Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Taasisi ya Ifakara yaomba vitendanishi serikalini

Sun, 2 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Taasisi ya Afya ya Ifakara (IHI) wilayani Kilombero mkoani Morogoro imeiomba Serikali kuondoa changamoto mbalimbali zinazoikabili ikiwemo kuipatia vitendanishi vya kupima kiwango cha wingi wa vimelea vya HIV kwenye damu.

Hayo yamebainishwa na mtafiti mkuu wa maabara wa taasisi hiyo, Farajo Abilahi katika taarifa yake aliyoitoa mwishoni mwa wiki kuhusu mafanikio na changamoto za taasisi hiyo kwa madiwani na viongozi wa serikali wa halmashauri za wilaya ya Ulanga na Kilombero waliotembelea taasisi hiyo.

Amesema vitenganishi vilivyopo ni vichache hali inayosababisha mashine ya kituo hicho kutofanya kazi kama inavyotakiwa na kusababisha uchelewaji wa kutoa majibu ya vipimo kwa wagonjwa hasa kutoka wilaya tatu za Malinyi, Kilombero na Ulanga zinazoizunguka taasisi hiyo.

Mtafiti huyo amesema kwa sasa upimaji wa wingi wa vimelea vya HIV kwenye damu unafanywa na hospitali kuu ya mkoa wa Morogoro tu na kuongeza uamuzi wa serikali kuipatia vitendanishi taasisi hiyo utasaidia kupunguza mrundikano wa sampuli za damu kwenye hospital yake ya mkoa.

“Fedha za miradi hutumika tu kwa kazi za utafiti na kuacha fedha kidogo kwa ajili ya maendeleo ya tassisi. Tunaiomba serikali itusaidie kupata vitendanishi kwa ajili ya kupima kiwango cha HIV kwenye damu ili tuweze kuhudumia wananchi kwa ukamilifu zaidi,” Abilahi amesema.

Akizungumzia mafanikio, mkuu huyo wa maabara amesema taasisi yake ndio pekee Afrika kufanya jaribio la chanjo ya ugonjwa hatari wa malaria nchini na duniani.

Ameongeza IHI imeshiriki kwenye tafiti zilizopelekea kutumika kwa vyandarua vyenye dawa Tanzania na mahali pengine duniani na ndiyo taasisi iliyogundua njia mpya ya kuzuia malaria kwa kutoa dawa za malaria kwa watoto wakati wa mahudhurio ya kliniki, yaani ‘intermittent Preventive Treatment’

Mkuu wa wilaya ya Kilombero, James Ihunyo amesema ofisi yake italiwasilisha ombi hilo kwenye sekretarieti ya mkoa kwa ajili ya utekelezaji zaidi kwenye vikao vya serikali ngazi mbalimbali.

Amesema Serikali ni mdau muhimu kwenye suala la afya kwa hiyo inawajibika moja kwa moja kuhakikisha afya za wananchi zinakuwa bora kwa kuboresha huduma ya afya katika ngazi zote kuanzia wilaya, mkoa mpaka Taifa.

“Napenda nipongeze juhudi kubwa na mchango unaofanywa na taasisi hii katika wilaya yangu ya jirani na hata mkoa kwa ujumla. Ninawiwa kuhakikisha huduma itolewayo inakuwa bora zaidi kwa kuunga mkono huduma zinazotolewa,” amesema  Ihunyo.

“Kama serikali tutaendelea kuunga mkono juhudi hizi kwa kuwasilisha hili kwenye sekretarieti ya mkoa ambayo itajadili na kulifanyia utekelezaji kadri itakavyoona inafaa kwa maslahi mapana ya ustawi wa afya za wananchi,” ameongeza.

Chanzo: mwananchi.co.tz