Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

USHAURI WA DAKTARI: Chunusi sugu ni dalili ya kuwa na maradhi mwilini

58422 Pic+chunusi

Sun, 19 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Uchovu, maumivu ya viungo na mwili mzima, maumivu ya tumbo na kichwa ni baadhi tu ya dalili ambazo wengi tumezizoea ambapo kupitia hizo tunaanza kutambua kuwa afya zetu hazipo sawa na huenda kuna baadhi ya magonjwa yanaashiria kutushambulia na hivyo inatulazimu kuchukua hatua za kupata matibabu haraka kabla hali haijawa mbaya zaidi.

Lakini kila tunapojiangalia kwenye vioo, nyuso zetu pia zinasema mengi kuhusu afya zetu. Baadhi ya magonjwa mengi yanayoweza kuleta madhara makubwa kiafya tunaweza kuyatambua kwa dalili zinazojitokeza kwenye nyuso zetu.

Kujiangalia kwenye vioo ni jambo la kawaida ambalo tunalifanya kila siku, lakini tunapojiangalia kwa makini, wakati mwingine tunaweza kuyaona mabadiliko madogo madogo ambayo yamejitokeza usoni.

Mabadiliko haya tunaweza kudhani ni ya kawaida, lakini ukweli ni kwamba hatupaswi kuyafumbia macho kwa sababu yanaashiria matatizo fulani ya kiafya.

Rangi ya ngozi na jicho kuwa njano

Hii ni homa ya manjano. Inatokea pale ambapo una uchafu mwingi mwilini au takamwili.

Pia Soma

Hali hii huwa ni ya kawaida na isiyokuwa na madhara kwa watoto wachanga wenye umri wa wiki 38 hadi 40 kwa sababu maini yao bado hayajakomaa kama yanavyotakiwa.

Lakini kwa watu wazima, homa ya manjano inaweza kuashiria matatizo makubwa zaidi ya kiafya kama vile maambukizi ya aina mbali mbali ya virusi kama vile yale yanayoshambulia ini (hepatitis), na magonjwa mengine ya ini, matatizo ya kongosho, au madhara yatokanayo na utumiaji wa vilevi.

Chunusi sugu

Mara chache unaweza kupata chunusi au vipele vyeusi usoni. Hivi mara nyingi vinaashiria aleji ya chakula au matumizi ya baadhi ya sabuni za kuogea na mchafuko wa damu na baada ya muda hutoweka. Lakini ni vyema kufanya vipimo hasa inapotokea chunusi hizi zinakuwa sugu.

Kwa kufanya hivi kutasaidia kutambua dalili za magonjwa mengine mapema zaidi na hasa saratani ya ngozi. Zungumza na mhudumu wako wa afya haraka iwezekanavyo kama ukiona chunusi kwenye uso wako zinadumu kwa muda mrefu.

Vidonda vidogo pembeni ya mdomo

Vidonda vinavyojitokeza pembeni ya mdomo mara nyingi vinasababishwa na baridi au na maambukizi ya magonjwa ya zinaa yanayotokana na kufanya tendo la ndoa aidha kwa njia ya mdomo au tabia ya kunyonya via vya uzazi wakati wa tendo la ndoa.

Maambukizi yanayopatikana kupitia njia hii yanasababishwa na aina fulani ya virusi ambavyo kitaalamu vinaitwa herpes viruses.

Inapotokea ukapata maambukizi ya virusi hivi, vinabaki kwako na baada ya muda vinatengeneza vidonda na malengelenge mdomoni.

Wakati mwingine pia ni kawaida kutokwa na vidonda vidogo vidogo nje ya mdomo baada ya maumivu makali ya kichwa, uchovu kupita kiasi, homa, sababu za kisaikolojia na hasa kuwa na wasiwasi, na kupigwa na jua kwa muda mrefu.

Vidonda vinavyotokana na sababu kama hizi hutoweka vyenyewe baada ya muda, lakini kama vinajitokeza mara kwa mara na vinadumu kwa muda mrefu, ni vyema kumuona daktari ili kupata tiba.

Chanzo: mwananchi.co.tz