Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tafiti 50 za tiba asili zafanyika nchini

Dkt Mollel Abainisha Mikakati Ya Kupambana Na Saratani Tafiti 50 za tiba asili zafanyika nchini

Thu, 15 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Zaidi ya tafiti 50 juu ya ubora na usalama wa dawa zinazotumika kwa tiba asilia zimefanyika kupitia Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) kati mwaka 2021 hadi 2024.

Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel amesema hayo leo Alhamisi, Februari 15, 2024 alipojibu swali la msingi la mbunge wa Baraza la Wawakilishi, Ameir Abdallah Ameir.

Ameir amehoji ni tafiti zipi ambazo taasisi za tiba asili zimekamilisha na kuwa suluhisho la maradhi kama tiba mbadala.

Dk Mollel amesema kuanzia mwaka 2021 hadi 2024 zaidi ya tafiti 50 zimefanyika ndani ya nchi juu ya ubora na usalama wa dawa zinazotumika kwa tiba asilia kupitia NIMR.

Amesema baadhi ya tafiti hizo ni wa dawa ya saratani ya Nimregenin, Tanghesha inayotibu selimundu, Pervivin inayotibu tezi dume, Warbugistat inayotibu magonjwa nyemelezi na Nimricaf inayotibu mfumo wa upumuaji.

Katika swali la nyongeza, Ameir amesema zaidi ya asilimia 60 ya Watanzania wanatumia tiba asili na miti ya tiba dawa iko 12,000.

Amehoji ni miti gani inatumika kutengeneza dawa za asili na Serikali ina mkakati gani wa kunusuru miti asili iliyo hatarini kutoweka.

Dk Mollel amesema ipo miti mingi ya kutengeneza dawa, ikiwamo inayotengeneza dawa za Alu na Quinidine.

Amesema wanalichukua suala hilo na kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii kuhakikisha miti inatunzwa.

Dk Mollel amesema watashirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kutengeneza watu wengi wenye akili vumbuzi.

Februari mwaka 2021, aliyekuwa Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Abel Makubi aliwataka wasomi na wataalamu wa afya kwa ujumla kubadili mtazamo juu ya tiba asili kwa kuwa zina mchango mkubwa wa kutibu magonjwa ya binadamu.

“Kama dawa sisi tumeshaihakiki na tukaikubali kwamba ni dawa salama, basi pasiwepo na kinyongo au ugumu wowote wa sisi watumishi wa afya kuruhusu mwananchi kutibiwa kwa dawa hiyo,” alisema Profesa Makubi ambaye sasa ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI).

Agosti mwaka 2023, katika ufunguzi wa kongamano la pili la kisayansi na maonyesho ya dawa za tiba asili, Mkurugenzi wa Tiba kutoka Wizara ya Afya, Profesa Paschal Ruggajo alisema Serikali imeanza tiba jumuishi katika hospitali za rufaa saba nchini.

Alizitaja kuwa ni hospitali za Rufaa za Temeke (Dar es Salaam), Morogoro, Dodoma, Sokou Toure (Mwanza), Mount Meru (Arusha), Bombo (Tanga) na Mbeya.

Dawa hizo ni Planet, Uzima, Shengena, Inkorora, Joy, Immunege, Africov, Life, Duraki, Coviba, Novirusa, Bupui, Kivambo, Valix, Boavix, Euclex, Pumax, Peptin, Sarax, Sphagnex, Ocyvox na Goshen.

Baadhi ya magonjwa yanayotibiwa na dawa hizo ni vidonda vya tumbo, tezi dume, pumu, homa ya matumbo, mambukizi ya mfumo wa hewa, maambukizi ya njia ya mkojo (UTI), kuungua na amiba.

Mengine ni maumivu makali siku za hedhi, kutopata hedhi (picou) gauti na mengine ya jointi, fangasi wa kucha, shinikizo la damu, kutowiana kwa homoni, uvimbe katika kizazi na kuharisha.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live