Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tuwape imani wataalamu wa afya walio mafunzoni

48960 Pic+wataalamu

Wed, 27 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Afya ni kitu cha muhimu kwa kila mwanadamu kwa kuwa ndiyo msingi unaoweza kuzibeba nyanja zote za maendeleo kwa mtu mmoja mmoja na jamii kwa ujumla.

Unapokuwa umelala kitandani kwa kuugua na hakuna kipato unachoingiza ni hasara inayochangia kurudisha nyuma maendeleo.

Hivyo kila mtu anapaswa kutunza afya yake kwa hali na mali ikiwa ni kwa kuchukua tahadhari dhidi ya maradhi au kutibu ugonjwa unaokukabili kabla haujafikia katika hatua mbaya inayoweza kugharimu sehemu ya muda, mali au maisha yako.

Hospitali, zahanati au vituo vya afya ni maeneo muhimu tunayoyategemea ili kuhakikisha afya zetu zinakuwa sawa, na wataalamu wa afya ndio watu pekee tunaowaamini kutibu na kutatua changamoto za kiafya.

Kutokana na umuhimu wa sekta hiyo ni muhimu kuhakikisha inaendelea kuimarishwa na kuboreshwa kikamilifu.

Nimewahi kusikia watu wakilalamikia utaratibu kwa baadhi ya hospitali kutumia wanafunzi wa taaluma za kitabibu kutibu wagonjwa, jambo ambalo kimsingi linaweza lisiwe tatizo kwani ni moja ya njia za msingi zinazofanikisha kupatikana wataalamu wabobezi hapo baadaye.

Hata hivyo, ni muhimu umakini ukaongezwa hasa kwa kuwapa uangalizi wa karibu zaidi wataalamu watarajiwa wa fani za tiba ili waive na kuja kuisaidia nchi hapo baadae.

Nimewahi kushuhudia mtoto ambaye alipata ulemavu wa kushindwa kukunja mguu kwa kile kilichodaiwa ni kuchomwa sindano vibaya na mtaalamu ambaye hakuwa na uzoefu wa kutosha.

Niliwahi kumsikia mama mmoja akisema ukifika wakati wa kumpeleka mwanae hospitali huwa anawaza sana kutokana na hofu kwamba huenda watakaomhudumia ni wanafunzi wasio na utaalamu wa kutosha, lakini kwa kuwa hulazimu kufanya hivyo kwa kuwa hakuna namna nyingine.

Kimsingi tunaweza kuona jambo hili si kubwa, lakini naamini kwa waliopata madhara kwa kutotibiwa kiweledi wanaona jinsi ilivyowagharimu kwa namna mbalimbali.

Hata hivyo, naamini hatuwezi kukwepa kuwatumia wataalamu wetu walioko mafunzoni ili kuwapa uwezo wa kukuwa kitaaluma ili baadae waje kuwa wabobezi kwa kutoa tiba kwa vitendo. Jambo la muhimu ni kutekeleza majukumu yao wakiwa karibu na wataalamu waliofuzu na wenye uzoefu.

Yawezekana yapo makosa yanayosababishwa na wataalamu kutokuwa na uzoefu wa kutosha kazini lakini naamini sio mengi kiasi cha kuwatazama kwa namna tofauti.

Mkoa wa Mbeya ni moja ya maeneo yenye zahanati, vituo vya afya na hospitali nyingi zinazotoa huduma muhimu za tiba, hivyo bila shaka wataalamu wanafunzi pia huletwa kujifunza kwa vitendo.

Rai yangu tuendelee kuwapa ushirikiano wa kutosha kuanzia wagonjwa wanaokwenda vituoni na hospitali na hata wataalamu wanaowasimamia.



Chanzo: mwananchi.co.tz