Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tabia zako ndicho chanzo cha maradhi ya kisukari

Sun, 1 Jul 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Ulaji wako ndiyo mchawi wako. Ndivyo unavyoweza kusema kwa sababu wataalamu wa afya wanathibitisha kuwa aina ya vyakula tunavyokula ndicho chanzo cha magonjwa yasiyoambukiza.

Shirika la Afya Duniani (WHO) linaeleza kuwa, asilimia 30 ya vifo vinavyotokea nchini husababishwa na maradhi yasiyoambukiza. Maradhi hayo ni pamoja na kisukari, saratani, moyo na mfumo wa upumuaji.

Akizungumza juzi, katika mjadala wa kwanza wa Mwananchi Jukwaa la Fikra ulioandaliwa na kampuni ya Mwananchi Communication, Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Kupambana na Magonjwa Yasiyo ambukiza (Tancda), Andrew Swai alisema unapokula vyakula vyenye sukari nyingi, vikiingia tumboni hukutana na hewa kisha nguvu hutengenezwa ambayo huchoma baadhi ya viungo mwilini.

Profesa Swai anasema kwa bahati nzuri magonjwa yasiyoambukiza yanaweza kuzuiwa kwa kuwa hutengenezwa na binadamu kutokana na mtindo wa maisha.

“Tunaweza kuzuia magonjwa haya kwani tunayatengeneza sisi wenyewe, lazima tuhakikishe tunafanya linalowezekana ili kuhakikisha tunatatua tatizo hilo,” anasema.

Akizungumzia zaidi kuhusu ugonjwa wa kisukari, Profesa Swai anasema ili binadamu aishi anatakiwa kula chakula apate nguvu na aweze kupumua.

“Hilo ni zoezi la tangu kuzaliwa hivyo lazima sukari ipatikane mwilini ili ubongo, maini, figo, mapafu yaafanye kazi,” anasema, lakini anaonya kwamba vikizidi huleta madhara. “Sasa sukari inatakiwa kuja kidogokidogo kadri inavyohitajika, mfano ukichoma nyama ukazidisha moto nyama inaungua na hata mwilini mwako sukari inaongeza nguvu lakini ikizidi ile nguvu ya ziada itachoma mwili, ndiyo maana wenye kisukari wanapofuka macho, mishipa ya fahamu, figo na mishipa ya damu.”

Profesa Swai anasema mwili hauna uwezo wa kuizuia sukari ikishakutana na hewa na ni lazima itengeneze nguvu. “Ukianza kula vyakula vyenye sukari nyingi tangu utotoni, ukifika miaka 40 ile nguvu ya ziada iliyozalishwa na sukari inaanza kuchoma viungo vya mwili, tayari ulishapata kisukari.”

Profesa Swai anatoa mfano akisema maziwa ya mama ni majimaji lakini yakifika tumboni huganda na mtu akila matunda kwa kuyakamua yanapita moja kwa moja na sukari itaingia mwilini na itamchoma.

Anashauri matunda yaliwe kwa kutafunwa zaidi na si kusagwa au kukamuliwa.

“Vyakula vya wanga vinaingia mwilini na vina sukari, vikifika tumboni humeng’enywa na mfumo maalumu, lakini sisi tunakosea tunapokoboa. Magamba yanakusaidia kupata choo, tukikoboa sana vinarudi mwilini na ndiyo sababu ya saratani,” anasema.

Tafiti ugonjwa wa kisukari

Profesa Swai anasema magonjwa yasiyoambukiza yanaongezeka kwa kasi nchini. Utafiti uliofanywa mwaka 1980 ulionyesha kuwa asilimia moja ya watu mijini walikuwa na kisukari.

Anasema ilipofika mwaka 2012 utafiti ulionyesha asilimia tisa ya watu wana kisukari na asilimia tano walikuwa na shinikizo la damu, lakini sasa asilimia 26 ya Watanzania wana shinikizo la damu.

