mabadilikokatika mfumo wa fahamu yaani ubongo yanayotokana na madhara ya shikizo la damu la muda mrefu,” alisema.

Akaongeza: “Kwa muda mrefu shinikizo la damu limekuwa likihusishwa kuleta matokeo hasi katika ubongo wa mwanadamu na matokeo hayo, yanatokana na shikizo la damu kuathiri mishipa ya damu inayopelekeka damu kwenye ubongo,” alisema.

Dk Pallangyo alisema wagonjwa ambao kwa namna moja au nyingine wameshindwa kudhibiti shikizo la damu katika viwango salama yaani chini ya kiwango cha 140 chini 90 wapo hatarini zaidi.

“Shinikizo la damu limehusishwa na kupunguza uwezo wa ubongo kufikiria na uwezo wa mwanadamu kuwa na kauli sawasawa na pia, umeonesha kupunguza uwezo wa kumbukumbu na umakini na haya yameripotiwa ulimwenguni pia,” alisema.

Dk Pallangyo alisema wagonjwa waliohusika katika utafiti huo ni nje kwa maana ya wanaofanya kliniki katika taasisi hiyo ambao tayari waligundulika na walianza matibabu.

“Asilimia 17 walikuwa na ugonjwa wa kisukari, asilimia 8 walikuwa na historia ya kupata kiharusi, asilimia 6 walikuwa na mioyo ambayo uwezo wake ulipungua na asilimia 17 walikuwa na matatizo ya figo ya kudumu, asilimia 54 walikuwa na upungufu wa damu na theluthi moja ya wagonjwa wote walikuwa na kiwango kikubwa cha mafuta kwenye damu,” alisema.

Kwa mujibu wa Dk Pallangyo, katika utafiti huo walitumia dodoso linalokubalika kimataifa linalotumika kupima uwezo wa ubongo.

“Tuliweza kwenda mbele kuangalia vitu gani vingine vilihusishwa na upungufu wa uwezo wa ubongo tulipata vitu kadhaa watu waliokuwa na elimu ya msingi na wasio nayo walikuwa na uwezo mara tatu na nusu kuwa na tatizo ukilinganisha na wale waliosoma elimu ya sekondari na kuendelea,” alisema.

Akaongeza: “Wahusika waliostaafu walikuwa na ongozeko la tatizo hilo ukilinganisha na wale ambao wana kazi za kila siku za kuingiza kipato.”

Alisema utafiti huo pia ulibainisha watu waliokuwa wanaishi katika mazingira ya kijijini walikuwa na ongezeko la asilimia 80 ya kuwa na upungufu huo ikinganishwa na waliokuwa wakiishi mjini.

“Mwisho wagonjwa waliokuwa na tatizo la figo la kudumu walikuwa na ongezeko la kupata tatizo hilo ukilinganisha na wagonjwa ambao figo zao zilikuwa vizuri,” alisema Dk Pallangyo.

Chanzo: Habarileo