Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tanzania kuelekea kitovu cha utalii wa matibabu Afrika

61c25d684c79acf823de07602f9b7175 Tanzania kuelekea kitovu cha utalii wa matibabu Afrika

Fri, 12 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MWAKA jana, nchi nyingi duniani zilikumbwa na mdororo wa uchumi kutokana na janga la ugonjwa naosababishwa na virusi vya korona (Covid-19).

Licha ya janga hilo, Tanzania chini ya Rais John Magufuli hali ilikuwa ni tofauti. Nchi iliendelea kufanya vyema zaidi katika nyanja zote za kiuchumi.

Kwa mujibu wa Benki ya Dunia, Pato la Taifa la kila mtu liliongezeka kutoka dola za Marekani 350 mwaka 2004 hadi dola za Marekani 1080 mwaka 2019.

Mafanikio makubwa ya Tanzania yametokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na serikali katika nyanja mbalimbali ikiwamo sekta ya afya ambayo makala haya yanaiangalia kwa kina.

Uwekezaji katika afya ni eneo muhimu ambalo linaonekana dhahiri kwamba litatoa mchango mkubwa siku za usoni kwa kuwezesha nchi kuendesha utalii wa matibabu.

Kutokana na uwekezaji unaofanyika sasa ni dhahiri Tanzania inaweza kuwa kitovu cha utalii wa matibabu barani Afrika.

Huko nyuma ilikuwa ni kawaida kuona wananchi wengi toka nchi masikini ikiwemo Tanzania wakisafiri kwenda nchi zilizoendelea kwa ajili ya kupata matibabu ambayo yalikuwa hayapatikani katika nchi zao.

Hata hivyo, katika siku za karibuni mambo yamebadilika sana kwani watu wamekuwa wakisafiri toka nchi tajiri na kwenda nchi za uchumi wa kati na nchi zinazoendelea ili kupata matibabu ambayo yana gharama nafuu kuliko nchi zao.

Wakati mwingine watu wamekuwa wakilazimika kusafiri nje ya nchi zao kupata matibabu kwa sababu tu nchi zao haziruhusu au hazijaidhinisha matumizi ya baadhi ya dawa na/au matibabu fulani.

Nchi nyingi zimekuwa zikiweka mazingira mazuri ya Utalii wa Matibabu kwa ajili ya kukuza na kuchochea uchumi wao. Mfano, wakati wa mdororo wa uchumi wa mwaka 1997 iliolikumba Bara Asia na wa 2008 ulioikumba dunia, nchi nyingi za Asia na Mashariki ya Mbali ziliboresha mazingira ya Utalii wa Matibabu na sasa kimekuwa chanzo kikuu cha fedha za kigeni.

Utalii wa matibabu India

Ukitaja nchi ambazo zimekuja juu sana kwa utalii wa matibabu duniani huwezi kuacha kuizungumzia India inayotoa matibabu ya hali ya juu na kwa gharama ya chini.

Kwa mfano, gharama za upandikizaji wa ini nchini Marekani ni zaidi ya dola laki tatu lakini India haizidi dola laki moja. Vivyo hivyo, upasuaji wa moyo kwa Marekani hugharimu takribani dola 120,000 wakati India inakadiriwa kuwa ni nusu ya gharama hizo.

Kutokana na ukweli huu wagonjwa husafiri kutoka Marekani kwenda nchi za Asia kwa ajili ya matibabu ambayo gharama zake ziko chini zaidi ya nchi zao.

Sababu nyingine ya watu wengi kuamua kusafiri nje ya nchi zao ni muda wa kusubiri matibabu kwani ugonjwa huwa hausubiri na hivyo mwenye fedha zake huona ni vyema kusafiri na kufanyiwa matibabu kwa haraka ili arudi kuendela na majukumu yake.

Ni kitu cha kawaida India kuona wizara inayosimamia afya na wizara ya utalii zikishirikiana kwa ukaribu katika kuhakikisha zinaifanya India kuwa kitovu cha utalii wa matibabu duniani. Hii ni pamoja na kuwafanya wanaopata viza za matibabu kuruhusiwa kuishi nchini humo kwa kipindi fulani.

Aidha, India pia huruhusu baadhi ya nchi kupata hizo viza za matibabu pindi tu wanapokuwa wamefika nchini humo hivyo kufanya watu wengi kupanga safari zao kwenda India bila ya kupoteza muda kuomba viza wakiwa nchini mwao.

Kuwepo kwa ubora wa vifaa tiba, vipimo vya kisasa na uhakika wa matibabu ni sababu nyingine inayofanya watu wengi kuamua kufanya utalii wa matibabu.

Kwa nini Tanzania sasa?

Tanzania kwa sasa ina vituo vingi vya kutolea huduma ukilinganisha na nchi zingine za Afrika. Vituo hivyo ni mchanganyiko, baadhi vikimilikiwa na Serikali, watu binafsi na mashirika ya dini.

Uwepo wa vituo vingi unaifanya Tanzania kuwa na faida ya ushindani baina ya nchi zingine. Ukienda Kanda ya Kusini utakuta hospitali kubwa ya kanda iliyoko Mtwara ambayo ujenzi wake uligharimu Sh bilion 15.8 sanjari na ujenzi wa vituo vya afya zaidi ya 25 mkoani humo.

