Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tiba za mifupa, misuli kutolewa hospitali ya Mara Tanzania

87559 Waziripic Tiba za mifupa, misuli kutolewa hospitali ya Mara Tanzania

Sat, 7 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Musoma. Serikali ya Tanzania inatarajia kufungua kitengo cha tiba za mifupa na misuli katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara Kwangwa mara baada ya hospitali hiyo itakapokamilika kujengwa.

Akizungumza baada ya kukagua ujenzi wa hospitali hiyo mjini Musoma leo Jumamosi Desemba 7, 2019, Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema kitengo hicho kitakuwa cha pili kwa ukubwa baada ya Taasisi ya Mifupi Muhimbili (MOI) cha jijini Dar es Salaam.

Amesema lengo la kufungua kitengo hicho ni kutaka kusogeza huduma karibu kwa wananchi hususan wa kanda ya ziwa ambao kwa sasa wanategemea huduma hizo katika Hospitali ya Bugando jijini Mwanza ambayo pia imezidiwa kwa kuwa na wagonjwa wengi kuliko uwezo wake.

Amesema ujenzi wa Hospitali ya Kwangwa ni miongoni mwa miradi ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali ya awamu ya tano ambapo mbali na kutoa huduma za afya lakini pia hospitali hiyo itafungua fursa zaidi za kiuchumi kwa mkoa wa Mara.

Amesema Rais wa Tanzania, John Magufuli aliagiza kutolewa kwa Sh15 bilioni kwaajili ya ujenzi wa hospitali hiyo iliyoanza kujengwa zaidi ya miaka 40 iliyopita huku akionyesha kuridhishwa na ujenzi wa mradi huo unaotekelezwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).

Awali, mkuu wa mkoa wa Mara, Adam Malima amesema hospitali hiyo inatarajiwa kuanza kutoa huduma ya mama na mtoto Februari 2020 baada ya kukamilika kwa ubawa A (wing) wa jengo hilo mapema mwakani.

Malima amsema huduma za rufaa za hospitali ya mkoa wa Mara zinatarajiwa kuanza kutolewa Mei 2020 huku huduma za kibingwa zikitarajiwa kuanza mwisho mwa 2020.

Malima amesema baada ya Rais Magufuli kupokea ombi kutoka mkoa wa Mara kuhusu kusaidia mkwamo wa ujenzi huo, Serikali ilitoa fedha zote Sh15 bilioni kwa mara moja ili kuweza kukamilisha ujenzi huo.

Chanzo: mwananchi.co.tz