Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Taasisi ilivyoibua fursa taka za hospitali zenye ncha kali

Ccd444d331602bd1c05b2f4d12b16fbe Taasisi ilivyoibua fursa taka za hospitali zenye ncha kali

Mon, 7 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

“TANGU huduma za hospitali zilipoanza nchini, maboksi ya kuhifadhi taka ngumu za hospitali zenye ncha kali yamekuwa yakiagizwa kutoka nje ya nchi; serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi kuagiza maboksi haya salama.”

“Imekuwa ni vigumu sana kuyatengeneza hapa nchini kutokana na sababu kuu mbili; kwanza, mazingira magumu ya kupata vibali na pili, ni ukosefu wa karatasi zinazokidhi viwango vilivyowekwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) na Shirika la Viwango Tanzania (TBS).”

Ndivyo anavyosema Mkurugenzi wa Kitengo cha Upimaji Ardhi na Utengenezaji Vifaa vya Ardhi wa Kampuni ya Technotrade Investment Limited, Deogratias Karulama, katika risala kwa mgeni rasmi wakati wa hafla ya uzinduzi wa kiwanda cha kutengeneza maboksi ya kutunzia taka ngumu za hospitali zenye ncha kali cha Tecnotrade. Uzinduzi huo uliofanyika wiki iliyopita, eneo la Sido-Vingunguti, Dar es Salaam.

Katika risala hiyo, Technotrade waliongeza: “Kama tujuavyo, maboksi haya ni muhimu sana katika uendeshaji wa hospitali na kukosekana kwa maboksi haya kunaweza kusababisha madhara mbalimbali, si tu kwa wafanyakazi wa hospitali, bali kwa jamii nzima.”

ASILI YA MRADI WA MABOKSI

Kwa mujibu wa Karulama, mwaka 2017 Technotrade ilifanya utafiti ulioibua mkakati wa kutengeneza maboksi hayo ili kuunga mkono sera ya Serikali ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa viwanda.

“Kwa bahati nzuri, tulipata ushirikiano mkubwa kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto. Barua ya utambulisho tuliyoipata kutoka wizarani ilitutia moyo wa kuanzisha utengenezaji wa maboksi japo tulikutana pia na vikwazo mbalimbali.”

Anasema kwa kuwa walianzia katika eneo la makazi ya watu, ilibidi waingie gharama kubwa kuhakikisha wanazuia sauti ya mashine ndogo ya kukata maboksi.

“Mashine tuliyoanza nayo ilishindwa kukata maboksi yenye kiwango na hata kiwango cha karatasi nacho kilishindwa kufikia kiwango cha WHO na TBS.

“Hatukukata tamaa na badala yake, tuliagiza mashine ya kukata maboksi yenye kiwango na pia, tukaagiza karatasi kutoka nchi zenye viwango vinavyokubalika na TBS na WHO.”

Karulama akaongeza: “Sehemu ya kufanyia kazi nayo ilikuja na changamoto kuu mbili. Kwanza, ilibidi jengo tulilopewa na Sido (Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo) kufanyia kazi likarabatiwe, pili eneo lilikuwa na mgogoro wa umeme. Hata hivyo, uongozi wa Sido na Tanesco (Shirika la ugavi wa Umeme Tanzania) walitatua changamoto hiyo.”

UWEZO WA KIWANDA

Technotrade katika risala hiyo kwa mgeni rasmi wanasema hadi sasa kiwanda hicho kimeajiri Watanzania tisa kati yao, wafanyakazi sita ni wa kudumu na watatu ni wa muda.

Inasema: “Kwa siku tunaweza kuzalisha maboksi 1,000 ingawa mashine yetu inaweza kuzalisha zaidi… Mpango wetu mkuu ni kuzalisha maboksi 2,000 hadi 3,000 kwa siku ili kukidhi mahitaji ya nchi nzima… Tunaamini tukifikia lengo hilo, hakutakuwa tena na utumiaji wa maboksi yaliyo chini ya viwango na utumiaji wa maboksi ya sabuni na chupa za plastiki utaisha.”

Ndipo Technotrade wanasema: “Mgeni rasmi, kama ulivyojionea, ifikapo Februari 2021, tutakuwa na maboksi 100,000. Tunakuomba utusaidie kusisitiza wadau na watumiaji wa maboksi haya kuhusu umuhimu wa kununua na kutumia bidhaa hizi tunazozalisha hapa nchini hususani haya maboksi ya kutunzia taka ngumu za hospitali zenye ncha kali hasa ikizingatiwa kuwa, kiwanda hiki kimekuja na suluhisho la tatizo hili. Kimsingi, utashi wa serikali katika jambo hili utasaidia kufikia malengo.”

