Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tupime shinikizo la damu kusudi tulinde figo zetu

9797 Figo+pic TZWeb

Sun, 24 Jun 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Shinikizo la juu la damu ni tatizo linaloonekana kuwakabili Watanzania wengi.

Sehemu ninakofanyia kazi, kila wagonjwa wawili kati ya 10 huwa wanakabiliwa na tatizo la shinikizo la damu kuwa juu. Kwangu mimi hali hii inaongeza wasiwasi tofauti na ilivyozoeleka awali.

Hata hivyo, hali hii inajitokeza wakati ambao Watanzania wanakabiliwa na changamoto nyingine ya uelewa mdogo kuhusu tatizo hilo.

Moja ya dhana hiyo potofu ni kwamba, wanaamini mtu anayeugua shinikizo la damu anapoanza kutumia dawa kwa kipindi cha muda mfupi, tatizo hilo linakoma mara moja.

Mara kadhaa ninawaeleza wagonjwa kuwa wakati shinikizo lao la damu likipanda, wanameza dawa na kupata nafuu kwa maana kwamba, dalili za tatizo hilo kama vile maumivu ya kichwa, kupapatika kwa moyo hutoweka.

Bahati mbaya wagonjwa wa namna hii waliositisha utumiaji wa dawa bila kujua kuwa, kufanya hivyo wanalikaribisha upya tatizo hilo na linapojirudia tena, linaweza kuharibu baadhi ya viungo kama vile figo na ubongo.

Ukweli ambao watu wanapaswa kuujua

Jambo ambalo watu wanapaswa kulijua ni kwamba shinikizo la juu la damu hutokea pale ambapo msukumo wa damu katika mishipa unakuwa juu kwa muda mrefu.

Muda mwingi hali hii inapotokea hakuna dalili yoyote inayojitokeza na ndiyo sababu kwanini watu wengi wanaweza wasijitambue kama wanakabiliwa na tatizo hilo.

Kila mara nilipofikiria kuhusu mada hii, nakumbuka kisa kimoja cha mgonjwa mmoja aliyekuja na kuniuliza “Daktari mbona pressure yangu iko juu? Na mimi siumwi?

Kama nilivyoeleza mwanzo kuwa shinikizo la damu linaweza lisiwe na dalili na mara nyingi ninachowaeleza wagonjwa wangu ni kuhakikisha wanajenga tabia ya kufuatilia mara kwa mara mwenendo wa shinikizo lao la damu, kula vizuri kiafya na kujiepusha na mwenendo wowote hatarishi ambao unaweza kusababisha kupanda kwa shinikizo la damu.

Jambo lingine baya ni kwamba, wakati wagonjwa wanapoanza kuonyesha dalili, inawezekana tayari wameingia katika matatizo mengine ya kiafya.

Nyakati zimebadilika

Zamani kulikuwa na dhana kwamba shinikizo la damu lilikuwa ni tatizo lililowakumba wazee na watu wanene. Lakini tafiti zimethibitisha kuwa hilo siyo kweli. Katika miaka ya karibuni imedhihirika kuwa shinikizo la juu la damu linaweza kujitokeza katika makundi ya watu wenye umri wowote.

Katika kampeni ya upimaji afya bure iliyofanyika hivi karibuni katika viwanja vya Mnazi mmoja jijini Dar es Salaam, watu 14,000 walipimwa na asilimia 23 kati yao waligundulika kuwa na shinikizo la damu.

Wengi wao walikuwa hawajui chochote kama walikuwa na hali hiyo. Sasa ni mambo gani yanaweza kuwakumba watu wa namna hii. Mtu mwenye historia ya kuwa na shinikizo la juu la damu bila kupatiwa matibabu, yuko hatarini kukumbwa na ugonjwa wa figo. Hiyo ni sehemu tu ya matatizo mengine ikiwamo kiharusi.

Ugonjwa wa figo hatimaye unaweza kusababisha figo lishindwe kufanya kazi. Kwa maneno mengine ni kusema kwamba kushindwa kudhibiti shinikizo la damu ni kuangamiza taratibu figo na viungo vingine.

Nafanya kazi katika kituo ambacho wagonjwa wa figo wamekuwa wakifanya dialysis ( usafishaji wa damu) na jambo la kutia wasiwasi zaidi ni kuona vijana, watu wazima wakija na matatizo yanayohusiana na figo.

Zaidi ya asilimia 90 ya shinikizo la juu la damu ni hali ya kawaida kwa maana kwamba linatokana na mfumo usio rasmi wa maisha na sababu nyingine za kijenetiki. Lakini tumebaini kuwepo kwa mwenendo wa ambao unachangia hali hii kama vile utumiaji wa chumvi kupita kiasi kwenye vyakula, unene na matumizi kupita kiasi ya pombe na sigara.

Nini kinatokea kwa figo wakati mtu anaposhindwa kudhibiti shinikizo la damu?

Figo zako ni viungo viwili vinavyofanya kazi ya udhibiti ndani ya mwili vilivyoko sehemu ya nyuma. Kazi yake kubwa ni chombo kinachochukua jukumu la kuchuja na kuondoa vitu vya mfumo wa majimaji ndani ya mwili.

Inapotokea shinikizo la damu halijadhibitiwa kwa kipindi kirefu (watu hawajui kama wanakabiliwa na tatizo hilo au watu kutozingatia kutumia dawa) mishipa midogo ya damu iliyopo kwenye figo inaharibiwa.

Katika mazingira haya, mishipa hiyo inakosa uwezo wa kupokea oksijeni na hivyo kufanya figo kupoteza uwezo wa kuchuja damu na kuanza kutengeneza vitu vinavyoharibu mwili.

Katika mzunguko huo, figo inakufa na hatimaye sasa mgonjwa analazimika kuingia hatua ya kusafisha damu kila wiki mara tatu katika kipindi chote cha maisha yake ili aweze kuendelea kuishi au apandikizwe figo.

Usafishaji wa damu au upandikizaji wa figo mambo yote hayo yana gharama kubwa.

Na kama tunavyoelezwa kuwa kinga ni bora kuliko tiba.

Kwa ujumla, Watanzania wengi wapo katika hatari ya kukumbwa na shinikizo la juu la damu kutokana na mtindo wa maisha na ulaji mbovu usiozingatia afya na ongezeko la karibuni la ugonjwa wa figo.

Kwa dhati kabisa, nakisihi kizazi cha sasa kuchukua hatua zaidi juu ya kile wanachokula, kufanya mazoezi na kuifanya miili yao iwe yenye afya njema.

Ni vema kufuatilia kwa ukaribu afya ya moyo. Uwapo wa shinikizo la juu la damu lililosababishwa na matatizo mengine ya kiafya yaliyodumu tangu mwanzo kama vile shinikizo la damu, lilisababishwa na ujauzito, maradhi ya moyo na maradhi ya figo. Hata hivyo, baadhi ya maradhi haya yanayosababisha shinikizo la juu la damu yanaweza kudhibitiwa na shinikizo la damu la mgonjwa likashuka na kuwa sawa.

Kwa hiyo ni muhimu kujua hali ya mzunguko wako wa damu na kisha chukua hatua.

Dk Essajee ni daktari katika idara ya wagonjwa wa dharura, Hospitali ya Regency.

Chanzo: mwananchi.co.tz