Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Taasisi ya Afya Ifakara yashindwa kupima CD4 kwa kukosa vitendanishi

Tue, 11 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Ifakara. Taasisi ya Afya Ifakara (IHL) imeiomba Serikali kupitia Bohari Kuu ya Dawa (Msd) kupeleka vitendanishi ili iweze kupima viwango vya kinga (CD4 ) kwa watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi.

Hatua hiyo itasaidia kuepuka gharama na usumbufu wa kusafirisha sampuli za damu kwenda Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Morogoro.

Ombi hilo lilitolewa jana na Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo, Dk Honorat Masanja wakati akitoa taarifa ya shughuli zinazofanywa na taasisi hiyo kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya Ukimwi na Dawa za Kulevya iliyofanya ziara kwenye taasisi hiyo.

Dk Masanja alisema kitendo cha taasisi hiyo kusafirisha sampuni hizo kutoka maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo na wilaya za jirani na kupeleka Hospitali ya Rufaa Morogoro kimekuwa kikisababisha mashaka kuhusu uhakika na usahihi wa majibu ya vipimo hivyo.

Alisema taasisi hiyo imefanikiwa kupata mashine aina ya Abbot kutoka kampuni ya Philips kwa ajili ya kupimia kiwango cha kinga CD4 ambayo ina uwezo wa kupima sampuli 300 hadi 900 kwa wiki.

Dk Masanja alisema taasisi hiyo ambayo imekuwa ikifanya tafiti, imekuwa ikitoa mafunzo na huduma mbalimbali za kiafya ikiwamo afya ya mama na mtoto pamoja na kliniki mseto inayowahusu wanafamilia wanaopatwa na maambukizi ya virusi vya ukimwi.  

Akijibu hoja hiyo ya vitendanishi Mwenyekiti wa kamati hiyo, Oscar Mkasa aliahidi kwa naiba ya wajumbe wa kamati  kuishauri Serikali kupeleka vitendanishi kwa ajili ya kupima kiwango cha CD4 badala ya kusafirisha kupeleka kwenye Hospitali ya Rufaa Morogogro.

Alisema lengo la ziara hiyo ni kujifunza na kupata taarifa ya tafiti mbalimbali zinazofanywa na taasisi hiyo ili kamati hiyo iweze kuishauri Serikali.

Mjumbe wa kamati hiyo, Salma Kikwembe alisema kumekuwa na changamoto ya kukosekana kwa mawasiliano baina ya watafiti na Serikali na hivyo kusababisha tafiti nyingi kushindwa kufika serikalini.

Alisema wao kama wabunge watahakikisha changamoto zote walizozisikia na kuziona wanazipeleka serikalini ili ziweze kufanyiwa kazi.

Kamati hiyo pia ilikutana na baraza la wanaoishi na virusi vya ukimwi wilaya ya Kilombero (Konga) ambalo limekuwa likifanya kazi ya kuwatafuta watoro wasiofika kliniki kuchukua dawa za kufubaza virusi vya ukimwi pamoja na kikundi cha wajasiliamali wanaoishi na VVU cha upendo. 

Mwenyekiti wa baraza hilo, Hilda Kumba aliuomba uongozi wa Hospitali ya Mtakatifu Francis kuwapa nafasi  baadhi ya watu wanaoishi na virusi vya ukimwi kufanya kazi zisizokuwa za kitaalam katika kituo cha kuchukulia dawa (CTV) ili waweze kutunza siri za wenzao wanaofika katika kituo hicho kuchukua dawa.

Naye mwakilishi wa kikundi cha wanaoishi na VVU cha Upendo, Mericia Yengulla, aliiomba hospitali hiyo  kuangalia uwezekano wa kuwapa dawa za miezi sita ili kupunguza usumbufu uliopo sasa ambapo wanalazimika kufuata dawa kila baada ya miezi mitatu.

Chanzo: mwananchi.co.tz