Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Taasisi ya moyo na hatua nyingine kubwa

5ce01c8a1e62f0cb0d2893297809e790 Taasisi ya moyo na hatua nyingine kubwa

Thu, 22 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MOYO ni kiungo muhimu katika maisha ya mwanadamu kinachomsaidia kuishi. Hata hivyo, moyo umekuwa ukipata mashambulizi ya maradhi mbalimbali na kusababisha watu kupoteza maisha na hivyo kupoteza nguvu kazi kubwa ya taifa na gharama kubwa ya matibabu nje ya nchi.

Ili kupunguza madhara ya maradhi ya moyo kwa wananchi na gharama kubwa za matibabu nje ya nchi, serikali iliamua kuanzisha Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Septemba 5, mwaka 2015 kupitia tangazo la Serikali namba 414 ili wagonjwa wenye matatizo ya moyo waweze kutibiwa hapa nchini.

JKCI ndio hospitali maalumu na pekee ya magonjwa ya moyo inayomilikiwa na serikali inayofanya tiba ya maradhi ya moyo nchini. Hutibu na kufanya upasuaji wa moyo kwa watoto na watu wazima.

Mkurugenzi Mkuu wa JKCI, Profesa Mohamed Janabi, anasema mbali na huduma za tiba, ni kitivo kwa ajili ya mafunzo ya madaktari na wauguzi kwa magonjwa ya moyo, kituo cha utafiti wa magonjwa hayo katika hali ya ngazi ya juu kabisa ya taaluma.

Profesa Janabi anasema taasisi hiyo yenye wafanyakazi 309 ikijumuisha madaktari bingwa, wauguzi mabingwa, mafundi wasanifu na wa kada nyingine, ni tegemeo, si tu kwa Watanzania bali mataifa mbalimbali.

Anasema ikiwa na vitanda 150, vyumba vitatu vikubwa vya upasuaji mkubwa wa moyo, mtambo mkubwa wa upasuaji kwa kutumia tundu dogo, vitanda 23 vya wodi za uangalizi maalumu (ICU) vinavyokidhi viwango vilivyowekwa na Shirika la Afya Duniani (WHO), inahudumia wananchi wa mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar na mataifa zaidi ya 10.

“Kila aina ya magonjwa ambayo yanahusiana na moyo yanapata tiba katika hospitali yetu. Imekuwa mkombozi mkubwa, si tu kwa wagonjwa wanaotoka mikoa yote nchini Bara na Zanzibar, lakini pia wagonjwa kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Malawi, Zambia, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Visiwa vya Comoro na balozi zote zilizopo jijini Dar es Salaam,” anaeleza Profesa Janabi.

Ikiwa na dira kuu ya kuwa na kiwango cha juu cha kimataifa katika huduma za moyo katika nyanja zote za matibabu, usimamizi na utafiti duniani, wiki hii imeandika historia kubwa ya kipekee katika upasuaji wa moyo.

Kwa mara ya kwanza imefanikiwa kufanya operesheni kubwa mbili ikiwamo upasuaji mkubwa wa kupandikiza mishipa ya damu huku moyo ukiendelea kupiga kwa wagonjwa 22 nchini na upasuaji wa mshipa mkubwa wa moyo uitwao Aorta.

Kwa miaka mitano sasa, JKCI imekuwa ikifanya upasuaji wa kupandikiza mishipa ya damu kwa kusimamisha moyo usiendelee na mapigo kwa muda wote wa upasuaji na kisha kuurejesha katika hali ya kawaida baada ya operesheni na haijawahi kufanya upasuaji wa Aorta.

Hatua hiyo ya kupandikiza mishipa ya damu huku moyo ukipiga, imeongezea ujuzi wa kipekee na mkubwa taasisi hiyo kwani sasa hatari ya wagonjwa wa aina hiyo kupoteza maisha inapungua, muda wa operesheni na wa mgonjwa kukaa hospitali baada ya upasuaji, unapungua.

Faida nyingine ya upasuaji huo ni kwamba, gharama zake zinapungua ikilinganishwa na kama wagonjwa hao wangepatiwa matibabu hayo nje ya nchi.

