Tanzania inaendelea kupiga hatua katika utoaji wa huduma za afya za kibingwa na kujiweka katika ramani nzuri kwenye sekta ya afya barani Afrika, baada ya uwekezaji uliofanyika katika Hospitali ya Kairuki kwa mashine yenye teknolojia ya kisasa ya kuondoa uvimbe mwilini bila kufanya upasuaji.
Tayari watu wawili wameshaondolewa uvimbe kwenye kizazi, huku wengine 11 wakisubiri tiba hiyo iliyoanza kutolewa Desemba 29, 2023.
Tiba hiyo inayofanyika kwenye mashine inayofahamika kama Hifu (High Intensity Focused Ultrasound) inaifanya Tanzania kuwa nchi ya kwanza Afrika Mashariki na ya nne barani Afrika kutoa matibabu ya kuondoa uvimbe bila kuhusisha upasuaji wa aina yoyote kwa mgonjwa.
Nchi nyingine zinazotoa tiba hii barani Afrika ni Nigeria, Afrika Kusini na Egypt ambapo mgonjwa anaondolewa uvimbe kwa muda usiozidi saa mbili tangu kuingia kwenye mashine ya Hifu.
Akizungumza na Mwananchi jana, mtaalamu wa teknolojia ya Hifu katika Hospitali ya Kairuki, Dk Fredy Rutachunzibwa alisema aina hiyo ya tiba ya kuondoa uvimbe mwilini inafanyika bila kumchana wala kumtoboa mgonjwa kama inavyofanyika kwa njia nyingine za kuondoa vivimbe.
“Mgonjwa hachanwi, hakatwi wala hatobolewi inayotumika na teknolojia ya kisasa ya kuibadilisha ultra sound energy kuwa nguvu joto ambalo linaelekezwa kwenye sehemu yenye uvimbe na kuunguza bila kuathiri kiungo kingine chochote.
“Ninavyosema haithiri sehemu nyingine yoyote namaanisha kama uvimbe upo kwenye kizazi hili joto litaelekezwa pale ulipo bila kugusa kiungo kingine chochote kwenye kizazi kinachozunguka uvimbe husika,” alisema Dk Rutachunzibwa.
Mtaalamu huyo alieleza teknolojia hiyo inaweza kuondoa uvimbe katika eneo lolote mwilini linalofikiwa na mashine isipokuwa kichwani.
Baadhi ya viungo ambayo mashine hiyo inaweza kuondoa uvimbe ni kongosho, ini, tezi dume, mfuko wa kizazi pamoja na matiti yakitajwa kuwa ni maeneo yanayowasumbua wanawake wengi.
Dk Rutachunzibwa alisema matibabu hayo hufanyika kwa saa zisizozidi mbili na ndani ya muda huo mgonjwa huruhusiwa kutoka hospitali na kuendelea na shughuli zake.
Pamoja na teknolojia hiyo kuwezesha uvimbe kuondolewa ndani ya muda mfupi, mtaalamu huyo alieleza upo uwezekano wa uondoaji huo kufanyika zaidi ya mara moja endapo itabainika kuwa uvimbe ni mkubwa zaidi ya sentimita 10.
Mkuu wa kitengo cha mawasiliano kwa umma wa Hospitali ya Kairuki, Arafa Juba alisema uwepo wa mashine hiyo nchini itapunguza gharama za matibabu, kwani mgonjwa hatalazimu kusafiri hadi Afrika Kusini kufuata tiba hiyo.