Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Trilioni za Global Fund kuimarisha sekta ya afya

CHANJO ED (1) Trilioni za Global Fund kuimarisha sekta ya afya

Sat, 26 Feb 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Serikali imesema zaidi ya Sh trilioni 1.66 zilizotolewa na Mfuko wa Dunia wa Kupambana na Ukimwi, Malaria na Kifua Kikuu (Global Fund), zitatumika kuongeza kasi ya kuimarisha sekta ya afya.

Kauli hiyo imetolewa Dodoma jana na Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Profesa Abel Makubi alipokutana na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Idara ya Afrika wa Mfuko wa Dunia wa Kupambana na Ukimwi, malaria na Kifua Kikuu (Global Fund), Linden Morrison pamoja na wataalamu waliopo nchini kwa ziara ya kukagua miradi ya maendeleo ya afya inayotekelezwa nchini.

Makubi alisema vipaumbele hivyo ni ujenzi na ukarabati wa miundombinu katika hospitali za mikoa ambapo mpaka sasa kiasi cha Sh bilioni 27 zimetumika na zinaendelea kutumika kwa ajili ya kuimarisha hospitali kwa kufanya ujenzi katika maeneo mbalimbali nchini.

Alisema ununuzi wa dawa na vitendanishi vya maabara kwa wagonjwa wa Ukimwi, kifua kikuu na malaria pia ni kipaumbele cha pili ambapo zaidi ya Sh bilioni 881 zimetumika na zinaendelea kutumika mpaka 2023.

“Eneo la tatu ni usimikaji wa vifaa tiba katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini hususani katika ngazi ya msingi kuanzia halmashauri, vituo vya afya mpaka zahanati ambapo husimikaji huu umetumia zaidi ya Sh bilioni tisa,” alieleza.

Makubi aliongeza kuwa mfuko huo umewezesha ununuzi wa magari 105 ya kubebea wagonjwa na mpaka sasa zimeanza kutumika Sh bilioni 8.8.

Lakini pia Profesa Makubi alisema eneo muhimu wakati wa Covid-19, Global Fund ilisaidia kununua mitambo ya kuzalisha hewa ya oksijeni katika hospitali za mikoa na baadhi za kanda ambapo bajeti yake imekuwa ni Sh bilioni 14.6.

“Tumeshirikiana nao katika kuimarisha mifumo ya Tehama katika vituo vyetu vya kutolea huduma za afya hasa katika hospitali za mikoa na halmashauri tumetumia Sh bilioni 12.1,” alisema Makubi.

Aliendelea kusema mfuko huo wa dunia utasaidia kujenga uwezo katika sekta ya afya ambapo wametoa ajira za muda mfupi za mkataba ili kuimarisha sekta hiyo kwa kupunguza uhaba wa wataalamu wa afya katika miundombinu iliyojengwa na inayoendelea kujengwa nchini.

Mkuu wa Idara ya Afrika wa Mfuko wa Dunia wa Kupambana na Ukimwi, malaria na Kifua Kikuu (Global Fund), Linden Morrison alisema wataendelea kudumisha ushirikiano uliopo kati yao na Tanzania.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live