Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Takukuru yaokoa bil 1.2/ dawa vifaa tiba MOI

1f1e49fa454a611b01a9c8e38cbc32ce Takukuru yaokoa bil 1.2/ dawa vifaa tiba MOI

Thu, 14 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru), kwa kushirikiana na Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI), wamedhibiti uchepushaji na ubadhirifu wa dawa za thamani ya zaidi ya Sh bilioni 1.2 uliokuwa unafanywa na watumishi wa Kitengo cha Famasia katika taasisi hiyo.

Aidha, katika sakata hilo, wafamasia 23 wa MOI wanahojiwa ambao baadhi yao baada ya kubaini wanachunguzwa, walikiri kufanya ubadhirifu huo na kuomba Takukuru iwakubalie warejeshe fedha.

Akizungumzia tukio hilo jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Brigedia Jenerali John Mbungo (pichani) alisema fedha hizo zilikuwa zinachepushwa katika mfumo wa MEDPRO4 ambao ni wa kutunza taarifa za kumbukumbu za utoaji wa dawa na vifaa tiba kwa wagonjwa unaotumiwa na MOI.

Brigedia Jenerali Mbungo alisema baada ya Takukuru kupata taarifa hiyo walianza uchunguzi na kubaini kuwa wafamasia hao walikuwa wanaongeza idadi ya dawa na vifaa tiba kwenye fomu ya mgonjwa iliyosainiwa na daktari.

“Baada ya taarifa kutufikia tukaanza uchunguzi na tukabaini tofauti kati ya taarifa za dawa zilizoingizwa na wafamasia kwenye mfumo wa MEDPRO4 na taarifa zilizoandikwa na madaktari kwenye mafaili au majalada ya wagonjwa ikilinganishwa na fomu za wagonjwa zilizotoa maelekezo ya aina ya dawa na matumizi yake kwa wagonjwa waliohudumiwa,” alisema Brigedia Jenerali Mbungo.

Akitoa mfano, alisema daktari akiandika dawa 30 za matumizi ya mgonjwa kwa mwezi mmoja, mfamasia anaongeza idadi ya dawa na kuingiza kwenye mfumo dawa 60 ambazo ni tofauti ya dawa 30 na mgonjwa hapatiwi dawa hizo.

“Uchunguzi umebaini pia kuwa wafamasia walikuwa wanasababisha upotevu wa dawa kwa kuingiza taarifa za uongo kwenye mifumo zinazoonesha mgonjwa amepatiwa dawa ya aina hiyo kwa zaidi ya mara moja jambo ambalo hata kama lingefanyika kwa makosa, basi ingesababisha madhara kwa wagonjwa,” alisema.

Aidha, ubadhirifu mwingine waliokuwa wakifanya watumishi wa Kitengo cha Famasia MOI ni kuingiza taarifa kwenye mfumo zikionesha dawa zimetolewa kwa wagonjwa huku wakijua ni wagonjwa hewa, na wengine wakiongeza dawa zenye bei kubwa kwenye fomu za madaktari ambazo kiuhalisia daktari wala hajatoa maelekezo hayo.

Mkuu huyo wa Takukuru alisema kwa sasa hawawezi kutaja majina ya watuhumiwa hao hadi uchunguzi utakapokamilika, na kusema Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Dorothy Gwajima, amekuwa akisisitiza wafanyakazi wa maduka ya dawa serikalini kufanya kazi kwa kuzingatia weledi na kuacha tabia ya kufanya kazi kienyeji.

Alisema katika hilo, Dk Gwajima alipokuwa kwenye ziara katika hospitali tofauti nchini alibaini maduka mengi ya dawa ya serikali watumishi wake hawafuati mfumo wa uwekaji kumbukumbu na kuagiza operesheni maalumu ianze ya kuwaelimisha viongozi wa kiutawala katika mikoa na wilaya nzima kuelewa utaratibu unaopaswa kufuatwa.

Aidha, Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru ametoa mwito kwa watumishi wote na wananchi kufanya kazi zao kwa weledi na kuacha vitendo vya ubadhirifu kwa sababu wako macho na itang’ata wote wanaojihusisha na vitendo viovu nchini.

Chanzo: habarileo.co.tz