Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tofauti ya kunywa juisi halisi na kula tunda

Juisi Matunda X Tofauti ya kunywa juisi halisi na kula tunda

Mon, 2 Jan 2023 Chanzo: Mwananchi

Mtaalamu wa lishe kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe (TFNC), Elizabeth Lyimo amesema matunda ni kundi mojawapo katika makundi matano ya chakula.

Pia, anasema matunda ni muhimu kuliwa katika kila chakula ili kukamilisha mlo kamili.

Hata hivyo, anapendekeza mtu ale tunda kama tunda ili kupata virutubishi vyote.

Lyimo anasema unywaji wa juisi ya matunda pia ni bora iwapo haitaongezwa ladha au kitu cha kuhifadhi ili kukaa kwa muda mrefu kwa kuwa, ubora wake utafanana na kula tunda zima.

“Juisi ya kutengeneza nyumbani inakuwa na nyuzinyuzi kwa wingi kama ilivyo katika tunda, juisi zinazonunuliwa madukani hazina viwango na ubora kama juisi za kutengenezwa nyumbani kutokana na kuongezwa vihifadhi na ladha,” anasema Elizabeth.

Anasema wakati wa kusaga juisi nyumbani hakikisha unaweka na sehemu ya maganda ya tunda ili kuboresha virutubishi.

Hata hivyo, mtu anashauriwa kula matunda yaliyo katika msimu uliopo ili kupata matunda halisi.

Elizabeth anatoa tahadhari kuwa juisi za madukani ikiwa zitatumiwa kwa muda mrefu humuweka mtumiaji katika hatari ya kuongezeka uzito.

Anasema tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa jamii inatumia kiasi kidogo cha matunda kwa siku tofauti na inavyoshauriwa kitaalamu.

“Kundi hili linajumuisha matunda ya aina mbalimbali kama papai, pera, pensheni, nanasi, peasi, chungwa, chenza, tikiti maji, parachichi, ndizi mbivu, stafeli, topetope na fenesi,” anasema Lyimo.

Mengine ni matunda pori ambayo ni ukwaju, zambarau, ubuyu, furu na mabungo.

“Matunda yana kiwango kikubwa cha vitamini na madini kama vile vitamini A, C pamoja na madini ya potassium, folate na sodiam, hivyo ili kukamilisha mlo kamili, lazima matunda yawepo katika mlo huo,” anasema Elizabeth.

Pia, anasema ulaji wa matunda husaidia kuimarisha mfumo wa kinga mwilini na yana kiwango kikubwa cha makapimlo ambayo humfanya mtu ajisikie kushiba.

Anasema makapimlo yanasaidia kumeng’enya na kuyeyusha chakula na kupunguza hatari ya kupata choo kigumu au kukosa choo.

Kama ulikuwa hujui, kutokana na wingi wa vitamini na madini, matunda yanasaidia kuimarisha kinga ya mwili na hivyo kuuwezesha mwili kujikinga na maradhi mbalimbali.

“Lakini vitamini A, C, D, E, K na selinium husaidia kuondoa chembe chembe haribifu mwilini (free radicals) hivyo hupunguza uwezekano wa kukinga magonjwa, ikiwamo saratani,” anasema Elizabeth.

Pia, anasema iwapo matunda yataliwa kwa wingi yanasaidia uponyaji wa mafua, vidonda, ngozi, meno na fizi.

Hata hivyo, mtaalamu huyo anafafanua kuwa kwa wastani mtu anatakiwa kula gramu 400 za matunda na mbogamboga kwa siku au zaidi.

Angalizo

Usinywe maji mara tu unapomaliza kula matunda kwa sababu matunda mengi yana asidi.

Chanzo: Mwananchi