Profesa Janabi anaeleza kwamba operesheni hizo zimegharimu Sh milioni 330 kwa wagonjwa wote 22 ikiwa ni sawa na Sh milioni 15 kwa kila mtu na kuokoa Sh milioni 660 kama wagonjwa hao wangepelekwa nje ya nchi kwa matibabu hayo. Nje ya nchi gharama ingekuwa Sh milioni 990.

Taasisi hiyo katika kuelekea kuwa kituo cha umahiri wa tiba ya moyo, si tu Afrika bali duniani kote, inajiandaa mwishoni mwa mwaka huu (2021) au mwanzoni mwa mwaka ujao, kuanza kufanya upasuaji wa tundu dogo la kifua kupandikiza mishipa hiyo ya damu.

Hivi sasa wanapasua kifua chote kufanya upasuaji huo wa kupandikiza mishipa ya damu ingawa wanafanya upasuaji wa tundu dogo kwa matatizo mengine ya moyo.

Kwa mara ya kwanza JKCI ilifanya upasuaji wa kupandikiza mishipa ya damu kwa mgonjwa wa kwanza mwaka 2016, mwaka mmoja baada ya kuanzishwa.

Profesa Janabi aliwaambia waandishi wa habari wiki hii kuwa, upasuaji huo wa kupandikiza mishipa ya moyo ukipiga umefanyika kwa mara ya kwanza katika taasisi hiyo kwa wagonjwa hao 22 na kama kusingekuwa na changamoto kubwa ya damu inayowasumbua hivi sasa, wangeweza kufanya upasuaji huo kwa wagonjwa wengi zaidi kutokana na uwezo mkubwa walionao.

Anasema upasuaji huo umefanyika kwa ushirikiano wa daktari bingwa wa moyo kutoka nchini India, Profesa Subhash Sinha ambaye ni daktari bingwa wa moyo kwa zaidi ya miaka 37 sasa na hivyo madaktari wa taasisi hiyo wameongezewa ujuzi huo mpya na wameiva katika kuendelea kuwahudumia wananchi.

“Sababu kubwa tuliomwitia kuja kushirikiana na sisi hapa kwenye mambo ya upasuaji wa moyo ni kufanya upasuaji wa kupandikiza mishipa ya damu wakati moyo unapiga. Si kwamba sisi tulikuwa hatufanyi lakini tofauti kubwa ni kwamba sisi tunasimamisha moyo kabisa na baada ya hapo tunaushtua moyo na kukamilisha operesheni,” anasema Profesa Janabi.

Akieleza tofauti ya operesheni hizo mbili, anasema operesheni ya kupandikiza mishipa ya damu wakati moyo unapiga inamsaidia mgonjwa kukaa muda mfupi zaidi hospitali kati ya siku 10 mkapa 14 kabla ya kuruhusiwa kurudi nyumbani na muda wa operesheni pia unakuwa mfupi (kati ya saa moja hadi tatu) na changamoto zinapungua tofauti na kusimamisha moyo kabisa.

Profesa Janabi pia anasema kupitia upasuaji huo, kwa mara ya kwanza pia wamefanikiwa kufanya upasuaji katika mshipa mkubwa wa moyo wa Aorta ambao walikuwa hawajawahi kufanya katika taasisi hiyo ikiwa ni hatua ya kujaribu kuongeza huduma mpya za kibingwa za moyo nchini.

“Napenda kusema kuwa operesheni hii ya kupandikiza mishipa wakati moyo unapiga, wagonjwa wote wapo salama na wengine wameruhusiwa kurudi nyumbani. Lakini tumepoteza wagonjwa watatu katika ule upasuaji mwingine wa mshipa mkubwa wa moyo kwa tuliowafanyia,” anasema Profesa Janabi.

Anasema tatizo linaloongeza hatari ya wagonjwa kupoteza maisha ni kufika hospitali wakiwa katika hatua mbaya za ugonjwa zinazowaachia asilimia 25 ya kuishi hivyo kitabibu madaktari wanapambana kutumia ujuzi wao wa mwisho kuokoa maisha ya mtu huyo ingawa moyo unakuwa umechoka mno.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Upasuaji wa taasisi hiyo, Dk Angela Muhozya, anasema JKCI imeshafanya upasuaji wa kupandikiza mishipa ya damu kwa kusimamisha moyo kwa wagonjwa zaidi ya 100 lakini changamoto kubwa ilikuwa muda mrefu wa operesheni na utaalamu huo mpya utawawezesha kuendelea na huduma hiyo bila kusimamisha moyo.

