Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

UCSAF kuwezesha tiba mtandao  

Fc52511432ee3fa26c7bc02baf3469c1 UCSAF kuwezesha tiba mtandao  

Sat, 13 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

SERIKALI kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), imekuja na mradi wa tiba mtandao ambao daktari bingwa atamhudumia mgonjwa kwa njia ya mtandao.

Hayo yalielezwa jana jijini Dodoma na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk Faustine Ndugulile wakati wa kikao cha Wizara hiyo na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu ambacho kilikuwa kikipokea taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya UCSAF.

Alisema kupitia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), madaktari wa kibingwa watatoa huduma kwa njia hiyo.

Alifafanua kuwa kusudio la serikali ni kuhakikisha sekta hiyo inakuwa njia kuu ya uchumi kama ilivyo barabara na viwanda.

“Huko tunakokwenda kupitia Mkongo sekta hii itakuwa ni moja ya zinazotengeneza uchumi, na majukumu yetu ndani ya miaka mitano ni kuhakikisha tunafikisha mkongo wa taifa kwa asilimia 85,”alisema.

Alieleza kuwa wizara hiyo hivi sasa inatengeneza mazingira wezeshi juu ya matumizi ya Tehama, ndani ya serikali ili taasisi za serikali ziwasiliane kwa njia za mawasiliano.

“Kwa sasa nchi imeingia uchumi wa kati hivyo kama nchi inapaswa kuendana na dunia kuhusu uchumi wa kidijitali biashara mtandao na mapinduzi ya viwanda," alisisitiza Ndugulile.

Katika kikao hicho, wajumbe wa kamati hiyo walipata fursa ya kuuliza na kushauri kuhusu suala la mawasiliano na wengi walisisitiza juu ya umuhimu wa mfuko huo kuhakikisha maeneo mengi hasa ya vijijini yanafikiwa na mawasiliano ipasavyo.

Mbunge wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu (CCM), alipongeza mfuko huo kwa kupeleka elimu shuleni kuhusu na Tehama na hivyo kurahisisha mawasiliano.Alishauri wakandarasi wanaopewa kazi ya kujenga minara kukamilisha kazi hiyo kwa wakati kwa mujibu wa makubaliano.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Seleman Kakoso ambaye ni mbunge wa Mpanda Vijijini (CCM), alisema wabunge watahakikisha wanashirikiana na serikali kuhakikisha mfuko huo unaimarika na kufikia malengo yake.

Awali, akiwasilisha mada katika semina hiyo, Mtendaji Mkuu wa UCSAF, Justina Mashaba, alisema mradi wa tiba kwa mtandao upo katika hatua za awali.

Alisema kwa kuanzia mfuko huo unatengeneza mtandao na daktari aliyepo kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) anaweze kumhudumia mgonjwa aliyepo hata nje ya mkoa wa Dar es Salaam.

“Wale wataalamu bingwa, kwa mfano unamtafuta Profesa Janabi mtaalamu wa moyo, kuna mtanzania yupo Kigoma anahitaji huduma sio lazima kusafiri kufuata huduma za moyo tunataka kuunganisha kupitia mtandao,"alisema.

Pia alisema mfuko huo umekuwa ukitekeleza miradi mbalimbali ikiwamo upelekaji mawasiliano viijijini kupeleka vifaa vya mawasilano kwenye shule za umma.

Chanzo: habarileo.co.tz