Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tanzania ya 4 duniani kwa selimundu

68b54b844a125ad353d0b39061f9e4b7.jpeg Tanzania ya 4 duniani kwa selimundu

Sun, 20 Jun 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

JUMLA ya watoto 11,000 hapa nchini huzaliwa na ugonjwa wa selimundu kila mwaka hali ambayo inaifanya Tanzania kuwa nchi ya nne duniani kwa idadi kubwa ya wagonjwa wa ugonjwa huo ambao umeshamiri zaidi katika mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Hayo yamesemwa jana jijini hapa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Profesa Abel Makubi alipokuwa akihutubia kwenye kilele

cha maadhimisho ya Siku ya Selimundu Duniani ambayo kitaifa yamefanyika jijini hapa yakiwa na kauli mbiu “Angaza, tambua ugonjwa wa sikoseli.”

Alisema kwa mujibu wa utafiti uliofanywa hivi karibuni na Shirika la Afya Duniani (WHO) unaonesha kuwa mtu mmoja kati ya watu wanne ana kinasaba cha selimundu na kuwataka Watanzania kuachana na mila potofu kwa kuwanyanyapaa watu waliopatwa na ugonjwa huo na badala yake wawape faraja.

Akitolea mfano yeye mwenyewe alisema kuwa alipoteza ndugu zake wawili ambao walikufa kwa ugonjwa huo kutokana na wakati huo jamii haikuwa na uelewa mpana juu ya ugonjwa huo.

“Ndio maana mara baada ya kuhitimu Shahada yangu ya pili pale Muhimbili, niliamua kusomea mambo ya damu ili niwe mbobezi kwenye eneo hili ili niweze kuisaidia jamii,”alisema.

Aliwataka waganga wakuu wa mikoa nchini kuhakikisha kuwa wanatoa elimu ya ugonjwa huo kwenye mikoa yao ili kuwawezesha wananchi kuondokana na imani potofu kama sehemu ya kupambana na ugonjwa huo.

Alisema mikakati ya serikali ni kuhakikisha watu wote wanaopata ugonjwa huo wanahakikishiwa mazingira bora ya kupatiwa huduma kupitia hospitali za kanda, mikoa na wilaya kwenye maeneo waliyopo.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando Dk Fabian Massaga alisema hospitali hiyo kupitia kliniki ya watoto kabla ya maadhimisho ya kilele cha selimundu , ilifanya uchunguzi wa selimundu kwa watu wazima na watoto 218 na kati ya hao, 34 walibainika kuwa na ugonjwa huo sawa na asilimia 15.6.

Alisema waliobeba kinasaba cha selimundu baada ya uchunguzi huo walikuwa 69 sawa na asilimia 31.6 na waliokuwa hawana selimundu ni 115 sawa na asilimia 52.8.

“Wagonjwa wote hawa wamesajiliwa tayari hapa Bugando kwa ajili ya kuanza kliniki endelevu ya tiba,” alisema na kuongeza hospitali hiyo imekuwa ikitoa huduma hiyo kwa wagonjwa kati ya 250 na 300 kwa mwezi. Takwimu hizi zinaonesha ukubwa wa ugonjwa huo seli nchini hasa kwa mikoa ya kanda ya ziwa,” alisema.

Kwa upande wake, Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Dk Silas Wambura aliishukuru serikali kwa kukubali maadhimisho ya siku ya selimundu kitaifa yafanyike jijini Mwanza na kufanya maboresho makubwa ya ujenzi wa miundombinu na uwezeshaji wa vifaa tiba katika sekta ya afya kwa mkoa wa Mwanza.

Akizungumza kwa niaba ya Bodi ya uongozi wa hospitali, Padri John Katembo aliishukuru serikali kwa utoaji wa vifaa tiba ambavyo alisema vitasaidia sana kwenye utoaji wa huduma za tiba hospitalini hapo.

Chanzo: www.habarileo.co.tz