“Lakini pia Profesa Sinha ana mambo mengi ya kutufundisha, natumaini atakuja tena kwa ajili ya kufanya operesheni kwa kupasua tundu dogo kwenye kifua. Nia ya JKCI ni kuwa kituo cha umahiri wa tiba,” anasema Dk Muhozya.

Wawakilishi wa madaktari waliopata ujuzi huo kwa kushiriki kufanya operesheni hizo 22, ambao ni madaktari bingwa wa upasuaji wa moyo, kifua na mishipa ya damu, Dk Alex Joseph na Dk Moses Byomuganyizi, wanasema kwa nyakati tofauti kuwa, ujuzi walioupata ni mkubwa na wapo tayari na mahiri kuwahudumia wananchi na wagonjwa wote.

Dk Joseph anasema awali operesheni hiyo ya kusimamisha moyo waliifanya kwa kati ya saa nne hadi sita lakini sasa ni saa mbili hadi mbili na nusu. Anasema operesheni zote 22 kwa asilimia 90 walifanya wao wakiongozwa kitaaluma na Profesa Sinha hivyo wameiva kuwahudumia Watanzania na wagonjwa watakaokuwa na tatizo hilo.

Akifafanua zaidi, Dk Byomuganyizi anasema katika upasuaji huo madaktari wote wa upasuaji wa moyo wameshiriki, jambo ambalo ni gumu kupata fursa hiyo kama wangepelekwa wao nje kujifunza.

Naye Profesa Sinha anasema anaiona JKCI kama kituo kikubwa cha umahiri wa tiba ya moyo Afrika katika miaka miwili ijayo kutokana na aina ya matibabu wanayotoa na kuendelea kuwezesha tiba zinazotumia teknolojia mpya huku akiwashauri waendelee kuwekeza vifaa na mashine za kisasa zaidi.

“Ni mara yangu ya kwanza kuja Tanzania, nimepata uzoefu mkubwa na mzuri sana hapa. Baada ya miaka miwili hadi mitatu hapa patakuwa kituo cha umahiri wa tiba ya moyo Afrika kwa kuwa hatua wanayopiga ni kubwa,” anasema Profesa Sinha ambaye alipata shahada ya udaktari mwaka 1977 na udaktari bingwa mwaka 1983.

Tanzania imekuwa ikifanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya afya, hatua ambayo inaonekana dhahiri kwamba itatoa mchango mkubwa siku za usoni kwa kuwezesha nchi kuendesha utalii wa matibabu.

Nchi nyingi zimekuwa zikiweka mazingira mazuri ya Utalii wa Matibabu kwa ajili ya kukuza na kuchochea uchumi wao. Ukitaja nchi ambazo zimekuja juu sana kwa utalii wa matibabu duniani huwezi kuacha kuizungumzia India inayotoa matibabu ya hali ya juu na kwa gharama ya chini.

Kwa mfano, gharama za upandikizaji wa ini nchini Marekani ni zaidi ya dola laki tatu lakini India haizidi dola laki moja. Vivyo hivyo, upasuaji wa moyo kwa Marekani hugharimu takribani dola 120,000 wakati India inakadiriwa kuwa ni nusu ya gharama hizo.

Kutokana na ukweli huu wagonjwa husafiri kutoka Marekani kwenda nchi za Asia kwa ajili ya matibabu ambayo gharama zake ziko chini zaidi ya nchi zao.

Sababu nyingine ya watu wengi kuamua kusafiri nje ya nchi zao ni muda wa kusubiri matibabu kwani ugonjwa huwa hausubiri na hivyo mwenye fedha zake huona ni vyema kusafiri na kufanyiwa matibabu kwa haraka ili arudi kuendela na majukumu yake.

Chanzo: www.habarileo.co.tz