Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

USHAURI WA DAKTARI: Kukojoa mara nyingi ikiwamo kitandani inaweza kuwa dalili ya maradhi mengine mwilini

68581 Dk+CHRIS

Sun, 28 Jul 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Nimeona leo nizungumzie tatizo la watu wazima kukojoa kitandani hasa baada ya kugundua kila mmoja ana mtazamo tofauti.

Tatizo hili, mara nyingi limekuwa likiwaathiri watoto na hasa wa chini ya miaka mitano, kwa umri huu inatambulika kuwa ni kawaida kutokana na sababu za kibaiolojia ambazo zipo kwenye ukuaji wa mtoto ingawa wakati mwingine tatizo hudumu hata baada ya miaka mitano na hapa sasa wazazi au walezi hujenga imani kwamba watoto hawa wanafanya makusudi.

Hapo wazazi huanza kuwaadhibu watoto ingawa adhabu haijawahi kutibu tatizo hili na mbaya zaidi sasa tatizo linaathiri hadi watu wazima.

Kuna waliokuwa nalo tangu utotoni na hata baada ya kukua linaendelea na wapo waliolipata ukubwani. Kukojoa kitandani ni makusudi au umefika wakati sasa jamii kutambua kama ni tatizo la kiafya kama mengine?

Kinachosikitisha ni kuwa watu wengi wana tatizo hili lakini wachache sana kati yao huenda kutafuta msaada wa kimatibabu, wengi huona aibu.

Tatizo hili linajulikana kama nocturnal enuresis kwa lugha ya kitabibu na linasababishwa na sababu kadhaa.

Pia Soma

Sababu ya kwanza inaweza kuwa figo kuchuja sana mkojo kuliko kawaida. Mwilini kuna kichocheo kinaitwa ADH, wakati wote kinafanya kazi ya kuwasiliana na mfumo wa mkojo kwa kuziamuru figo kuchuja kiwango kidogo cha mkojo.

Kwa baadhi ya watu kichocheo hiki hakifanyi kazi wakati wamelala au kinafanya kazi kidogo wakati huo na kuziacha figo zikichuja mkojo kupita kiasi kwani hazidhibitiwi na homoni hii ya ADH. Hivyo kifupi ni kwamba, moja ya sababu za kukojoa kitandani kwa watu wazima ni kushindwa kufanya kazi kwa homoni ya ADH.

Utendaji kazi wa homoni hii huathiriwa na sababu kadhaa ikiwemo ugonjwa ya kisukari na ndio maana wenye kisukari wanakojoa sana.

Sababu nyingine ni kibofu kushindwa kuhifadhi kiasi kikubwa cha mkojo. Wakati mwingine sababu za kiafya zinaathiri kibofu, zinavuruga kabisa utendaji wake na kusababisha kishindwe kuhifadhi mkojo kabla ya kujaa unapitiliza moja kwa moja na kutoka nje. Mara zote misuli ya ndani ya kibofu, hukaza na kukakamaa wakati ambao tayari kibofu kimeshajaa ili kuruhusu mtu akojoe, sasa wakati mwingine misuli hii hukaza wakati ambao si sahihi.

Yote ni kutokana na sababu za kiafya ambazo zimeenda kuathiri kibofu na kuvuruga utendaji kazi wake.

Pia, tatizo hili linaweza kuwa ni dalili ya baadhi maradhi mengine ambayo unaweza usiyatambue haraka. Maradhi hayo utahisi yameingia mwilini mwako kupitia tatizo la kukojoa kupitiliza hata wakati wa mchana, lakini zaidi ni kukojoa kitandani.

Hivyo kwa mtu mzima ambaye tatizo hili limemkuta ukubwani, ni vyema akatambua kuwa huenda ananyemelewa na baadhi ya magonjwa kama saratani ya tezi dume, uwepo wa mawe kwenye figo (kidney stones) uwepo wa mawe kwenye kibofu (bladder stones) au kisukari.

Tatizo la kukojoa kitandani lichukuliwe kuwa ni tatizo la kiafya na si uzembe, mhusika asione aibu kutafuta matibabu kwa kuwa linatibika.

Chanzo: mwananchi.co.tz