Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

USHAURI WA DAKTARI: Mambo yanayoweza kuharibu ujauzito

59793 Shita+Samweli

Sun, 26 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Inapotokea mtoto kufia katika nyumba ya uzazi au kuzaliwa akiwa na maumbile yasiyo timilifu na kumpa ulemavu wa kudumu, huwa ni mshtuko na masikitiko kwa wanajamii, hasa wazazi.

Mama aliyemzaa au kumbeba mtoto huyo katika nyumba ya uzazi, ndiye anayekua na huzuni zaidi. Hii ni kutokana na uhusiano wa moja kwa moja na ujauzito alioubeba kwa miezi tisa.

Yapo mambo ambayo yamekuwa yakichangia madhara tofauti ya kiafya kwa mtoto ambaye bado hajazaliwa, kama dawa za matibabu, kemikali za viwandani zitumikazo majumbani, dawa za kulevya, utumiaji wa tumbaku (uvutaji wa sigara), utumiaji wa pombe na baadhi ya vyakula vilivyogusana na taka sumu.

Mambo mengine ni pamoja na maambukizi ya maradhi, kama virusi na bakteria, uvutaji wa hewa chafu zenye gesi zenye sumu, hasa katika maeneo yenye viwanda vya kemikali na nyuklia, pamoja na baadhi ya mienendo na mitindo mibaya ya kimaisha.

Madhara yanayotokana na mambo hayo ni kama vile mtoto kufia tumboni, mimba kuharibika na kutoka, mtoto kuzaliwa njiti au kabla ya siku zake kutimia, mtoto kupata majeraha ya mfumo wa fahamu na kuzaliwa na uzito mdogo.

Madhara mengine ni pamoja na mtoto kutokuwa na ukuaji mzuri katika nyumba ya uzazi, kuwa na viungo visivyo timilifu, kama vile kuzaliwa bila mikono au miguu na mdomo sungura, kuwa na ogani zenye hitilafu kama vile moyo, figo, mapafu, ubongo na mfumo wa chakula.

Pia Soma

Mambo haya yanaweza kuchangiwa na tabia zetu hasa ya kutumia dawa kiholela pasipo kuandikiwa na daktari ama kutozingatia ushauri unaotolewa na wataalamu wa afya.

Mara nyingi wanaotumia dawa kiholela ni wale wanaozinunua katika maduka yasiyosajiliwa, mbaya zaidi muuzaji wa dawa hizo ni yule asiye na ujuzi wa mambo ya madawa ambaye ni vigumu kujua dawa hiyo kama ni salama kwa mjamzito.

Wimbi la matabibu wa kienyeji ambao hawana sifa za kutibu wala kumiliki leseni ya kutibu na ambao hujitangaza kuwavutia wagonjwa, ni kati ya changamoto mpya ya afya ya uzazi.

Matabibu hawa huwafanya watu, hasa wajawazito kuvutiwa na matangazo hayo na kutumia dawa hizo ambazo hazifahamiki wala kutafitiwa kisayansi kama ni salama kwa wajawazito.

Wajawazito wanapaswa kuwa waangalifu. Wasitumie dawa yoyote bila kushauriwa na daktari anayetambulika serikalini, kwa kuwa baadhi ya dawa zinaweza kuwa na faida kutibu ugonjwa fulani, lakini kumbe kwa mjamzito inamdhuru mtoto aliye tumboni.

Si ajabu pia ujauzito ukaharibika na sababu isijulikane moja kwa moja.

Chanzo: mwananchi.co.tz