“Wizara imebaini kuwa asilimia 22 ya Watanzania wana kisuakri na asilimia 31 wana shinikizo la damu, wengine hawajijui. Lakini ukiamua kuwatibu hawa utatumia asilimia saba ya bajeti yote ya afya na asilimia 20 ya bajeti ya mfuko wa huduma za jamii (NHIF), ni mzigo ambao hatuwezi kuubeba,” anasema.

Hata hivyo anasema bajeti ya nchi ni ndogo na iwapo sera itatekelezwa haiwezi kutosheleza mahitaji.

“Chama cha wagonjwa wa kisukari tumekaa kimya kwa maana sera yetu inasema kwamba wagojnwa wa kisukari wapewe dawa bure, lakini utafanya hivyo hiyo fedha itoke wapi haiwezekani hilo ni tatizo kubwa,” anasema.

Profesa Swai anasisitiza kuwa ni lazima kila mtu ahakikishe kuwa hazidishi vijiko vitano vya sukari kwa siku kwani matumizi makubwa ya sukari na chumvi ndicho chanzo cha maradhi yasiyoambukiza .

“Ili nchi ipambane na maradhi haya ni vyema watu wakaacha matumizi ya vyakula visivyofaa, matumizi ya sigara, pombe kupita kiasi,” anasema.

Mazoezi huepusha kisukari

Anasema mtu anapokula vyakula vinavyoongeza mafuta kwa wingi mwilini au sukari nyingi ni lazima ahakikishe anafanya mazoezi.

“Naonya hili kwa sababu ni hatari kwa afya yako,” anasema.

“Unapofanya mazoezi bila shaka mafuta yanajichoma yenyewe mwilini na unabaki ukiwa na yale yanayohitajika kwa wakati huo pekee, la sivyo kwa kutofanya mazoezi yatasalia mwilini na kukuletea madhara.”

Anasema kuwa miezi tisa mtoto huishi ndani ya tumbo la mama akiwa amejikunja, lakini akitoka anahitaji miaka miwili aweze kutembea na asipofanya mazoezi misuli inasahau kutumia sukari.

“Mazoezi ni ya kila siku mpaka kufa, usipofanya mazoezi unahatarisha afya yako,” anasema.

Anasema mazoezi humfanya mtu avuje jasho na bila kufanya hivyo huifanya sukari ishindwe kufanya kazi vizuri mwilini.

“Usipokuwa makini sehemu ya kongosho, maini, mapafu zote zitakwisha. Hatuna viungo vya ziada tuna mapafu mawili, tuna figo mbili na kongosho,” anasisitiza.

Mwanafunzi wa udaktari Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili (Muhas), Lusia Silayo anasema kasi inayofanywa na Serikali kupambana na magonjwa yanayoambukiza inapaswa kutumika kwa yale yasiyoambukiza.

“Vilevile kuelimisha jamii kuhusu magonjwa yasiyoambukiza ambayo yanakua kwa kasi na tunayasahau,” anasema Lusia.

Mwanafunzi wa udaktari kutoka Muhas, Daniel Magomele anashauri kuanzisha kitengo cha tiba kinga kwa kila hospitali ambacho kitaendeshwa kwa mfumo wa kliniki. “Napendekeza kaulimbiu iwe ‘Onana nami kabla hujaugua’ na katika kitengo hiki napendekeza kuwepo na dodoso linalojijibu lenyewe, mhusika aone yupo kwenye hatari kiasi gani kupata magonjwa yasiyoambukiza,” anasema.

Mkurugenzi mkuu wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (Nimr), Profesa Yunus Mgaya anasema ni vyema Serikali ikatenga bajeti ili kupambana na maradhi yasiyoambukiza.

“Katika tafiti zetu tunazofanya sasa tunaangalia namna ya kupunguza au kutokomeza kabisa maradhi yasiyoambukiza kwa kuangalia viashiria vinavyosababisha,” anasema Profesa Mgaya.

Chanzo: mwananchi.co.tz