Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

USHAURI WA DAKTARI: Majimaji haya ukeni ni dalili ya ugonjwa

44682 Shita+Samweli USHAURI WA DAKTARI: Majimaji haya ukeni ni dalili ya ugonjwa

Tue, 5 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mchozo ni msamiati wa kiswahili ukimaanisha ni uchafu unaotoka ukeni ambao si wa kawaida. Leo nitajibu maswali mawili muhimu kwa wanawake.

Mmoja wa msomaji wetu ameuliza hivi, mimi ni msichana wa miaka 22 ninaishi Mwanza, nina shida ya kuumwa tumbo na kutokwa na ute mweupe mzito ila hauna harufu. Tafadhali daktari nisaidie tatizo nini na je nitumie dawa gani ili niweze kuondokana nalo?

Jibu: pole sana, kwa kawaida uke hutoa maji maji yenye rangi ya maziwa ambayo huwa myembamba na meupe na huwa hayana harufu ya kukera, kuchoma/mwasho au kuambatana na vipele. Kiwango chake pamoja na muonekano wake kwa siku unaweza kubadilika kadri umri unavyopiga hatua.

Kutokana na maelezo yako ina maana ute huo si wa kawaida kwani ni mzito.Dalili hiyo ni dalili za fangasi za ukeni, inaweza kuwa na mwonekano kama vile maziwa ya mgando inaweza kuwa na muwasho.

Tatizo hili linaweza kutibiwa kwa dawa za fangasi za kutumbukiza ukeni. Nakushauri fika katika huduma za afya zilizo jirani kwa ajili ya uchunguzi wa visababishia au vihatarishi vya tatizo hilo na kuthibitisha tatizo.

Swali: Dr habari, pole na majukumu. Mke wangu anasumbuliwa na tatizo la V.Discharge kwa muda mrefu ambalo huwa na kawaida ya kujirudia mara kwa mara.

Amekuwa akipewa sindano ya Power safe na vidonge vya Fluconazole pale tatizo hili linapojitokeza, lakini bado tatizo hujirudia tena. Naomba msaada wako tafadhali, je mke wangu atumie dawa gani au njia gani ili aweze kupona tatizo hili?

Jibu :V.discharge maana yake ni utokaji wa uchafu ukeni usio wa kawaida. Zipo sababu mbalimbali zinazoweza kuchangia kutokwa na uchafu huo ikiwamo uwepo wa vitu vigeni ukeni kama vile vipande vya pedi au pamba, uambukizi wa bakteria, parasite, fangasi na virusi.

Maambukizi ya bakteria mara kwa mara ni vijidudu vya kisonono, chlamydia, mycoplasma na parasite huwa ni trichomonas vaginalis na fangasi ni candida albicans na virusi huwa ni herpes simplex.

Uchafu unaotokana na uambukizi wa bacteria huwa na harufu kama shombo la samaki ambayo huhisiwa baada ya kujamiana na unaweza kuwa na rangi ya kijivu, kijani kibichi njano au mchanganyiko na damu.

Kama ni maambukizi ya fangasi ni kama nilivyoeleza katika swali la kwanza, uambukizi wa parasite uchafu unaotoka huwa ni mwingi na unakuwa na harufu mbaya, wenye rangi kijani-njano wenye povu.

Vile vile uambukizi wa bakteria unaweza kuambatana na utokaji wa usaha, vipele au vidonda, mwasho.

Kwa jinsi ulivyouliza na maelezo yako inawezekana kabisa una maaambukizi mchanganyiko yaani fangasi sugu za ukeni na uambukizi wa bakteria au parasite.

Nakushauri ufike katika vituo vya afya vya wilaya au hospitali ya mkoa uliopo, kwani zipo idara maalum za magonjwa hayo ambayo ipo miongozo sahihi ya matibabu na uchafu huo unaweza kuchukuliwa kwa ajili ya upimaji na uoteshaji.

Kumbuka magonjwa hayo yanahitajika kutibiwa na wenza wote wawili mnaoshirikiana tendo la ndoa ili kuepuka tatizo kujirudia. Mtapewa matibabu huku mkiendelea kufuatiliwa maendeleo yenu mpaka kupona.

Tendo la ndoa lazima liwekwe kando kwanza mpaka atakapopona.



Chanzo: mwananchi.co.tz