Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

USHAURI WA DAKTARI: Tofauti na ujauzito, sababu zinazokufanya ukose hedhi ni hizi

67696 Dk+CHRIS

Mon, 22 Jul 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Sababu kuu ya kukosa hedhi ambayo wengi pia tumeizoea ni ujauzito. Kwa kawaida mwanamke hapati hedhi kwa kipindi chote cha ujauzito, kutokana na sababu za kibaiolojia. Lakini sababu nyingine zinaweza kuwa ni matatizo ya kwenye via vya uzazi na mfumo wa uzazi kwa ujumla au tezi zinazosaidia kuratibu viwango vya homoni mwilini kama nilivyoeleza hapo awali. Ni muhimu kupata ushauri wa daktari ili kuchunguza moja ya matatizo haya.

Vipindi ambavyo mwanamke anakosa hedhi kiasili ni pamoja na anapokuwa mjamzito, anakoma siku na imethibitika baadhi yao wanapokuwa wananyonyesha.

Sababu nyingine ni matumizi ya baadhi ya njia za uzazi wa mpango. Baadhi ya wanawake wanaotumia vidonge vya uzazi wa mpango wanaweza kukosa hedhi kwa kipindi fulani.

Hata baada ya kuacha kutumia vidonge hivyo au njia nyingine za uzazi wa mpango kama sindano, vipandikizi huchukua muda kupata hedhi.

Matumizi ya aina fulani za dawa pia huchangia tatizo hilo, kwa kuwa na uwezekano wa kuharibu mfumo wa homoni mwilini na kusababisha kukosa hedhi kwa kipindi fulani zikiwamo za magonjwa ya akili, tiba ya magonjwa ya saratani, dawa za sonona, dawa za shinikizo la damu na dawa za aleji.

Hivyo ni kawaida kwa mwanamke anayetumia dawa hizi kukosa hedhi kwa kipindi chote cha tiba.

Pia Soma

Lakini pia sababu za aina ya maisha zinachangia kukosa hedhi, mathalani uzito uliopungua kwa zaidi ya asilimia 10 chini ya uzito wa kawaida, unaweza kuvuruga utendaji kazi wa mfumo wa homoni mwilini. Kwa wanawake wenye matatizo ya kukosa hamu ya kula wapo hatarini sana kupata tatizo hili.

Msongo wa mawazo pia unachangia. Msongo wa mawazo unaweza ukasimamisha kwa muda utendaji kazi wa “hypothalamus”- eneo ambalo ubongo unahimili vichocheo na kuratibu mzunguko wa hedhi. Na matokeo yake hedhi inaweza kusimama. Ratiba ya mzunguko wa hedhi ya kawaida inaendelea baada ya msongo wa mawazo kupungua.

Kutopata hedhi pia kunachangiwa na kutokuwa na uwiano kwenye mfumo wa homoni ambako mara nyingi hutokana na matatizo ya kiafya kama vile kuwa na vimbe kwenye tezi za pituitari ambako kunaingilia utendaji kazi wa homoni.

Lakini pia matatizo machache yanayojitokeza kwenye viungo vya uzazi kama vile ndani ya ukuta wa mfuko wa uzazi yanaota makovu ambayo yamejitokeza baada ya tiba mbalimbali ambayo mwanamke alilazimika kufanyiwa upasuaji au tiba yoyote ya kutibu vimbe zilizoota kwenye mfuko wa uzazi.

Pia kuna sababu ambayo hutokea kwa nadra sana ambayo ni ya kimuundo wa via vya uzazi kwa mwanamke ambaye mlango wake wa kizazi ni mdogo na hauwezi kufunguka kuruhusu kutoka kwa damu.

Chanzo: mwananchi.co.tz