Hospitali hiyo, pamoja na kutumika kwa huduma za matibabu na mafunzo, inaweza kutumika kama sehemu ya utalii kutokana na kujengwa katika eneo la ufukweni mwa bahari ya Hindi na tayari idara ya ardhi katika halmashauri ya Mikindani imehakikisha eneo hilo linapangwa katika sura ya kitalii.

Kanda ya Ziwa kuna hospitali tatu kubwa za Kanda ikiwemo Hospitali ya Bugando iliyopo Jijini Mwanza na Hospitali mpya ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere iliyo mjini Musoma.

Historia imeandikwa kwa kukamilika ujenzi wa hospitali hiyo ya Mwalimu Nyerere uliogharimu Sh bilioni 15 na kuhuisha ndoto ya tangu mwaka 1976 wakati Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere alipoiasisi.

Hospitali nyingine kubwa ni Hospitali ya Rufaa ya Kanda inayojengwa Chato mkoani Geita iliyowekwa jiwe la msingi na Rais wa Msumbiji na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Filipe Nyusi tarehe 11 Januari, 2021.

Hii itakuwa na uwezo wa kuhudumia watu milioni 14 kutoka Mikoa ya Kagera, Kigoma, Tabora, Rukwa, Geita, na wilaya za Mikoa ya Mwanza na Shinyanga pamoja na nchi za jirani. Hospitali za Kanda ya Ziwa pia zinazungukwa na vivutio kadhaa kama mbuga ya Serengeti, Rubondo, Kisiwa cha Saa Nane, Burigi Chato, Ziwa Victoria na kadhalika.

Kanda ya Kaskazini kuna hospitali kubwa zaidi ya tatu ambazo ni pamoja na Kilimajaro Christian Medical Centre (KCMC) iliyo mkoani Kilimanjaro iliyozungukwa na milima yenye volcano na barafu.

Nyingine ni Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC) iliyo jijini Arusha na Haydom Lutheran Hospital iliyoko Mbulu Mkoani Manyara. Hospitali zote hizi zina madaktari bingwa wengi, vifaa vya uchunguzi wa kisasa kama CT-scan na faida nyingine ni kwamba zimekaa maeneo yanayoongoza kwa vivutio vya utalii nchini na hivyo kuwa na faida ya kiushindani zaidi.

Kanda ya Nyanda za Juu Kusini kuna hospitali za Rufaa za Kanda mbili ambazo zote zina madaktari bingwa pamoja na uwepo wa vifaa vya uchunguzi na tiba vya kisasa kama CT scan, upasuaji wa nyonga na usafishaji wa damu/figo. Hizi ni pamoja na Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya na Hospitali ya Consolata Ikonda iliyo katika wilaya ya Makete Mkoani Njombe.

Kanda ya Kati kuna hospitali kubwa nne ambazo zinatoa huduma za matibabu ya kibobezi kama Hospitali ya Rufaa ya Milembe; Hospitali ya Benjamin Mkapa iliyo katika Chuo Kikuu cha Dodoma inayofanya matibabu makubwa kama upandikizaji wa figo (renal transplant), usafishaji wa figo/damu na matibabu ya uchunguzi na tiba ya moyo.

Hospitali nyingine ni ya Rufaa ya Uhuru iliyo Wilayani Chamwino ambayo ni mpya na Hospitali ya St. Gaspar iliyoko Itigi, Singida.

Ukiacha uwepo wa hospitali za rufaa za kanda na hospitali za rufaa za kila mkoa, Tanzania ina hospitali zingine kubwa za kitaifa kama Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI), Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) pamoja na Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI). Hospitali au taasisi hizi zinatoa huduma za kibingwa na kibobezi katika nyanja takribani zote za tiba kuanzia uchunguzi wa kitaalamu mpaka matibabu.

Kuendelea kuboreshwa kwa Sekta ya Afya kwa kuwasomesha na kuwajengea uwezo wataalamu kumefanya huduma nyingi za matibabu kufanyika ndani ya nchi ambazo awali tulizowea kuona huduma kama hizi zinapoanzishwa lazima kuwe na wataalamu kutoka nje ya nchi, lakini leo tunaona huduma nyingi zimeanzishwa na wataalamu wa Kitanzania .

Wataalamu hawa ni katika nyanja nyingi za magonjwa kama ya figo, kusafisha damu na upandikizaji wa figo, upasuaji wa magonjwa ya moyo ikiwemo matundu na kuziba kwa mishipa, upasuaji wa upandikizi wa nyonga na goti, vipimo na uchunguzi wa matibabu ya saratani pamoja na maeneo mengine.

Serikali ya Awamu ya Tano imewekeza mabilioni ya fedha katika ununuzi wa mashine mpya na za kisasa za uchunguzi na matibabu ya magonjwa mbalimbali kama ya matibabu ya magonjwa ya moyo kwa kutumia maabara maalumu inayojulikana kwa jina la Cath-lab katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete na Hospitali ya Benjamin Mkapa iliyopo jijini Dodoma kwa lengo la kuboresha na kupanua wigo wa huduma za matibabu ya kibingwa nchini.

Vifaa vingine vya uchunguzi na matibabu ni kama CT-Scan, MRI pamoja na Maabara za kisasa za uchunguzi wa magonjwa mbalimbali (Radiology and Diagnostic intervention therapy).

Mwandishi wa mkala haya ambaye ni Ofisa Mwandamizi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ni msomaji wa gazeti hili.

Chanzo: www.habarileo.co.tz