Mtaalamu wa afya nchini Uingereza ametoa tahadhari ya kiafya dhidi ya tabia ya kutobadilisha chupi kila siku, baada ya kufanya uchunguzi uliobaini kuwapo tatizo la kiafya kwa wanaovaa chui zaidi ya siku moja.
Kwa mujibu wa daktari huyo ambaye ni mtaalamu wa afya kwenye vipindi vya televisheni nchini Uingereza, Dk Jen Caudle alisema katika uchunguzi uliofanywa kwa zaidi ya wakazi 2,000 wa Uingereza kuhusu tabia zao za uvaaji chupi, walipata matokeo ya kutatanisha.
Alisema kati ya watu waliowahoji, asilimia 54 ya washiriki walisema huwa wanafua chupi zao kila baada ya kuvaa mara moja. Katika matokeo hayo, mwanamume mmoja kati ya watano, alikiri kufua chupi yake baada ya kuivaa kwa wiki nzima.
“Cha kushtua zaidi ni kwamba asilimia tano ya wanaume walisema kuwa wanavaa chupi kwa muda wa wiki mbili hadi tatu kabla ya kuifua.”
Alisema wanawake wengi (asilimia 81) walisema wanabadilisha chupi kila siku, huku asilimia tisa wakikubali kuwa wanavaa chupi moja hadi wiki au zaidi kabla ya kuifua.
Dk Caudle ambaye hukusanya mamilioni ya maoni kwenye video zake za TikTok, alishauri watu wawe wanabadili chupi kila siku kwa sababu za kiafya.
"Kubadilisha nguo zako za ndani kila siku kunasaidia kupunguza hatari ya unyevunyevu kunaswa kwenye sehemu yako ya siri na kupata maambukizi ya bakteria na vitu kama hivyo," alisema Dk Caudle.
Aliongeza kuwa kutobadili chupi kila siku kunaongeza hatari ya magonjwa ya ngozi. Hata hivyo, wataalamu wa ngozi wanasema wanaume wanaweza kuvaa suruali moja kwa siku kadhaa bila kubadilisha bila tishio la kiafya.
Daktari wa ngozi katika kiliniki ya michezo, alisema hii inatumika tu katika hali ambapo mtu anafanya shughuli nyepesi na hatoki jasho.