Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tofauti ya mazoezi kwa mwenye VVU na Ukimwi

89314 Mazoezi+pic Tofauti ya mazoezi kwa mwenye VVU na Ukimwi

Fri, 20 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Desemba mosi ya kila mwaka ni Siku ya Ukimwi Duniani. Wadau mbalimbali wa sekta ya afya huutumia mwezi huu kufanya kampeni mbalimbali dhidi ya ugonjwa huo usio na tiba.

Katika kuiadhimisha, nitawapa uelewa kuhusu mazoezi anayotakiwa kufanya watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi (VVU) tofauti na mgonjwa wa Ukimwi ambaye yuko mahututi kitandani.

Ieleweke kuwa mtu ambaye anaishi na VVU akiwa mwenye afya njema anaweza kufanya mazoezi kama watu wengine ili kujenga afya ya mwili.

Ingawa ni kweli kabisa mtu anayeishi na VVU mazoezi yake anayotakiwa kufanya huwa na tofauti ndogo sana na yule asiye na maambukizi ya VVU.

Mwenye maambukizi kama alivyo wengine atahitajika kuwa na utamaduni ule ule wa kufanya mazoezi mepesi mara kwa mara katika maisha yake.

Atahitajika kufanya mazoezi yasiyo magumu ambayo ni yale mepesi kama yanavyojulikana Aerobics Exercises.

Sababu ya kutakiwa kufanya mazoezi haya ni kwa sababu hayauchoshi mwili na hutumia kiasi cha wastani cha nishati ya mwili akulinganisha na mazoezi magumu Anaerobics Exercises.

Ikumbukwe kuwa mtu anayeishi na VVU hutakiwa kutunza kiasi cha nishati kilichopo mwilini mwake kwa kuwa anahitaji nishati hiyo kwa ajili ya mambo muhimu ikiwamo kujenga mwili na kinga imara.

Mazoezi mepesi ambayo mtu mwenye VVU anashauriwa kuyafanya ni kutembea, kukimbia kidogo kidogo, kuruka kamba, kuogelea, kuendesha baiskeli na kucheza mziki wa harakaharaka.

Mazoezi mengine anayoweza kuchanganya na hayo ni pamoja na mazoezi ya viungo ikiwamo kupasha mwili moto na kunyoosha misuli na kunyanyua vitu vyenye uzito wa wastani kwa ajili ya kujenga misuli.

Mazoezi mengine ambayo yanawafaa zaidi watu wazima wanaoishi na VVU ni Yoga yenye asili ya Asia ambalo ni zoezi rahisi kujifunza na kulifanya na linafaida lukuki kiafya.

Mazoezi haya yote yanafaida mbalimbali kwa mtu anayeishi na VVU ikiwamo kuimarisha afya ya moyo na mapafu, kujenga misuli imara ya mwili, kuondoa taka mwili kwa njia ya jasho, kudhibiti uzito wa mwili kwa kupunguza mrundikano wa mafuta mwilini.

Faida zingine ni pamoja na kujenga kinga imara, kumpa burudani na kumpa furaha, kumfanya kulala usingizi mnono na kumuepusha na magonjwa ya akili ikiwamo msongo wa mawazo na sonona.

Pia, mazoezi haya yanamuepusha na vishawishi vinavyoweza kumuingiza kujamiiana na wenza wapya na matumizi ya vilevi.

Mazoezi mepesi ni salama kwa mtu ambaye anaishi na VVU na yanaweza kufanyika nusu saa (dakika 30) kwa siku katika siku tano za wiki.

Ili kuwa salama na mazoezi haya atahitajika kula mlo kamili uliozingatia kanuni za afya pamoja na kuwa na utamaduni wa kunywa maji mengi angalau kwa siku glasi 10 au lita 1.5-3 kwa siku.

Chanzo: mwananchi.co.tz