Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

‘Tumezingatia mwongozo WHO chanjo corona’

02da75cfede1a6e355b88bd93ff1a6d8 ‘Tumezingatia mwongozo WHO chanjo corona’

Thu, 22 Jul 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

SERIKALI imesisitiza kuwa chanjo ya corona nchini itatolewa kwa hiyari kwa kuzingatia mwongozo wake ambao umezingatia uliotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO).

Akizungumza na HabariLEO jana, Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Aifello Sichalwe alisema serikali ilitoa mwongozo kuwa chanjo ya corona ni ya hiyari kwa anayehitaji.

Alisema hayo wakati gazeti hili lilipotaka ufafanuzi baada ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe kusema kuwa utaratibu wa serikali wa kutoa chanjo hizo kwa hiyari unapingana na mwongozo wa WHO na akataka utangazwe uamuzi kuwa chanjo ya corona iwe ya lazima.

"Kama mimi nikibeba corona na nikakuambukiza wewe au nikamuambukiza mwingine ambaye hana chanjo ina maana naendelea kusambaza ugonjwa ule, kwenye nchi za wenzetu chanjo ni lazima kwa watu wote yakiwemo makundi ya wazee, waathirika na madaktari wanaotoa huduma za tiba," alisema Mbowe alipozungumza na waandishi wa habari jijini Mwanza.

Dk Aifello Sichalwe alisema kwa mujibu wa tamko la WHO la Aprili 13 mwaka huu, ili chanjo iwe lazima lazima masuala kadhaa yazingatiwe ikiwamo umuhimu na uwiano.

Alisema WHO ilisema chanjo ya lazima inapaswa kuzingatia umuhimu na uwiano katika kufikia lengo la afya ya jamii ikiwamo malengo ya kijamii na kiuchumi yaliyotambuliwa na mamlaka halali ya afya ya umma.

Alisema ulazima huo pia unapaswa kuthibitishwa kwa kuzingatia misingi ya kimaadili na kuheshimu uhuru wa mtu kujiamulia na katika hilo, elimu kwa umma ni muhimu badala ya kulazimisha.

Alisema WHO ilitaja jambo la pili kuwa ni lazima uwapo ushahidi wa kutosha wa usalama wa chanjo husika.

“Katika hilo WHO ilisisitiza kuwapo takwimu za kutosha kuonesha kwamba chanjo ya lazima ni salama kwa watu waliokusudiwa kupewa na endapo taarifa za usalama wa chanjo unakosekana au kama uwezekano wa kutokea madhara ya chanjo ni mkubwa kuliko kutokuwa na chanjo, ulazima huo unakuwa haujazingatia maadili.”

“WHO pia inataka uwapo ushahidi wa kutosha kama chanjo itakuwa na ufanisi na kuleta matokeo yaliyokusudiwa kwa watu wanaopaswa kupewa chanjo ya lazima,” alisema.

Dk Sichalwe alisema shirika hilo limetaja ugavi ni jambo jingine la kuzingatiwa pale chanjo ya lazima inapotakiwa.

Alisema kwa mujibu wa WHO, ili ulazima uzingatiwe, usambazaji wa chanjo iliyoidhinishwa unapaswa kuwa wa kutosha na wa kuaminika na chanjo zitolewe bure kwa waliokusudiwa.

Alisema imani ya umma au jamii pia ni miongoni mwa mambo ya kuzingatiwa, ambapo katika hilo, watunga sera wana wajibu wa kuzingatia matokeo ya chanjo ya lazima na imani ya jamii kwa chanjo hiyo.

Alisema jambo la sita la kuzingatiwa ni michakato ya kimaadili ya kufanya uamuzi. “WHO inasisitiza uwapo wa uwazi na uamuzi wa hatua kwa hatua wa mamlaka halali za afya ya umma. Jambo hilo linapaswa kuwa msingi wa maadili katika kufanya uamuzi kuhusu chanjo ya lazima na jitihada za busara zinapaswa kufanywa kwa kushirikisha wahusika na wadau sahihi,” alisema.

Alisema kwa mujibu wa mwongozo wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kuhusu ya chanjo ya Covid 19, chanjo hizo ni za hiyari, zitatolewa bure na kabla ya mtu kuzipata atasaini fomu maalumu.

Alisema mwongozo huo uliotolewa mwezi huu umebainisha chanjo zilizopewa kipaumbele zitumike nchini ni BioNTech/Pfizer BNT162b2, Moderna mRNA 1273, Novavax NVX-CoV2373 na Johnson & Johnson (Janssen) Ad26.

Mwezi uliopita, Rais Samia Suluhu Hassan alipokuwa akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam, alisema uongozi wa juu wa Tanzania umekubaliana kupitia kikao cha Baraza la Mawaziri kuwa chanjo ya corona itakuwa ya hiyari.

Alisema Tanzania ilituma maombi ya kujiunga na Mpango wa Chanjo kwa Nchi Masikini (Covax).

Hivi karibuni wakati akiwa njiani kutoka Dodoma kwenda Morogoro, Rais Samia alihimiza wananchi wasiupuuze ugonjwa wa covid-19 bali wajikinge wasipate maambukizi ya virusi vya corona vinavyosababisha ugonjwa huo.

Kwa mujibu wa mwongozo wa serikali wa matumizi ya chanjo ya covid 19, serikali inakusudia kulinda watu wake wote dhidi ya ugonjwa huo kwa kuchukua hatua zinazokubalika za kisayansi, pamoja na utoaji salama wa chanjo zenye ufanisi na zenye ubora.

Aidha, mwongozo huo umetaja makundi yaliyopewa kipaumbele kupata chanjo hizo kuwa ni watoa huduma za afya wanaoshughulika moja kwa moja na wagonjwa wa corona, watu wenye matatizo ya afya kuanzia umri wa miaka 18 na kuendelea na watu wazima kuanzia umri wa miaka 45 na kuendelea.

Wengine ni wafanyakazi katika maeneo kama bandarini, vikosi vya ulinzi na usalama, wahadhiri na walimu wa shule za msingi na skondari, makundi maalumu kama vile wasafiri wa kimataifa, mahujaji, wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa na wanadiplomasia, wasio wakazi na wafanyakazi muhimu kutoka sekta ya utalii.

Mwongozo huo umesisitiza kuwa, chanjo dhidi ya covid-19 pamoja na kwamba itakuwa ni ya hiyari, serikali itaendesha kampeni na kuisambaza kwa makundi mbalimbali na itapatikana katika zahanati, vituo vya afya na hospitali.

Kwa makundi muhimu yaliyobainishwa, chanjo hiyo itatolewa bure isipokuwa kwa wasafiri ambao watahitajika kuchangia gharama.

Aidha, mwongozo huo umebainisha kuwa, pindi chanjo hizo zitakapowasili, umma utatangaziwa na mahali zitakapopatikana, huku ukiwekwa utaratibu kwa watakaohitaji kujisajili kwenye mtandao au kwenye vituo chanjo hizo zitakapopatikana na kupangiwa siku ya kuchanjwa na mahali.

Hivi karibuni, kupitia Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Profesa Abel Makubi ilisema serikali imeagiza aina nne ya chanjo za kujikinga na corona na zinaotarajiwa kuanza kutumika ndani ya miezi mitatu au minne ijayo.

Chanzo: www.habarileo.co.tz