Rasimu ya kwanza ya mwongozo wa teknolojia ya upandikizaji mimba nchini, inatarajiwa kupatikana ndani ya siku nne baada ya kikosi maalum chini ya Wizara ya Afya kuanza kazi hiyo.
Kadhalika, mwongozo rasmi unatarajiwa kupatikana ndani ya mwezi mmoja baada ya wadau kuupitia na kutoa maoni yao, na unalenga kusaidia kampuni binafsi na Serikali kujua nini kifanyike kusaidia familia ambazo zimeshindwa kupata watoto kwa njia ya kawaida.
Mapema mwezi huu, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema kwa sasa Tanzania haina sera ya In Vitro Fertility (IVF) na kuiagiza wizara yake kuunda kikosi kazi kitakachoshirikisha sekta binafsi ili kuandaa sera inayohusu suala hilo.
Akizungumza jana, Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake, Sunday Dominico alisema kuna changamoto ya uzazi kwa wanaume na wanawake, hivyo teknolojia hiyo inakuja kurejesha tabasamu lao kwa sababu matokeo yameonekana.
Dk Dominico alisema hayo katika warsha ya siku nne iliyoandaliwa na Wizara ya Afya kwa kushirikiana na taaisi ya Nulife Advanced Fertility Centre.
Ilielezwa kwamba changamoto ya ugumba kwa familia ni kubwa kwa sasa nchini Tanzania, na licha ya kutokuwapo kwa takwimu rasmi, inakadiriwa kuwa asilimia 25 ya familia zinapitia changamoto hiyo.
Kwa mujibu daktari huyo, miongozo hiyo itawasaidia watoa huduma hizo kujua wanatakiwa kuwa na vigezo gani, huku hivi karibuni Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ikianza kutoa huduma hiyo.
Alisema kuna mambo kadhaa ambayo yanafanyiwa kazi likiwamo suala la wataalamu na teknolojia.
“Maagizo tayari yameshatolewa na kazi yetu ni kuyatekeleza na ndiyo maana kazi imeanza mara moja na baada ya siku nne tutatoa rasimu ya kwanza na ndani ya mwezi mmoja mwongozo rasmi utatolewa ili baadhi ya familia ziweze kurejesha hali hiyo ya tabasamu la kutokuwa na watoto,” alibainisha.
Kwa upande mwingine, Mkurugenzi mkuu wa kituo cha Nulife Advanced Fertility Centre Ashutosh Jog alisema wamefurahi kuona Serikali imeamua kuandaa mwongozo katika eneo hilo.
“Tumeamua kuungana na Serikali ili tupate mwongozo mzuri, uhitaji wa huduma hizi ni mkubwa sana, hivyo mwongozo utaweka wazi kuhusu zahanati ambazo hazina sifa, zisizo na uwezo wa kutoa huduma hizi, lengo ni kusaidia wananchi,” alisema.
Naye Mkuu wa kitengo cha mfumo wa uzazi kutoka Hospitali ya Muhimbili, , Dk Matilda Ngarina alisema pamoja na kwamba hakuna takwimu rasmi, uhitaji wa huduma hiyo nchini ni mkubwa, na kwamba kuna baadhi ya taasisi tayari zimeanza kutumia teknolojia hiyo ikiwamo hospitali ya Muhimbili.