Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tahadhari vipimo vya typhoid

Vipimo Pc Data3333 Tahadhari vipimo vya typhoid

Sun, 3 Oct 2021 Chanzo: mwananchidigital

Wakati kanuni za kitabibu zikielekeza majibu ya ugonjwa wa homa ya matumbo (typhoid) yatolewe ndani ya saa 24 baada ya kupitia hatua mbili za upimaji, uchunguzi wa Mwananchi umebaini kuwa vituo vingi vya upimaji hutoa majibu hayo kati ya dakika 30 hadi saa moja.

Kutokana na sintofahamu hiyo ya vipimo vya typhoid, baadhi ya taasisi zinazojihusisha na utoaji wa bima ya afya, ukiwemo Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) zimekataa kutambua na kulipia vipimo vinavyotolewa kwa muda mfupi.

Baadhi ya maabara hupima na kutoa majibu ya ugonjwa huo kwa wagonjwa kuwa au kutokuwa na vidudu vya typhoid katika hatua ya awali ya upimaji bila kwenda kwenye hatua ya pili.

Kwa mujibu wa mtaalamu wa afya ya binadamu, Dk Patrick Ntakisigaye, ili kuthibitisha uwepo na kiwango cha wadudu wa ugonjwa wa typhoid, sampuli inatakiwa kupitia hatua mbili, moja ikiwa ya awali ya kuangalia matokeo baada ya kuweka vitendanishi kwenye sampuli ya mgonjwa.

“Kukiwa kuna antibody reaction (mwitikio wa kingamwili), sampuli husika hufanyiwa incubation ambayo majibu yake yanatoka baada ya saa 18. Hapo ndipo mtaalamu atajua iwapo mwitikio ulioonekana kwenye hatua ya awali umetokana na uwepo wa wadudu au la,” alisema Dk Ntakisigaye.

Alifafanua; “Mwitikio wa kingamwili unaweza kuonekana hata kama mgonjwa aliugua, akatibiwa na kupona typhoid. Hatua ya pili ndiyo hutoa majibu sahihi ili kujiridhisha, inabidi sampuli ionyeshe reaction kiwango cha wadudu kama ni 100/150 au 100/180.”

Uchunguzi Kilimanjaro

Uchunguzi uliofanywa miji ya Moshi na Bomang’ombe katika Wilaya za Hai na Rombo mkoani Kilimanjaro, umebaini kuwa zahanati na hospitali nyingi za binafsi hazifanyi kipimo cha typhoid na wahudumu katika mapokezi huwaelekeza kwenda hospitali kubwa.

Hospitali zinazofanya kipimo hicho ni Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini ya KCMC, hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Kilimanjaro ya Mawenzi na maabara binafsi za Conrad Serafin Kimario na Lancet na baadhi ya hospitali za wilaya.

Mathalani, mwandishi wetu alifika katika maabara ya Serafin Septemba 16, 2021 saa 6:37 mchana na kuomba kupima typhoid ambapo alikubaliwa kwa gharama ya Sh5,000 ambapo alilipa na kupewa risiti ya kielektroniki (EFD) namba 9165.

Alitolewa sampuli ya damu na kupimwa kipimo cha Widal Test na kutakiwa kufuata majibu siku inayofuata kuanzia saa 5 asubuhi ikiwa ni baada ya saa 24 kama inavyotakiwa kitaalamu. Katika baadhi ya zahanati wahudumu wake walisitasita kabla ya kujibu kuwa hawapimi.

Mwandishi wetu mwingine alikwenda mara mbili katika hospitali binafsi ya CRCT Kilimanjaro maarufu kama Kilimanjaro Hospital ambapo alipofika mapokezi na kuomba kupima kipimo hicho, wahudumu walimweleza kuwa hawapimi.

“Sisi hatufanyi hicho kipimo. Nenda KCMC, Mawenzi au Lancet. Ukienda popote nje ya hapo ukapima hicho wakakupa majibu siku hiyo hiyo ujue umedanganywa. Majibu yanatakiwa yatoke saa 24 na kwingine hadi siku 3,” alielezwa.

Waandishi wetu walizunguka pia katika zahanati zilizopo maeneo ya Majengo katika Manispaa ya Moshi na katikati ya mji ambapo wauguzi waliokutwa mapokezi walieleza kuwa hawapimi kipimo hicho labda kwa hospitali kubwa.

Ofisa Uhusiano wa KCMC, Gabriel Chisseo alipoulizwa juu ya kipimo hicho alisema: “Typhoid Inspires inapima kwa namna mbili. Ya kwanza ni kwa kutumia damu ambayo inajulikana kama ‘widal test’ kwa Sh10,000 na majibu ni baada ya saa 24”.

Kwa mujibu wa ofisa uhusiano huyo, kipimo cha pili ni ‘culture’ ambayo hupimwa kwa kuchukua sampuli ya damu au choo kikubwa na gharama yake ni Sh30,000 na majibu ya kipimo hicho huchukua muda wa siku tatu na wakati mwingine tano.

Uchunguzi jijini Mwanza

Katika baadhi ya hospitali jijini Mwanza, vipimo vya typhoid vilitolewa ndani ya muda wa saa moja.

“Majibu yanaonyesha huna typhoid; labda ufanye vipimo vingine,” alisema mmoja wa wataalamu wa afya katika moja ya maabara jijini Mwanza (jina linahifadhiwa) wakati alipotoa majibu ya kipimo cha ugonjwa yaliyotoka ndani ya muda wa saa moja.

