Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tamu, chungu za bima ya afya kwa wote

Bimapiic Data Tamu, chungu za bima ya afya kwa wote

Wed, 25 Jan 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wizara ya Afya imeyataja mambo muhimu yaliyozingatiwa kwenye muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote, likiwamo la kila Mtanzania kupatiwa huduma za afya hata kwa wale wasio na uwezo.

Hata hivyo, imefafanua juu ya wastaafu waliokuwa wakichangia bima ya afya binafsi, iwapo muswada huo utapita, watalazimika kujiunga na skimu ya bima ya afya ya umma ili kuwa na sifa ya uchangiaji wa miaka 15.

Hatua hiyo inakuja wakati Serikali tayari imeweka bayana kwamba, Februari 2023 itawasilisha bungeni kwa mara ya pili muswada huo baada ya kuondolewa mwaka jana kutokana na kile kilichoelezwa, ni kukosekana kwa chanzo halisi cha mapato ya kuwezesha kutoa huduma hizo kwa wote.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari, Waziri wa Afya Ummy Mwalimu alisema;

“Ili kuwa na uendelevu wa mfuko tunachoangalia ni michango, kama vile ilivyo kwa mifuko ya hifadhi ya jamii ya NSSF na WCF (PSSSF), kwamba uwe walau umechangia kwa miaka 15.”

Akifafanua hilo la wastaafu, Mwenyekiti wa kikosi kazi cha muswada huo wa Bima ya Afya kwa Wote, Bernard Konga alisema hata kama mtu amechangia miaka 15 kwenye bima za sekta binafsi, hataweza kunufaika na bima hizo baada ya kustaafu.

Konga ambaye pia ni mkurugenzi mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) NHIF, alisema mchangiaji huyo sasa atapaswa kuwa na michango isiyopungua miaka 15 katika skimu ya umma.

Akizungumzia umuhimu wa michango, Ummy alikosoa baadhi ya wafanyakazi ambao wanasubiri hadi wastaafu ndipo wajiunge na bima ya afya, jambo alilosema si sahihi kwa uchangiaji wa mfuko huo.

“Tunataka walau awe amechangia kwa miaka 15, na kwenye bima ya afya, wastaafu ndiyo wenye matumizi makubwa kutokana na kushambuliwa zaidi na magonjwa yasiyo ya kuambukiza,” alisema Waziri Ummy.

Alisema kwa sasa asilimia 99 ya watu wenye bima ya afya nchini, wamejiunga wakiwa wagonjwa huku wengine wakilazimika kuuza mali zao kuhudumia wagonjwa waliopo hospitalini kutokana na kukosa bima.

“Mtu anachangia kwenye Bima ya Afya ya Toto Card, matumizi yake ni asilimia 300 maana yake katika kila Sh100 anayochangia, anatumia Sh300. Ndio maana tukaifanya lazima ili sasa wale wasioumwa waweze kuingia, japo tunasema ni lazima hakuna atakayefungwa kwa kukosa bima ya afya, lakini ukitaka leseni ya biashara, basi uwe na bima ya afya.

“Nitoe wito kwa Watanzania kuanza kudunduliza ili kuwa na gharama za matibabu kabla ya kuugua na hatutomuacha nyuma Mtanzania yeyote,” alisema Ummy.

Alisema lengo la Serikali kufungamanisha bima ya afya na huduma zingine ni kutaka kuhakikisha wananchi wote wanakuwa na bima.

Akifafanua zaidi, Konga, alitaja jambo lingine lililozingatiwa kwenye muswada huo, kuwa ni Serikali kupitia Wizara ya Fedha itatenga bajeti kwa ajili ya matibabu kwa wananchi wasio na uwezo.

Alisema katika utoaji wa huduma katika ngazi ya kaya endapo muswada huo utapitishwa na kuwa sheria, unakwenda kuwatambua watu sita ambao ni mwanachama mchangiaji, mwenza na wategemezi wasiozidi wanne.

Kwa familia yenye watu zaidi ya sita, alisema watalazimika kuanzisha kaya nyingine ili kuwapatia nafasi wanakaya hao ambao wanaweza wakawa ni wakwe, wazazi au watoto.

