Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tumia mafuta ya maboga kulinda, kutibu ngozi yako

13496 Mafuta+pic TanzaniaWeb

Fri, 24 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Umewahi kufikiria kuwa boga lina mafuta safi ya yanayoweza kurejesha afya ya ngozi? Si boga pekee hata majani ya chai maarufu kama green tea nayo hutumika kama malighafi katika kutengeneza mafuta yakichanganywa na viambata vingine.

Maboga na green tea yakichanganywa na malighafi nyingine hutengeneza mafuta ya mwili yanayozuia na kutibu maradhi tofauti ya ngozi na kuifanya ya kuvutia.

Kwa kuitambua siri hiyo, Beatrice Mkama, mjasiriamali mdogo jijini Dar es Salaam ameamua kuitumia fursa hiyo kwa kutengeneza mafuta kwa ajili ya watu wenye matatizo ya ngozi huku akijiongezea kipato.

Amasema mafuta hayo hutibu maradhi kadhaa kama vile mapunye, mba, harara na kuondoa muwasho. Husaidia kutibu chunusi, tetekuwanga, utangotango na fangasi za kila aina.

Pamoja na hayo, Beatrice nasema: “Mafuta haya huondoa harufu mbaya miguuni na kufanya ngozi ya mtumiaji kuwa nyororo.”

Licha ya majukumu yake ya ukatibu mutahsi katika ofisi ya wakili wa kujitegemea, Beatrice anasema alijifunza utengenezaji wa bidhaa hizo kutoka kwa mjasiriamali mwenye ujuzi kisha uzalishaji kwa mtaji wa Sh74,000 tangu Mei.

Kwa muda wake wa ziada anaofanya shughuli hii hujiongezea kipato. Kwa kipindi alichojishughulisha na uzalishaji huo, anasema mtaji wake umekua hadi Sh2 milioni.

Kwenye mafuta yatokanayo na maboga, anasema hutumia nazi pia katika utengenezaji huku yale ya green tea akichanganya na mafuta ya mzeituni maarufu kama olive oil na mchachai.

“Kwa wiki huwa nazalishaji lita nne kwa kila aina ya mafuta. Kila lita nne hutoa chupa 32 ambazo kila moja huwa naiuza kwa Sh10,000,” anasema Beatrice.

Anasema soko la mafuta hayo ni la uhakika na hajaweza kuwafikia wateja wote kutokana na uzalishaji wake kuwa mdogo na ukweli kwamba hana mawakala mikoani.

Kutokana na matangazo anayoweka kwenye mitandao ya kijamii huwa anapata oda kutoka maeneo tofauti nchini lakini ni katika mikoamitano pekee ambako ana mawakala wanaomsaidia kusambaza mafuta yake.

Anasema kati ya wateja hao wapo wanaohitaji ujazo mkubwa ambao bado hajaanza kufunga kutokana na wateja wengi kuwa wa kipato cha kawaida.

“Niliweka ujazo mdogo ili kila mtu amudu gharama lakini katika mikakati yangu nitaanza kufungasha katika ujazo mkubwa pia ili kuwafikia wanaohitaji,” anasema Beatrice.

Katika malengo yake ya muda mrefu Beatrice anasema anatamani kuona bidhaa zake siku moja zinapatikana katika kila duka nchini na kutumiwa na watu wengi kama zilivyo za wafanya biashara wakubwa akimtolea mfano Said Bakhresa.

“Ili kufanikisha hilo nimeanza kutafuta mawakala watakaonisaidia kuuza mafuta haya katika mikoa ambayo bado sijaifikia,” anasema Beatrice.

Chanzo: mwananchi.co.tz