Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tanzania, China zasherehekea miaka 50 ya ushirikiano sekta ya afya

24591 Pic+china TanzaniaWeb

Wed, 31 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es salaam. Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema katika kipindi cha miaka mitatu, uwezo wa madaktari wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) katika kufanya upasuaji umeongezeka hadi kufikia asilimia 80 kutoka 45.

Kuongezeka kwa uwezo huo kunatokana na ushirikiano kati ya Tanzania na China katika masuala ya afya hususani katika kuleta wataalamu wa wagonjwa mbalimbali na kuwapatia wataalamu wa ndani mafunzo.

Akizungumza katika maadhimisho ya miaka 50 ya ushirikiano katika masuala ya afya  kati ya nchi hizo mbili leo Jumatatu Oktoba 29, 2018, Waziri Ummy amesema China imekuwa msaada mkubwa katika kuboresha utoaji wa huduma za upasuaji hasa katika magonjwa ya moyo.

"Hata ukiangalia kwa nadharia, wagonjwa wanaopelekwa nje kwa ajili ya matibabu siku hizi ni wachache kuliko wale wanaotibiwa ndani ya nchi.”

“Hii ni faida kwetu na hata zile pesa zilizokuwa zikitumika katika kuwatibia tunaweza kufanya maboresho katika huduma za afya," amesema Ummy.

Balozi wa China nchini, Wang Ke emesema mbali na kuinua uwezo wa wataalamu wa Tanzania katika kufanya upasuaji pia wataendelea kutoa huduma katika majanga mbalimbali yanayoikumba nchi.

"Kwa mfano katika tetemeko la Kagera wataalamu wetu waliweza kuhudumia zaidi ya wagonjwa 500 na kuwawezesha kurudi katika hali yao ya kawaida," amesema Wang.

"Na tutaendelea kutoa mafunzo kwa kupitia wataalamu wetu watakaokuwa wanafanya kazi na wale waliopo nchini na tunashukuru kwa sababu mnawapatia ushirikiano wa kutosha kuanzia serikalini, hospitalini na hata watumishi wenzao," ameongeza.

Chanzo: mwananchi.co.tz