Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tumbaku inavyowaathiri zaidi wanawake, watoto

Wed, 26 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wakati takwimu zikionyesha kuwa asilimia 16 ya Watanzania wanatumia tumbaku, Shirika la Afya Duniani (WHO) limebainisha kuwa waathirika wakubwa ni wanawake na watoto.

WHO imesema njia sahihi zisipotumika katika kuzuia matangazo ya tumbaku na kutoa elimu, ukuaji wa maradhi yasiyoambukiza utaongezeka.

Mratibu wa Programu ya Usalama Barabarani kutoka Shirika la Afya Duniani, Merry Kessi alisema juzi kuwa kuna vifo milioni 7.2 duniani kila mwaka vinavyosababishwa na matumizi ya tumbaku.

“Kati ya vifo hivyo wanaoathirika ni wale wanaopokea moshi utokanao na tumbaku ambao ni wanawake na watoto, wengi hufariki kwa saratani mbalimbali,” alisema Kessi.

Mtaalamu wa maradhi ya saratani kutoka Hospitali ya Ocean Road, Dk Maghuha Stephano alisema kemikali inayotoka kwa mtu anayevuta bidhaa ya tumbaku huwa sumu mbaya zaidi ikipokewa na mtu mwingine.

“Ile kemikali iliyopo kwenye sigara mtu anapokuwa anavuta, ule moshi unaotoka nje ndiyo una sumu nyingi zaidi kuliko ule unaoingia kwa mvutaji,” alisema.

Dk Maghuha alisema mtu anayepokea moshi wa sigara kutoka kwa mvutaji, anaweza kupata matatizo ya kawaida kwenye njia za hewa kama kupaliwa na hata maradhi ya mfumo wa hewa.

“Baada ya muda mrefu, ndiyo anaweza kupata madhara kama ya kuugua saratani ya mapafu, koo na kichwa, lakini pia saratani ya ini na aina nyingine kama ya shingo ya kizazi,” alisema.

Alisema asilimia 99 ya saratani ya shingo ya kizazi hutokana na virusi vya HPV na mwanamke anayevuta sigara au anayepokea moshi wa sigara huwa hatarini zaidi kukumbwa na ugonjwa huo.

Alisema tumbaku ni kisababishi cha saratani karibu za aina zote ukiachilia mbali maradhi ya moyo na kisukari.

Ofisa Mawasiliano wa Wizara ya Afya, Said Makora alisema upo mkakati wa kuangalia namna ya kupunguza kilimo cha tumbaku kwa baadhi ya maeneo yanayoonekana kuathirika zaidi.

“Kanda ya Ziwa na Tabora ni maeneo ambayo tumbaku inalimwa na ukiangalia kuna waathirika wa saratani, tunaangalia mikoa hiyo kuona kama wanaweza kupata mazao mengine mbadala ili kupunguza tatizo, lakini pia kupunguza matangazo ya uvutaji sigara, kuongeza kodi hivi vyote vinashughulikiwa,” alisema.

Wataalamu wanabainisha kuwa uvutaji sigara huathiri mwili kwa njia tofauti.

Hadi sasa kumegunduliwa kemikali zipatazo 7,000 katika moshi wa sigara na 250 kati ya hizo ni sumu na 70 zinasababisha saratani.

Mvutaji mdogo hutumia nusu ya pakiti ya sigara kwa siku na kujikuta akiathiri mwili wake kwa kemikali hizi mara 3,500 kwa mwaka.



Chanzo: mwananchi.co.tz