Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tanzania yaeleza mikakati kupambana ukatili wa kijinsia

67015 Mikakatipic

Tue, 16 Jul 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imesema inatekeleza mikakati mbalimbali kupambana na ukatili wa kijinsia kwa watoto na wanawake.

Hayo yameelezwa na naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,  Dk Faustine Ndungulile leo Julai 16, 2019 wakati akifungua mkutano wa kikanda kuhusu ukatili wa kijinsia na ukusanyaji takwimu unaoendeshwa na Shirika la kimataifa linaloshughulikia masuala ya wanawake (UN Women).

Akitumia takwimu za Tanzania Demographic Survey (TDHS 2017),  Dk Ndungulile amesema wanawake wanne kati ya kumi wameshafanyiwa ukatili wa kingono, kimwili au kisaikolojia nchini.

Amesema kati ya matukio 41,000 kuhusu ukatili wa kijinsia yaliyoripotiwa mwaka jana, 13,000 yanawagusa watoto.

Amebainisha kuwa kutokana na hali hiyo,  Serikali inatekeleza mikakati mbalimbali kukomesha ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto.

Ametaja baadhi ya mikakati hiyo kuwa ni utekelezaji wa mpango kazi wa kutokomeza ukatili wa kijinsia, uimarishaji wa madawati ya jinsia ya jeshi la polisi na uanzishwaji wa vituo vya pamoja vya huduma kwa waliofanyiwa ukatili huo.

Pia Soma

Ametaja mkakati mwingine kuwa ni uundwaji wa kamati za ulinzi wa wanawake na watoto kuanzia ngazi ya Taifa mpaka vijijini na elimu kwa umma kupitia njia mbalimbali ikiwamo ya sanaa.

Awali mwakilishi mkazi wa UN Women,  Hodan Addou amesema mkutano huo una lengo la kuhuisha upatikanaji sahihi wa takwimu za ukatili wa kijinsia ili kuandaa mipango halisi itakayosaidia kupambana na tatizo hilo.

Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa), Joyce Shebe amesema ushirikiano baina ya jamii, mashirika na Serikali utasaidia kuondoa ukatili wa kijinsia.

 

Chanzo: mwananchi.co.tz