Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tanzania yakiri upungufu watumishi sekta ya afya

Thu, 9 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Serikali ya Tanzania imesema kuna upungufu ya watumishi 56,841 katika sekta ya afya ambayo ni sawa na asilimia 48.

Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Josephat Kandege amesema hayo leo Jumatano Mei  wakati akijibu hoja za wabunge waliokuwa wakichangia makadirio ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Watoto na Wazee kwa mwaka wa fedha 2019/2020.

Amesema  upungufu huo umechangiwa pia na uwekezaji mkubwa uliofanywa katika sekta ya afya.

Amesema wameomba kibali cha kuajiri watumishi  15,000 na kwamba Taasisi ya Benjamin imeajiri watumishi 300 ambao watakaa kwa  muda wa miaka miwili.

“Tunahakikisha pia wataalam wanapelekwa vijijini,” amesema.

Naye Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Watoto na Wazee, Dk Faustine Ndungulile amesema wanahakikisha Watanzania wanajiunga na huduma ya bima ya afya.

“Haipendezi mtu anaenda hospitali wakati anaumwa anashindwa kupata huduma kwa sababu hana bima ya afya,” amesema.

Kuhusu upungufu wa watumishi, Dk Ndungulile amesema hawajakaa tu wakiangalia changamoto hiyo, bali wamekuwa wabunifu kwa kutumia raslimali chache ili kuleta tija.

Alisema pamoja na hatua nyingine wameshaanza kufunga mashine za kisasa za X Ray ambazo zinaweza kusomwa katika hospitali kubwa ikiwemo Muhimbili  na kisha mtu aliyeko eneo lolote kupata majibu yake.

“Madaktari bingwa wanaenda maeneo mbalimbali kuendesha kambi mbalimbali ili wananchi waweze kupata huduma za kibingwa tutaendelea na utaratibu huo,” amesema.

Amesema pamoja na changamoto hizo bado huduma zinaendelea kwa ubora unatakiwa.

Kuhusu chanjo ya malaria, Dk Ndungulile amesema hadi sasa hakuna chanjo iliyothibitika kutoa majibu kwa asilimia 100.

Amesema chanjo zilizopo zinatoa majibu kwa kati ya asilimia 20 hadi 40 na kwamba chanjo hizo ziko katika utafiti.

Kwa upande wa hoja ya chanjo ya ugonjwa wa ini, Dk Ndungulile amesema ugonjwa huo ni tatizo na kwamba wanatoa chanjo hizo kwa watoto walio chini ya miaka 10.

Pia wanatoa huduma hiyo kwa watu ambao wako kwenye hatari ya kupata ugonjwa huo wakiwamo wataalam wa afya.

Amesema kwa wale wanaohitaji wataweka utaratibu wa kuchanja kwa gharama nafuu kama ilivyo kwa wabunge.



Chanzo: mwananchi.co.tz