Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

USHAURI WA DAKTARI: Simanzi ya kuachika yaweza kukupa ugonjwa wa moyo

80956 Kuachika+pic USHAURI WA DAKTARI: Simanzi ya kuachika yaweza kukupa ugonjwa wa moyo

Mon, 21 Oct 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Broken heart syndrome au Takostubo ni tatizo la moyo linalosababishwa na mtu kupata simanzi au huzuni kali baada ya kutengana au kuachika na mwenza au mpenzi.

Tatizo hili husababishwa na kudhoofika ghafla kwa misuli ya moyo kwa kipindi kifupi huitwa Takastubo, hilo jina limetokana na ukweli kwamba mgunduzi wa ugonjwa huu ni Mjapani.

Wataalam wa magonjwa ya moyo wanalitofautisha tatizo hili na yale matatizo ya kukosekana kwa damu ya kutosha katika misuli ya moyo.

Takostubo inajitokeza zaidi pale watu wa karibu au wenza wa karibu ambao wanamgusa moja kwa moja mwathirika wanapofariki ghafla, wanaachwa na kuwa na hofu au wasiwasi kwa muda mrefu. Jumuiya ya wataalam wa moyo duniani wanakubaliana kuwa tatizo hili huweza kusababisha kushindwa kufanya kazi kwa moyo ghafla, moyo kudunda bila mpangilio.

Tatizo huwa na dalili mbalimbali ikiwamo maumivu makali ya kifua, kupumua kwa shida, kuhema kwa taabu, uchovu, kuweweseka, kuhisi mapigo ya moyo kudunda bila mpangilio na kuhisi kizunguzungu.

Tatizo hili huweza kuonekana zaidi pale mtu anapopokea taarifa ya kufiwa, kuibiwa mali au pesa zenye thamani kubwa, kugundulika kuugua magonjwa sugu kama vile Ukimwi na saratani, kutakiwa kuongea katika hadhara na kushtukizwa jambo.

Pia Soma

Advertisement
Vilevile watu wenye hatari ya kupata tatizo hili ni kama wale wenye magonjwa kama pumu, maambukizi hatari, kupata ajali mbaya au kufanyiwa upasuaji mkubwa mwilini.

Vipimo vya msingi ambavyo ni muhimu kufanyika haraka ni pamoja na kipimo cha kuchunguza mwenendo wa moyo ECG, picha ya xray ya kifua, Echocardiogram, picha ya MRI na CAG.

Vipimo vingine ni pamoja kutazama taswira nzima ya damu na chembechembe zake, kipimo cha kuangalia vimeng’enyo vya moyo na vipimo vingine kubaini magonjwa sugu ikiwamo VVU.

Vipimo hivi ni muhimu ili kumwezesha daktari kutofautisha ugonjwa huu na shambulizi la moyo (heart attack)

Hakuna tiba ya madawa iliyo maalum kwa ajili ya kutibu tatizo hili pekee. Matibabu yake yanaweza kufanana na matibabu ya shambulio la moyo, na mgonjwa anaweza kuhitaji kulazwa hospitali kwa muda tu.

Daktari akishathibitisha kuwa chanzo cha dalili ni broken heart syndrome na wala si shambulio la moyo anaweza kukupatia dawa zilizo katika makundi mawili.

Dawa hizo husaidia kupunguza mzigo katika moyo na pia kuzuia usipate shambulio jipya. Kwa kawaida wagonjwa wengi hupata nafuu baada ya muda wa mwezi mmoja hadi miwili.

Kuna uwezekano mkubwa sana wa hali hii kujirudia tena mara baada ya shambulio la kwanza.

Mpaka sasa hakuna dawa zilizothibitishwa zinazoweza kusaidia kuzuia hali hii isijitokeze tena, ingawa baadhi ya madaktari wanashauri matumizi ya muda mrefu ya dawa za kundi la beta blockers au dawa zenye kuzuia uzalishaji wa homoni zenye kuchochea shinikizo katika moyo.

Pamoja na matumizi ya dawa, ushauri nasaha pamoja na kubadili mfumo wa maisha ni mambo ya muhimu kusaidia kukukinga na tatizo hili.

Vilevile tatizo hili huweza kupelekea moyo kushindwa kufanya kazi ghafla, moyo kupiga bila mpangilio na kasi isiyo ya kawaida.

Chanzo: mwananchi.co.tz