Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tanzania yang’ara chanjo ya Covid-19 Afrika

Chanjo Covid.jpeg Tanzania yang’ara chanjo ya Covid-19 Afrika

Fri, 21 Apr 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Tanzania imetajwa kuwa kinara wa utendaji bora katika utoaji chanjo ya Covid-19, mafanikio ambayo Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema yamechangiwa na utashi wa kisiasa kuanzia ngazi ya taifa.

Mwakilishi wa WHO nchini, Dk Zabulon Yoti alisema Tanzania imeibuka kuwa nchi iliyofanya vizuri zaidi kati ya nchi 34 za Afrika zilizokuwa zimetoa chanjo chini ya asilimia 10 ya watu wake.

Kupitia taarifa iliyotolewa jana, Dk Yoti alisema katikati ya Januari mwaka jana, asilimia 2.8 ya Watanzania ndiyo ilikuwa imepata chanjo ya Covid-19 lakini hadi Januari mwaka huu, idadi imeongezeka hadi asilimia 49.

Januari mwaka jana WHO, Shirika la Umoja la Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) na taasisi ya Gavi walianzisha ushirikiano katika utoaji chanjo kwenye maeneo yaliyokuwa na kiwango kidogo cha utoaji wa kinga hiyo.

Dk Yoti alisema utashi wa kisiasa kuanzia ngazi ya taifa, umeiwezesha Tanzania kuongeza kasi katika utoaji chanjo hiyo.

“Ongezeko la haraka la chanjo ya Covid-19 ni matokeo ya kuongezeka kwa dhamira ya kisiasa katika ngazi ya kitaifa, mkoa na wilaya,” alisema.

Alisema katika mkutano ulioratibiwa na kuwezeshwa na WHO Mei, mwaka jana jijini Dodoma serikali na washirika waliunga mkono msimamo chanya wa uongozi wa kitaifa wa kuandaa na kuidhinisha mpango wa haraka wa utekelezaji wa kampeni ya chanjo ya haraka.

Kwa mujibu wa Dk Yoti, hadi Februari mwaka huu watu 32,093,549 walikuwa wamepewa chanjo kamili nchini hatua inayotafsiri kuwa takribani asilimia 45 ya idadi ya watu walipata na asilimia 87 ya lengo ilifikiwa kwa watu wenye umri wa miaka 18.

Aidha, zaidi ya dozi milioni 38. 9 za chanjo zilipokewa Tanzania Bara na Zanzibar kupitia mpango wa chanjo wa Covax. Vilevile zaidi ya asilimia 90 ya dozi zilisambazwa mikoani.

“Tangu mwanzoni mwa mwaka 2022, takwimu zilizopatika zinaonesha kupungua kwa idadi ya wanaolazwa hospitalini kutokana na Covid-19. Mwelekeo wa kushuka kwa wanaolazwa hospitalini una uhusiano na ongezeko la upatikanaji wa chanjo nchini Tanzania,” alisema Dk Yoti.

Taarifa hiyo ya WHO inafafanua kuwa Juni mwaka jana Tanzania ilikuwa miongoni mwa nchi 11 zilizochaguliwa kupitia mpango wa Global Vaccine Access (Global VAX), ushirikiano wa serikali ya Marekani na Tanzania ulihamasisha kuhusu umuhimu wa kupata chanjo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live