Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tiba kwa mfumo wa bima hulea taifa imara

77dd3b8bd444fc18f4efa064067f5f64 Tiba kwa mfumo wa bima hulea taifa imara

Mon, 14 Sep 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

“ WAKATI wa amani ambao ni wakati upo mzima unatakiwa uwekeze na NHIF kwa kukata kadi ya Bima ya Afya na wakati wa vita ambao ni wa maradhi NHIF ni waokoaji kwa kujitibia. Jiungeni na NHIF ili tuwe na uhakika wa matibabu,” Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira.

Na Beda Msimbe ILI kuwepo na utaratibu mzuri wa afya duniani, wataalamu walibuni matumizi ya bima ambapo mtu huchangia mapema na kisha kupata ahueni kwa shida ya tiba anapokumbwa na madhila ya maradhi.

Ni kutokana na ukweli huo, nchi nyingi duniani zimeona umuhimu wa kuwa na bima ya afya kwa wananchi wake ili kila mmoja apate afueni anapopata na madhila ya maradhi.

Suala hili la kuwa na bima ya afya Tanzania halikuanza jana, lilianza baada ya kupata uhuru wakati Israel ilipoombwa kuangalia namna bora ya kusaidia wananchi wa Tanganyika kupata huduma za tiba.

Ilikuwa ni Julai 20, 1962 miezi saba baada ya kupatikana Uhuru kamili (Desemba 9,1961), Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje walitaka msaada wa kiufundi kutoka Israel kuhusu mpango wa bima ya afya kwa waajiriwa.

Mtaalamu kutoka Israel alifanya kazi hiyo Oktoba 1962 na kuja na majibu ambayo yalionesha uwezekano wa kuanzishwa kwa mpango huo.

Pamoja na mapendekezo mpango haukuanzishwa na mwaka 1967 wakati wa kutangazwa kwa Azimio la Arusha ilielezwa wazi kwamba wananchi wa Tanzania watapata huduma za afya na elimu bure.

Hiyo ilikuwa ni sera ambayo iliungana na sera ya vijiji vya ujamaa ya mwaka 1974 hivyo kufanya huduma za afya kutolewa bure na hivyo kwa miaka 40 mfumo wa bima ya afya nchini haukutekelezwa.

lionekana wazi kwamba serikali imezidiwa na sera mpya zikaundwa ili kukabiliana na changamoto mbalimbali zilizokuwa zikijitokeza katika sekta ya afya na elimu na ndipo mwaka 1995 Serikali ya Uingereza iliombwa kuangalia uwezekano wa kuanzishwa bima ya afya ambapo wanachama wake wataingia kwa mujibu wa sheria.

Kitabu cha A historical Development of the National health Insurance Fund of Tanzania (2011) kimeelezea kwa undani zaidi nini kilijiri tangu wakati wa ukoloni hadi wazo la kuwa na bima ya afya mwaka 1962 na serikali kuamua kuwa na huduma bure hadi ilipoanza kubadili sera miaka ya 1990.

Tangu awali dhana ya bima ya afya iliangaliwa kwa namna tofauti huku historia na utamaduni ukiathiri maelezo mengi ya kiufundi kutoka katika mataifa ambayo yana mifumo mbalimbali ya bima ya afya.

Kimsingi bima ya afya ni mfumo wa kujiunga kwa hiari ama kwa lazima unaomhakikishia mwananchi ambaye anakuwa mwanachama kugharamiwa katika kupata huduma za kiafya zikiwemo za kumwona daktari, kufanya vipimo pamoja na kupata matibabu na dawa.

Kwa upande fulani bima ya afya ni kama mkataba unaoingizwa na anayetaka huduma pamoja na mtoa huduma kwa kupitia mifuko au taasisi inayowaunganisha mtoa huduma pamoja na mhitaji wa wahuduma husika.

Kwa sasa inatambulika zaidi kwamba bima ya afya huchukuliwa kwenye makato anayoyatoa mwajiri kwa waajiriwa wake na pia mwajiriwa mwenyewe.

Hapa nchini pamoja na kuundwa kwa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, pia zipo Bima zinazohusu watu binafsi, wazee na wasiojiweza, wajawazito na wengine wenye mahitaji maalumu bila kusahau wanafunzi kipindi cha masomo yao.

Mara nyingi wanachama huchagua taasisi ama mifuko inayotoa bima kulingana na aina, viwango na mipaka ya taasisi hizo au bima hizo. Pamoja na kuwa na makampuni ya bima kama Strategies, AAR na nyinginezo, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ndio bima inayozungumzwa sana kwa kuwa imebeba wanachama wengi na hasa baada ya kuunganishwa na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF).

Mwanzo wa bima Tanzania Kutokana na mageuzi ya sera ya sekta ya afya 1993 serikali iliangalia namna nzuri ya kuhudumia wananchi wake, mwaka 1999 serikali ilianzia NHIF kama taasisi ya umma chini ya sheria namba 8 ya mwaka 1999 (sura ya 395 kama ilivyorekebishwa mwaka 2002) Mfumo wa uchangiaji unategemea kundi la huduma na pia uwezo wa kulipa wa mwanachama na si vinginevyo.

Kwa mujibu wa sheria ya NHIF wafanyakazi na waajiriwa katuika sekta ya umma wana wajibu wa kujiandikisha na kuchangia asilimia sita ya mishahara yao ya kila mwezi.

Pamoja na mambo mengine, utaratibu wa waajiriwa ambao upo kwa mujibu wa sheria wigo umepanuka zaidi kwa sasa na kuingiza makundi mengine kama wanafunzi, watoto, viongozi wa dini, mama lishe na kadhalika.

