Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tacaids: Wafanyakazi walia uhaba wa kondomu maofisini

Uhaba Kenya Kondomu Tacaids: Wafanyakazi walia uhaba wa kondomu maofisini

Thu, 17 Aug 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakati ikionekana tamaa za kimapenzi mahala pa kazi ni jambo la kawaida, huku wengine wakitumia ushawishi wa rushwa ya pesa au vyeo ili kufanya ngono na wanaowataka, imeelezwa kuwa uhitaji wa kondomu ofisini ni muhimu.

Hali hiyo ya ushawishi wa ngono inashabihiana na tafiti mbalimbali, ikiwamo ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa) mwaka jana.

Kutokana na mazingira hayo, Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (Tacaids) jana ilitoa angalizo linalohitaji umakini wa kuzingatia tahadhari za kujikinga na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU).

“Hali sio mbaya sana mahali pa kazi, lakini kiwango cha mahitaji ya kondomu ni kikubwa sana,” alisema Mkurugenzi wa Uraghibishi na Habari wa tume hiyo, Jumanne Isango katika mkutano wa wadau kujadili masuala ya usalama wa afya ya mfanyakazi chini ya Taasisi ya Waajiri Tanzania (ATE).

Licha ya kutokuwa na takwimu za hali ilivyo kwenye maeneo ya kazi, Isango alisema taasisi na wizara zimeendelea kuwasilisha maombi kwa ajili ya mahitaji ya kondomu.

“Taasisi zimekuwa zinaomba kondomu kupitia utaratibu wa Tacaids inayowasiliana na wadau na kondomu zinafika pale, tumefunga condom dispensers (makasha) ya kuhifadhi kondomu karibu kila wizara, kila taasisi ziko pale ili watu kujikinga na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi,” alisema Isango.

“Hatusemi ndio watu wanaofanya sana ngono kazini, inamaanisha kuna wakati utazihitaji, utachukua pale kazini kwa ajili ya kutumia, maombi pia ya makasha kwenye taasisi za Serikali, idara ni mengi, tunahitaji kusambaza na hata nyie waandishi wa habari mnaweza kuyaona huko tulivyofunga.”

Kwa mujibu wa Tacaids, hadi Februari mwaka jana idadi ya watu wanaofahamu kuwa wanaishi na VVU ni asilimia 84, asilimia 98 wanatumia dawa za kufubaza VVU (ARVs) na asilimia 92 wanaotumia ARVs wamefubaza virusi vya Ukimwi.

Hata hivyo, Isango alisema pamoja na mwitikio huo, Ukimwi bado upo, akisisitiza kila ofisi ya umma na binafsi kuzingatia Mwongozo wa Kudhibiti Maambukizi ya Ukimwi na magonjwa yasiyoambukizwa mahala pa kazi wa 2016, unaoelekeza kutoa mafunzo, upimaji binafsi na elimu ya matumizi ya kondomu. Pamoja na uwepo wa kondomu za kutosha nchini, Isango alisema changamoto bado ipo kwenye usambazaji wa kondomu hizo maeneo mbalimbali nchini. “Wakati mwingine unakuta ziko kituo cha afya lakini hazijasambazwa, tunataka waratibu wa wilayani wasaidie kusambaza kwenye maeneo ya jamii,” alisema.

Kwa mujibu wa Tacaids, mwongozo huo unaagiza kwa lazima taasisi zote kuandaa mpango kazi wa utekelezaji wake utakaofanyiwa tathimini kila baada ya miezi mitatu, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuelekea kwenye utekelezaji wa malengo ya kimataifa ya 95-95-95.

Henry Mkunda, Katibu wa Shirikisho la Vyama 13 vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), alisema wanaendelea kusisitiza waajiri kutambua umuhimu wa afya za wafanyakazi. “Tunashauri waweke mipango kazi ya kutekeleza mwongozo, na wawe na bajeti ya kufuatilia afya zao,” alisema Mkunda, aliyewakilisha vyama hivyo 13 vyenye wanachama wake zaidi ya milioni 2.5 nchini. “Kwa sababu mfanyakazi akiwa na afya njema ndio chanzo cha kampuni kuwa na uzalishaji mzuri, ambao ndio msingi wa uchumi wa taifa, isiwe VVU tu ila hata magonjwa mengine.” James Kahatano, Meneja Rasilimali Watu katika Kampuni ya Uwakala wa Ajira ya Erolink Tanzania Limited alisema tayari kampuni hiyo imeendelea kutekeleza mwongozo kwa njia ya huduma za kondomu, ikiwa ni sehemu ya kusaidia juhudi za Serikali katika kukabiliana na changamoto hiyo. “Erolink imeendelea kutekeleza kwa vitendo juhudi za kulinda afya ya mfanyakazi, kupitia mwongozo tunaopewa na ATE, tunao wafanyakazi takribani 250 na tumekuwa tunaweka kondomu zaidi ya 100 kila siku za kazi, na zinakwisha ndani ya saa tatu, pia tunatoa elimu ya kufanya vipimo,” alisema Kahatano. Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waajiri Tanzania (Ate), Suzanne Ndomba alisema mkutano huo wa kuongeza uelewa wa afya mahali pa kazi utahusisha pia mafunzo kwa baadhi ya maofisa watakaosaidia kushusha maarifa hayo ngazi za wafanyakazi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live