Katika kituo kingine (jina linahifadhiwa), majibu ya kipimo cha ugonjwa huo yalitolewa ndani ya muda wa dakika 30, yakionyesha kuwa aliyepimwa hakuwa na wadudu wa typhoid.

Hali kama hiyo pia ilijitokeza jijini Dodoma ambako mwandishi wetu alikwenda kupima ugonjwa huo katika maabara binafsi iliyopo eneo la Chang’ombe jijini humo na kupewa majibu ndani ya nusu saa.

Mwandishi wetu alipoingia kwa daktari huyo saa 5.52 asubuhi alisikilizwa tatizo lake na kuulizwa shughuli anayofanya.

Daktari aliyekuwepo alichukua damu kwenye mshipa mkubwa na kumuomba asubiri ambapo ilipofika saa 6.27 mchana mwandishi aliitwa kupewa majibu.

Daktari huyo alimueleza mwandishi kuwa majibu ya vipimo vyake yameonyesha hana malaria isipokuwa kwenye kipimo cha typhoid kumeonekana kuna maambukizi kidogo na hivyo alishauri atumie dawa ambazo aliziandika.

Gharama za vipimo zinalipwa kwa daktari mwenyewe anayechukua maelezo ya mgonjwa. Maabara hiyo pia haitoi risiti za malipo ya gharama za vipimo. Daktari huyo alipoulizwa alisema wameishiwa na bado hazijaja. Katika hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Dodoma (RRH) vipimo vya typhoid vinachukua muda wa nusu saa hadi dakika 40 kutegemeana na wingi wa watu.

Mwandishi wa gazeti hili alifika hospitalini hapo kuchukua vipimo, lakini ilichukua dakika 28 tangu kupimwa na kupata majibu ya vipimo vyake.

Tofauti na vituo binafsi, hapa utaratibu ulikuwa ni kufungua faili, kwenda kwa daktari na baada ya kuandikiwa, mgonjwa anarudi dirisha la kulipia ambako anatakiwa kutoa Sh3,000 kama malipo ili kupimwa typhoid.

Vipimo vilichukuliwa saa nne na dakika 24 asubuhi na majibu yalitoka saa nne na dakika 52 ambayo yalitakiwa kwenda kusomwa na daktari aliyeandika au mwingine katika hadhi ya udaktari.

Typhoid na bima

Baadhi ya wananchi waliozungumza na gazeti hili walisema wamekuwa wakiambiwa kwamba kipimo cha ugonjwa huo hakilipiwi na bima.

“Nilishawahi kupimwa typhoid mimi binafsi na hata watoto wangu. Lakini mara zote nimekuwa nikiambiwa hicho hakilipiwi na bima,” alisema Anna Kyando, mkazi wa jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Huduma za Matibabu Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Dk David Mwenesano alisema wanachama wao wanalipiwa kipimo hicho kwa sharti la kufuata mwongozo uliopo.

“Kwa mujibu wa mwongozo sisi tunalipia vipimo vya ‘culture’ pekee, yaani vile vinavyotoa majibu baada ya saa 24 vinapatikana kuanzia hospitali za wilaya, hatulipii vipimo vya muda mfupi ‘rapid test’, hivi havipo kwenye mwongozo wa nchi kutambua magonjwa, wakifanya kwa hivyo vipimo hatuwalipi kabisa, lazima wafuate miongozo,” alisema Dk Mwenesano.

Kipimo sahihi

Kwa mujibu wa Msajili wa Maabara binafsi nchini iliyo chini ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dominic Fwiling’afu, mwongozo unaelekeza kuwa kipimo cha ugonjwa wa typhoid huchukua saa 24 mpaka 72 kutoa majibu, kinyume cha hapo hayo majibu si ya kweli na hayana uhalisia.

Fwiling’afu alisema kipimo cha typhoid kilishatolewa mwongozo na kwamba upimaji wa kutumia rapid test hautakiwi, kwani hauna majibu ya uhakika.

“Katika kipimo hiki kwanza itapunguza gharama kwa wananchi, pili usugu wa dawa, watu wanatumia dawa kiholela,” alisema.

Kwa mujibu wa msajili huyo, sheria ya maabara inatakiwa kuomba ridhaa kwa bodi ni vipimo gani itavitumia na kuna vipimo vingine ambavyo hupimwa kuanzia ngazi za hospitali, ni vema kuzingatia miongozo, kwani maabara zisizo na uwezo haziruhusiwi kupima.

“Sheria namba 10 ya mwaka 1997 pamoja na kanuni yake ya mwaka 2005 zinatoa maelekezo thabiti kabisa namna gani ya kuweza kusajili na kuendesha huduma hizi na inatoa katazo kupitia kifungu cha 14 na 15 mtu yeyote haruhusiwi kutoa au kuanzisha huduma hii bila kusajiliwa na usajili unatolewa na bodi ya maabara binafsi Tanzania.

Naye Mtendaji mkuu wa shirika lisilo la kiserikali la RBA Initiative ambaye pia ni Mfamasia, Erick Venant alisema typhoid imejenga usugu wa dawa kwa sababu ya watu kuzitumia kiholela.

Imeandikwa Peter Saramba (Mwanza), Daniel Mjema na Florah Temba (Kilimanjaro), Elias Msuya na Herieth Makwetta (Dar es Salaam), Habel Chidawali na Noor Shija (Dodoma).

Chanzo: mwananchidigital