“Ndiyo maana tunasema bima hii haitamuacha mtu, kila mmoja atapatiwa huduma, hii ni tofauti na hii tuliyonayo sasa inayokwenda na idadi ndogo ya wategemezi. Kwa hii, mtu akiona ameshasajili kaya moja, anaweza akasajili kaya nyingine ya watu sita na ikaendelea kuchangia,” alifafanua Konga.

Mamlaka ya udhibiti

Akizungumzia kuhusu kuwepo kwa mamlaka ya udhibiti wa bima ya afya, Konga alisema; “Tumeimarisha usimamizi na udhibiti wa masuala ya bima ya afya, jukumu litakalotekelezwa na Mamlaka ya Bima Tanzania (Tira), pia tumezingatia dhana ya ufungamanishaji wa huduma wenye lengo la kutaka kila mwananchi awe na bima ya afya.

Akifafanua kuhusu hoja hiyo, Waziri Ummy alisema mapendekezo ya awali ya huduma zilizofungamanishwa na upatikanaji wa bima zilikuwa tisa.

“Lakini baada ya majadiliano, tuliona kuna baadhi ya huduma zinapaswa kuondolewa ambazo ni utambulisho wa mlipa kodi, usajili wa laini za simu, hati za kusafiria, utoaji wa kitambulisho cha Taifa na Usajili wa wanafunzi wa kidato cha tano na sita,” alisema waziri huyo.

Alizitaja huduma zilizobaki katika ufungamanishaji kuwa ni pamoja na ya leseni za udereva, bima ya vyombo vya moto, leseni za biashara na usajili wa wanafunzi vyuoni.

Akifafanua hilo, Konga alisema athari ya kutofungamanisha bima ya afya na huduma, kutasababisha kushindwa kutekelezeka kwa Sheria ya Bima ya Afya kwa wote.

Lakini alisema kwa wananchi kujiunga na bima wakiwa tayari wagonjwa, kunaweza kudhoofisha uhai na uendelevu wa siku za bima ya afya.

Jambo lingine, Konga alisema wamezingatia kuwepo kwa kitita cha mafao ya huduma muhimu ambacho kila skimu ya bima ya afya, italazimika kukitoa na itakuwa ni haki ya kila mwanachama.

“Kitita cha mafao cha huduma muhimu itajumuisha ada ya kumuona daktari, gharama za vipimo, gharama za dawa aina zote, gharama za upasuaji mkubwa na mdogo, mgonjwa kulazwa, huduma ya kinywa na meno, tiba ya macho, vifaa saidizi na huduma ya mazoezi na viungo,” alisema.

Maandalizi ya Serikali

Akizungumzia maandalizi ya Serikali kuwahudumia wananchi wote, Konga alisema kuna ongezeko la vituo vya kutolea huduma za afya kutoka 8,449 hadi kufikia vituo 10,067.

Alisema Serikali inatoa Sh20 bilioni kila mwezi kwa ajili ya ununuzi na usambazaji wa dawa, hadi kufikia Desemba 2022 upatikanaji wake ulikuwa kwa asilimia 67 kutoka asilimia 62 Agosti mwaka jana.

“Serikali imenunua na kusimika vifaa vya kisasa vya uchunguzi na matibabu ikiwemo X-Ray (95) CT Scan (30) na MRI (4) katika vituo vya kutolea huduma. Pia wizara inaendelea kutekeleza mkakati wa kuongeza rasilimali watu katika sekta na mwaka 2020/2021 watumishi 3,347 na mwaka 2021/2022, iliajiri watumishi 9,262. Kwa mwaka wa fedha 2022/2023, wizara imetenga Sh8 bilioni kwa ajili ya ufadhili wa mafunzo ya ubingwa na ubobezi,”alisema.

Akizungumza katika mkutano huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Profesa Abel Makubi alisema ili kuiwezesha Tira ifanye kazi zake kwa ufanisi, Serikali itaiongezea mamlaka hiyo wataalam

Chanzo: www.tanzaniaweb.live