Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tahadhari kwa watumiaji wa mbolea za viwandani

81802 MBOLEA+OPIC Tahadhari kwa watumiaji wa mbolea za viwandani

Sat, 26 Oct 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mbolea ni chakula cha mimea, ambacho ni mchanganyiko wa virutubisho mbalimbali vinavyoongezwa kwenye udongo au vinavyowekwa moja kwa moja kwenye mimea, ili kuongeza ukuaji na uzalishaji wa mimea.

Virutubisho hivyo ni pamoja na madini muhimu yanayohitajika na mmea kwa kiasi kikubwa kama vile naitrojeni, fosiforasi na potashi. Haya yanahitajika kwa kiasi kikubwa na ndio mana kila mbolea inayotengenezwa kiwandani huwekwa madini haya muhimu matatu.

Madini mengine muhimu ni salfa, chokaa, magneziam, boroni, shaba. Zinki, molybedenum, chuma na mengineyo.

Pamoja na umuhimu huo kwa mimea, yapo makosa ambayo hufanywa na baadhi ya wakulima katika matumizi ya mbolea, hali inayosababisha mimea kudumaa au kupoteza uwezo wa kutoa mazao mengi.

Wapo baadhi ya wakulima wanaotumia mbolea bila kupata ushauri kutoka kwa wataalamu wa kilimo; hawa wanatumia mbolea kwa kufuata mkumbo.

Ramadhani Shabani mkulima wa matikiti mkoani Lindi, ni miongoni mwa wakulima waliokuwa wakifanya makosa ya kutumia mbolea pasipo kufuata taratibu. Yeye alizoea kusikiliza maelekezo kutoka kwa wauzaji wa mbolea badala ya wataalamu wa kilimo.

Pia Soma

Advertisement
Anasema mimea yake ilikuwa ikibadilika rangi na kuwa ya njano akidhani kwamba haikumwagilwa vizuri, matokea yake akawa anapata mazao kidogo tofauti na matarajio yake.

“Nilishawahi kufanya kilimo Wilaya ya Rufiji, nilidumu kwa miezi sita nikaondoka na kuja huku Lindi wakati mwingine nilihisi kama nina mkosi lakini baadaye nilipata ushauri kutoka kwa mmoja wa wataalamu wa kilimo kutoka Naliendele Mtwara kunielezea mbinu bora za kilimo akagusia hilo la mbolea,”anaeleza.

Anasema baada ya ushauri huo na kubadili aina ya mbolea hadi sasa anafurahia maisha ya kilimo chake.

“Alinambia kwanza nipime udongo ili kujua ni aina gani ya mbolea nitumie, lakini pia aliniambia matikiti maji hayahitaji mbolea ya mara kwa mara kwa sababu ni mazao ya muda mfupi na sasa nimepiga hatua kutoka Sh 2.3milioni nilizokuwa napata kwa ekari mbili sasa napata Sh 5 milioni,”.

Naye Aisha Bendera ambaye ni mkulima wa mbogamboga katika bonde la Chang’ombe lililopo Temeke jijini Dar es Salaam anasema matumizi yasiyo sahihi ya ambolea yalimsababishia hasara ya zaidi ya Sh 600,000 baada ya kuotesha vitalu sita vya mbogamboga na baadaye kudumaa.

Anasema kilichomponza ni kufuata mkumbo baada ya kuona mkulima mwenzake ambaye wanapakana katika bonde hilo akitumia mbolea.

“Nilikuwa natumia mbolea ya kinyesi cha kuku kila wakati, baada ya kuona jirani yangu anatumia mbolea ya viwandani na mimi nikaaza kutumia. Nakumbuka ilikuwa kama chenga chenga nikaamua kutumia nikidhani kuwa mbogamboga zitastawi matokeo yake zikabadilika rangi na kuwa njano,” anasema na kuongeza:

“Sikujua kuwa tatizo ni ile mbolea na sikuwahi kuuliza namna ya kuitumia na baada ya kuona hali inazidi kuwa mbaya ikabidi niulize kwa watu tofauti na wakaniambia niache kutumia mbolea hiyo kwani ndiyo chanzo cha mazao yangu kudumaa.”

Wasemavyo wataalamu

Mkufunzi masuala ya kilimo kutoka Chuo cha Kilimo Tengeru kilichopo Arusha, Suleiman Mkingama anataja aina mbili za mbolea ikiwamo Urea anayosema hutumika katika kupandia. Ni mbolea muhimu inayopaswa kutumika mmea unapoanza kuota.

Anasema wakulima wengi wanakosea kwenye vipimo, kwani kila mbolea ina kiasi ambacho mkulima anatakiwa kutumia.

“Kwa mfano kama atazidisha kipimo cha mbolea mmea unakuwa sana na hautoi mazao mengi, lakini vilevile kama atatumia mbolea kidogo mmea utadumaa,”anasema na kuongeza:

“Kingine wakulima wanakosea kwenye uwekaji wa mbolea hawana uelewa wa kutosha ni hatua gani, kwa mfano mbolea ya kupandia inatakiwa kutumika mmea unapoota na ya kukuzia mkulima atatakiwa asubiri hadi mmea ufike magotini.”

Kutokana na uzoefu wake, anasema amebaini kuwa wakulima wengi wanatumia mbolea bila kupima udongo.

“Kabla hajatumia mbolea mkulima anatakiwa kupima aina ya udongo kwa sababu siyo kila udongo unatakiwa kutumia mbolea. Lakini pia utakapopima udongo ni rahisi kufahamu kuwa inahitajika mbolea kiasi gani kwa sababu kuna sehemu inahitajika kidogo na kuna sehemu inahitajika kwa wingi. Suala hili ni muhimu na mkulima anapaswa kulizingatia,”anasema.

Kaimu mkurugenzi mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania Dk Stephan Ngailo anasema kabla ya kutumia mkulima anatakiwa kufahamu anatumia mbolea ya aina gani.

“Wakulima wengi wanakosea, anatumia tu mbolea kiholela kwa sababu tu kaona mwenzake anatumia na yeye anaingia kwenye mkumbo wa kutumia mbolea,”anasema.

Anasema baada ya kuandaa shamba mkulima anatakiwa kutumia mbolea ya kupandia ambayo inasaidia kurahisisha uotaji wa mizizi ya. Hata hivyo, anashauri kabla mkulima hajatumia mbolea hiyo, ahakikishe kuwa ardhi yake ina unyevunyevu wa kutosha.

“Baada ya kupanda mkulima anaweza kutumia mbolea ya kukuzia lakini hapa nitoe angalizo siyo kila mimea mkulima anahitaji kutumia mbolea kwa hiyo anatakiwa kupata ushauri kutoka kwa wataalamu wa kilimo waliopo katika maeneo mbalimbali,”anasema.

Anaongeza: “Ikiwa wataalamu watajiridhisha kuwa unaweza kutumia mbolea ya kukuzia, basi itumike kwa usahihi kwani mbolea hii inasaidia mmea kutengeneza chakula cha kutosha kwa ajili ya ukuaji,”.

Anasema madhara ya matumizi yasiyo sahihi ya mbolea ni kutopata matokea mazuri… “Kwa sababu kila mkulima anaingia shambani akiwa na matarajio ya kupata mazao mengi hivyo akifanya kosa katika matumizi ya mbolea, hawezi kufikia malengo yake aliyoyatarajia.’’

Chanzo: mwananchi.co.tz