Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tume yashtushwa wagonjwa kuzuiwa

Mhina.webp Tume yashtushwa wagonjwa kuzuiwa

Fri, 15 May 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

TUME ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imeeleza kusikitishwa na taarifa ya vitendo vinavyofanywa na baadhi ya madaktari na wauguzi wa Hospitali ya Rufani ya Mkoa ya Mwananyamala jijini Dar es Salaam, vya kuwanyanyapaa na kuwasumbua wagonjwa wanaoenda kupata matibabu.

Aidha, Tume hiyo imesema wagonjwa hao wanatakiwa kufanya vipimo vya virusi vya corona kabla ya kuanza kupata matibabu.

Taarifa ya Tume iliyotolewa na Mwenyekiti wake, Jaji mstaafu Mathew Pauwa Mhina Mwaimu, ilieleza kuwa:

“Tume imesikitishwa na jambo hilo kwa sababu kila mwananchi ana haki ya kufurahia haki ya afya kwa kupata matibabu mazuri na ya uhakika. madaktari na wauguzi wanapaswa kutambua kuwa sio kila mgonjwa ana maambukizo ya corona.

“Tume inaamini vitendo vya namna hiyo ni ukiukwaji wa haki ya afya kwa wananchi, na vinaweza kusababisha wagonjwa kupoteza maisha.”

Hata hivyo, THBUB imempongeza Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Ummy Mwalimu, kwa kuchukua hatua za haraka za kukemea vitendo hivyo vya baadhi ya madaktari na wauguzi, ambavyo vinaweza kuchafua taswira nzuri ya sekta ya afya na jitihada mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali.

Kadhalika, Tume inaiomba Serikali iendelee kuhakikisha hospitali zinaendelea kutoa huduma nzuri kwa wagonjwa ili kuepusha malalamiko yasiyo ya lazima.

Aidha, Tume imeiomba Serikali kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini chanzo cha vitendo hivyo vinavyofanywa na baadhi ya madaktari na wauguzi ili kuvitafutia ufumbuzi wa haraka.

ALICHOBAINI WAZIRI UMMY

Hivi karibuni, Waziri Mwalimu, alifanya ziara ya kushtukiza katika Hospitali ya Mwananyamala na kukuta wagonja wengi wakisubiri huduma baada ya kupigwa danadana kwenye hospitali mbalimbali za Jiji la Dar es Salaam na kutakiwa kupima corona kwanza kabla ya huduma.

“Tunaaambiwa tuende Palestina saa nane usiku hawapigia X ray, tumerudi Magomeni wanatuambia mpelekeni mgonjwa wenu nyumbani, tunakuja naye hospitalini Magomeni wanatuambia tuende tena Mwananyamala, tunakuja hapa tunaambia turudi tena Magomeni,mgonjwa wtu huyu hapa na hali yake ni mbaya,” alisema mmoja wa ndugu wa mgonjwa.

Mwingine alimwambia Waziri: “Tangu saa 12 asubuhi tuko hapa hatujapata huduma, tunaomba huduma wangetuokoa sisi turudi nyumbani tunawatoto ili tusijazane hapa.”

“Tulifika hapa baba ana sukari wakasema hawana kipimo cha sukari, tumenunua kipimo wakakataa, wakasema hawamshiki mgonjwa hadi apimwe corona, tukaaomba tuelekezwe pa kumpima corona, lakini hawajatoa jibu, tangu asubuhi mgonjwa wetu yupo hapa hajapata huduma,” alisema mmoja wa ndugu.

Kutokana na vilio hivyo, Waziri Ummy alionyesha kukasirika na kumwambia “Mganga Mkuu hiki mnachokifanya mjue mtakuja kuua watu, mtu ameata ajali tangu jana usiku hadi sasa hajapata huduma, mtu ana sukari unamwambia apime kwanza corona.”

Alisema madaktari na wahudumua wa afya wanapaswa kuendelea kutoa huduma kwa uangalifu mkubwa kwa kuwa maisha lazima yaendelee.

“Watoa huduma za Afya wa Serikali na binafsi acheni kunyanyapaa wagonjwa, mgonjwa amekuja na tatizo la sukari mtibuni sukari, mnaleta ya corona… hayo ni mambo mengine, mtamuua mtu si kwa sababu ya corona bali kwa sababu hamkumpa matibabu ya sukari,” alisema Waziri.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live