Kwani muhimu kujiunga na bima Kuna sababu nyingi zinazozungumzwa lakini kubwa zaidi kwa mujibu wa Basil Msongo, Mhariri wa Habari wa HabariLeo ni mkombozi wa dharura.

Bima husaidia sana mambo ya ghafla wakati huna fedha taslimu na wakati mwingine ukiwa mgonjwa ghafla na huku ukiwa na kitambulisho chako cha kadi ya uanachama.

Mwanachama wa NHIF anayekaa Magomeni Usalama, Maulid Ahmed anasema kwamba Bima ya Afya imemsaidia sana kutokana na matatizo ambayo anayo kama kisukari ambapo huchukua dawa kila mwezi na vifaa vya kupima sukari nyumbani.

Na pamoja na dawa anazochukua kila mwezi, kabla ya ugonjwa huo ameshafanyiwa operesheni kwa kutumia kadi ya NHIF. “Naishi kwa amani, najua nikiumwa wakati wowote sihitaji hela kwa matibabu kwa kuwa nina bima,” anasema Maulid.

Pamoja na manufaa yake anasema kuna haja ya kuangalia sheria upya ya ushiriki wa bima hiyo, kutosubiri muda mrefu kabla ya kuanza kupata matibabu na pia kuhamishwa kwa akaunti ikiwa mwenye akaunti amekufa wakati ndio kwanza kalipia bima tena kwa fedha ndefu.

Alfred Lasteck anayeishi Kimara akizungumzia faida za bima anasema: “Kimsingi nimepunguza gharama za matibabu. Pia nimeweza kusaidia wengine kutoniomba huduma za matibabu.” Kwa hatua yake ya kuchukua bima anasema amesaidia watu wengine, mkewe na watoto na wategemezi ambao wananufaika na matibabu na huduma nyingine za bima zinazotolewa na NHIF.

Oliva Kibua anayekaa Mbezi Malamba Mawili akizungumza akiwa katika kituo cha afya Kimara anasema kwamba yeye hana bima ya afya kwake na mtoto wake, na anapata shida sana mtoto wake au yeye mwenyewe anapougua.

Kutojiunga kwake na bima ya afya anasema kunatokana kutokuwa na fedha. Anapoulizwa kama anajua kwamba kuna bidhaa nyingi (huduma) katika mfuko anasema hajui na haelewi apate hizo habari wapi.

Tofauti na nchi nyingine za Afrika Mashariki kama Rwanda na Kenya, Watanzania wengi hawana huduma ya bima na wengi hawafahamu faida za kuwa na utaratibu wa bima.

Ingawa Watanzania walio wengi (iwe mijini au vijijini), hawana huduma za bima, lakini walio na kipato kidogo hutaabika zaidi kunapotokea kadhia kubwa katika familia huku wakiwa hawana Bima.

Familia hizi zenye kipato kidogo au kisichokuwa na uhakika hutumia akiba yao yote, kuuza mali au mashamba yao, kukopa kwa marafiki, au hata kukopa mahali ambapo wanatozwa riba kubwa sana ili kusaidia kukabiliana na ugonjwa ulioingia katika familia hiyo.

Takwimu zilizopo zinaonesha kwamba asilimia 92 ya Watanzania hawana huduma yoyote ya bima huku wenye bima rasmi wakiwa asilimia 6.4 na isiyo rasmi asilimia 1.9.

Hii ni kwa mujibu wa FSDT/Finscope Survey ya mwaka 2009. Pia, utafiti uliofanywa mwaka 2009 na The First Microinsurance Agency Limited iliyopo Dar es Salaam iliyohusisha watu 600 na ikifanywa na kundi la Steadman ulionesha kuwa walio wengi wanapendelea kuwa na bima ya Afya.

Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ambao unasimamia pia huduma kupitia Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) ina jumla ya walengwa 10,206,980 ambayo ni sawa na asilimia 23.46 ya Watanzania wote.

Kufikia Desemba 2019, wanachama wa NHIF walikuwa 4,856,062, sawa na asilimia 9 ya watanzania. Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mfuko wa Bima ya afya, Mama Anne Makinda amekuwa akisisitiza watanzania kujiunga na mpango wa bima ya afya ambao ndio mfumo bora wa afya duniani kote.

Kukiwa na zaidi ya vituo 7,000 vilivyosajiliwa na NHIF kwa Tanzania nzima kuanzia zahanati, hospitali za mikoa, kanda na Taifa, Mwanachama wa NHIF ananufaika na mambo zaidi ya 10.

Meneja mawasiliano wa NHIF, Angela Mziray anasema mwanachama wa NHIF kwanza ananufaika na ada ya kujiandikisha na kumwona daktari, huduma ya dawa, huduma za vipimo, huduma za wagonjwa wa nje na kulazwa na huduma za upasuaji mdogo, mkubwa na wa kitaalamu.

Anataja manufaa mengine kuwa ni kupewa huduma ya tiba ya kinywa na meno, huduma ya tiba ya macho, huduma za miwani ya kusomea kwa mwanachama mchangiaji, huduma za mazoezi ya kimatibabu ya viungo, matibabu kwa wanachama wastaafu na wenza wao bila kuendelea kuchangia, kwa wale wanachama waliokuwa wanachama kupitia ajira zao na kupatiwa vifaa tiba saidizi kama vile fimbo nyeupe, magongo ya kutembelea na vifaa vya usikivu.

Chanzo: habarileo.co.tz