Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

UNDP yakabidhi vifaa tiba

Dcd0aaf6e0448f1758945826f6247d03 UNDP yakabidhi vifaa tiba

Fri, 4 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

WIZARA ya Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia na Watoto imepokea vifaa tiba kutoka Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) vitakavyosaidia kukabiliana na maradhi ya kuambukiza na yasiyoambukiza.

Akikabidhi vifaa hivyo Meneja Uendeshaji wa UNDP, Jeremiah Mallongo katika Ofisi ya Wizara hiyo Mnazi mmoja, alisema wanatambua juhudi kubwa za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kupanga, kuratibu na kutekeleza mpango wa tahadhari katika kukabiliana na magonjwa hayo.

Alisema vifaa hivyo vitasaidia katika kupambana na kudhibiti maradhi ya kuambukiza ambayo yanarejesha nyuma soko na mfumo wa utalii na kuzorotesha biashara hiyo muhimu ya kukuza uchumi wa nchi.

''Shirika la UNDP limejipanga vizuri kusaidia maendeleo ya sekta ya afya kwa wananchi wa Zanzibar na kupambana na maradhi yasiyoambukiza ambayo yamekuwa chanzo cha vifo vingi vya wananchi wa Unguja na Pemba,'' alisema.

Alisema vifaa hivyo gharama zake ni Sh milioni 271.5 vinavyojumuisha vifaa vinavyotumika katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU), pamoja na vifaa vya kusaidia kupumua kwa wagonjwa wenye matatizo ya pumzi na dawa mbalimbali yakiwemo kwa wagonjwa wa kisukari.

Aidha, alisema shirika hilo litagharamia ufungaji wa vifaa tiba vyote katika sehemu ambazo wizara itaamua vifungwe mara baada ya uainishaji wa maeneo hayo utakapofanyika ikiwemo katika hospitali zilizopo vijijini.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu ambaye pia ni Mkurugenzi wa Tiba wa Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia na Watoto, Juma Salum Mbwana alisema wamepokea msaada wa vifaa hivyo na kuhakikisha watavitumia vizuri kwa lengo la kujikinga na magonjwa na wananchi waishi katika hali ya salama na amani.

Aidha, alisema vifaa hivyo ambavyo baadhi vitawekwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Abeid Amani Karume, vitasaidia katika hali ya usalama kwa watalii watakaoingia nchini na kuwakumbusha kufuata taratibu zilizowekwa ili kuhakikisha mikusanyiko inakuwa ya amani katika kipindi chote watakachokuwepo Zanzibar.

''Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia na Watoto tunatoa shukrani zetu za dhati kwa Shirika la UNDP kwa msaada huu mkubwa ambao utasaidia kudhibiti maradhi ikiwemo yanayoambukiza na yale yasiyoambukiza ambayo yamekuwa yakisababisha vifo kwa wananchi wengi,'' alisema.

Chanzo: habarileo.co.tz