Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

‘Tumieni Folic Acid kuepushia watoto mgongo wazi’

84fe3c265e352f61589ea7fa1037249e.jpeg ‘Tumieni Folic Acid kuepushia watoto mgongo wazi’

Mon, 15 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WANAWAKE na wanaume wanaotarajia kupata watoto wanatakiwa kutumia vidoge vya Folic Acid kwa miezi mitatu kabla ya ujauzito na kuendelea ili kuepuka kuzaa watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi.

Hatua hiyo inatokana utafiti uliofanyika kuhusu sababu za ongezeko la ulemavu huo na kubainisha kuwa, hali hiyo kwa watoto inatokana na wazazi kutotumia vidonge hivyo pamoja na mbogamboga na matunda.

Akifungua semina ya waandishi wa habari wanawake pamoja na wanawake wenye watoto wenye ulemavu huo katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Abel Makubi, Katibu wa Afya Mkoa wa Dar es Salaam, Sister Mathew, alisema kumekuwa na ongezeko la tatizo hilo, hivyo Mkoa wa Dar es Salaam utahakikisha dawa hizo zinakuwepo katika vituo vyote vya afya ili zipatikane kwa urahisi.

Semina hiyo iliandaliwa na Shirika la Global Alliance for Improved Nutrition (Gain) na Chama cha Wazazi wa Watoto wenye Kichwa Kikubwa na Mgongo Wazi (ASBAHT).

“Jamii haina uelewa kuhusu tatizo la vichwa vikubwa na mgongo wazi na kuona kama ni ushirikina au balaa, hivyo ni vema kuhakikisha wanawake na wanaume wakapata dawa hizo na kuzitumia,”alisema.

Alisema wapo baadhi ya wanawake wanaopewa dawa hizo, lakini hawazitumii kwa madai kuwa zinanuka na kwamba, hazina ladha.

Alisema dawa hizo ndizo jawabu la tatizo hilo kubwa la kuzaa mtoto anayehitaji msaada wa mama kwa muda mrefu.

Dk Consolata Shayo kutoka Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI), alisisitiza ulaji wa vidonge vya Folic Acid kwa miezi mitatu hadi sita kabla ya kupata ujauzito na kueleza kuwa, dawa hizo hazina madhara kwa binadamu, bali huimarisha afya.

Alitoa takwimu kuwa watoto watatu kati ya 100 wanaozaliwa wanakutwa na tatizo hilo huku hospitali hiyo ikifanya upasuaji wa watoto 200 hadi 300 kwa mwaka.

Ofisa Maendeleo ya Jamii wa Chama cha Wazazi wa Watoto wenye Kichwa Kikubwa na Mgongo Wazi (ASBAHT), Theresia Jacob, alisema kumekuwa na ongezeko la watoto wanaozaliwa na tatizo hilo kwani kila wiki watoto wapya watano mpaka sita wamekuwa wakifika katika chama hicho.

Chanzo: www.habarileo.co.tz