Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tuchukue tahadhari matatizo ya figo

Fbead5229adb6c2a77bdc198ba530d07 Tuchukue tahadhari matatizo ya figo

Fri, 12 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

LEO Tanzania inaungana na mataifa mengine dunia kuadhimisha Siku ya Afya ya Figo Duniani inayoadhimishwa kila Alhamisi ya Pili ya Mwezi Machi.

Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, maaadhimisho haya kila mwaka yanalenga kuhakikisha jamii inapata elimu endelevu kuhusu ugonjwa wa figo unaogharimu fedha nyingi.

Aidha, inalenga kuelimisha umma mintarafu madhara yatokanayo na ugonjwa huu na hatua zinazopaswa kuchukuliwa kuuzuia na kupambana nao.

Kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni: “Ishi Salama, na Ugonjwa wa Figo,” inayolenga kuhamasisha ushirikishwaji wa mgonjwa wa figo, familia, jamii na marafiki wanaowahudumia waathirika wa ugonjwa huu kuhusu tiba na afya yake ili aishi salama na ugonjwa wa figo alio nao.

Taarifa ya wizara inabainisha kuwa, lengo la Siku ya Afya ya Figo Duniani, pia ni kuongeza uelewa na mwamko wa jamii kuhusu namna ya kukabiliana na dalili za ugonjwa wa figo sambamba na kumwezesha mgonjwa kushiriki kikamilifu kusimamia tiba yake kwa kushirikiana na watoa huduma.

Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonesha kuwa, asilimia 10 ya watu dunia wameathiriwa na ugonjwa sugu wa figo.

Aidha, takwimu zinaonesha kuwa Tanzania inakadiriwa kuwa na wagonjwa sugu wa figo kati ya 4,800 hadi 5,200 wanaohitaji huduma ya kusafisha damu au kupandikizwa figo.

Hii ni idadi kubwa isiyopaswa kufumbiwa macho wala kufanyiwa mzaha na yeyote.

Kimsingi, Watanzania wanapaswa kuchukua hatua za kujikinga ili kuepuka ugonjwa huo hatari ambao kama magonjwa mengine, unapunguza nguvukazi ya nchi na una athari kubwa za kiuchumi.

Ndiyo maana tunasema, jamii itambue na kuchukua hatua kujikinga kwa kuepuka mambo yote yanayochangia watu kupata ugonjwa huo.

Miongoni mwa hayo ni pamoja na kufanya mazoezi, kula lishe bora na kamili, na kunywa angalau lita moja na nusu ya maji kwa siku.

Mengine ni usafi wa mwili, kutokuvuta sigara au kunywa pombe kupita kiasi pamoja na kudhibiti shinikizo la juu la damu, kisukari na maambukizi ya mara kwa mara ya mfumo wa mkojo maarufu kwa jina la UTI.

Tunasema, tukiunganisha nguvu na kila mmoja akawajibika kwa nafasi yake, tutaukabili ugonjwa wa figo.

Jamii ijenge utamaduni wa kufanya uchunguzi wa afya angalau mara moja kwa mwaka ili kunapokuwa na tatizo au dalili, tiba ianze mapema, badala ya kusbiri tatizo likomae.

Sisi tunasema, kuwepo elimu endelevu ya mara kwa mara katika maeneo mbalimbali hata vijijini kwani Watanzania wakipata elimu sahihi na ya kutosha, watashiriki kikamilifu kupambana na tatizo hili.

Chanzo: www.habarileo.co.tz