Awali akizungumza na HabariLEO, Meneja wa Technotarde, Kanda ya Dodoma, Mushumba Philbert, alisema kukosekana kwa maboksi hayo katika hospitali, vituo vya afya na zahanati nchini kunaweza kusababisha madhara kwa wafanyakazi wa hospitali mbalimba na jamii nzima kwa jumla.

Alisema miongoni mwa taka ngumu za hospitali zenye ncha kali ni pamoja na sindano za dawa zilizotumika, nyembe na sindano za kuchoma ili kutoa damu kwa ajili ya kupima malaria.

“Hivyo ukivitupa au kuvifukia, watoto wakivipata au kuviokota au hata kuvifukua, vinaweza kuleta madhara kwao na kwa jamii na hata kwa wahudumu wa afya wenyewe,” alisema Mushumba.

Technotrade Investment Limited ambayo Mkurugenzi Mkuu wake ni Gordian Ntake, inajishughulisha pia na usambazaji wa vifaa vya kisayansi vikiwamo vya ‘survey’, maabara, upimaji wa udongo, kemikali na vifaa vya teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama).

Katika uzinduzi huo wa kiwanda, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Viwanda katika Wizara ya Viwanda na Biashara, Ramson Mwilangali, aliyemwakilisha Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Ludovick Nduhiye aliyekuwa mgeni rasmi, anasema serikali itafanya kila jitihada kuhakikisha maboksi yaliyozalishwa yanaingia sokoni.

Anafafanua kwamba hilo linatokana na viwango vya ubora unaokubalika na TBS na WHO wa maboksi hayo na pia ambayo anahitajika nchini hivyo, hakuna sababu ya watumiaji kuagiza nje ya nchi au kutumia bidhaa zenye viwango duni vya ubora.

Kimsingi, serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, imetoa Mwongozo wa kuhifadhi taka ngumu za hospitali zenye ncha kali (National Policy Guidelines for Healthcare Waste Management in Tanzania).

Wataalamu mbalimbali wa afya wanasema kwa nyakati na mazingira tofauti kuwa, taka hizo zisipohifadhiwa ipasavyo, zinaweza kusababisha maambukizi mbalimbali ya magonjwa kwa wafanyakazi wa sekta ya afya wakiwa wa hospitali na jamii kwa jumla.

Mwilangali anasema katika uzinduzi huo kuwa, taka zenye ncha kali zinapaswa kuteketezwa mara tu, zinapotokea kwa sababu ni hatari zaidi hata kwa watoto kwa sababu wanaweza kuzitumia hususan sindano katika michezo yao.

“Ripoti kadhaa zimeonesha namna hata wanyama hususan mbwa wanavyofukua taka hizo zilizozikwa wakidhani watapata chakula. Zoezi hili linaposhidikana, taka zenye ncha kali huachwa wazi na kuwa hatari zaidi kwa jamii,” anasema.

Mgeni rasmi anabainisha kuwa, ingawa zimekuwa zikitumika chupa za maji za plastiki (PET Botlles) na vidumu vya plastiki kuhifadhi taka hizo katika hospitali, zahanati na vituo vya afya nchini, uhifadhi huo wa taka zenye ncha kali si salama.

Kwa mujibu wa Mwilangali, kampuni ya Technotrade imeonesha ubunifu mkubwa unaounga mkono sera ya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa viwanda inayosisitizwa na Rais John Magufuli hivyo, wadau wengine zikiwamo hospitali, vituo vya afya na zahanati zinapaswa kuiunga mkono kwa kutumia bidhaa zake.

“Tunazo taarifa kuwa Technotrade imeuteua Mkoa wa Dar es Salaam kuwa ‘darasa mama’ kwa ajili ya matumizi sahihi ya maboksi hayo salama. Serikali ina matumaini makubwa kuwa juhudi zenu zitafanikiwa na serikali itashirikiana nanyi kuhakikisha mnafanikiwa kufikia malengo ya kutoa huduma nchi nzima,” alisema.

Akaongeza: “Wadau na watumiaji sasa wayatumie maboksi haya ambayo yamethibitishwa ubora wake na TBS na yanakidhi viwango vya Shirika la Afya Duniani, badala ya kuagiza nje ya nchi hali inayotumia muda na gharama kubwa.”

“… Mradi mlioubuni wa kutengeneza maboksi salama kwa ajili ya kuhifadhia taka za hospitali zenye ncha kali una soko la kutosha hapa nchini maana serikali na sekta binafsi zina hospitali, zahanati na vituo vya afya 8163, aidha, Bohari Kuu ya Dawa (MSD) ina zabuni SADC ya dawa na vifaa tiba. Hilo nalo, ni soko la kutosha mnatakiwa mlifanyie kazi.”

Aliwataka wadau mbalimbali kuupa kipaumbele mradi huu ili serikali isipoteze fedha za kigeni kuagiza maboksi hayo nje ya nchi hasa India ambako yananunuliwa kwa sasa na akatoa mwito kwa Technotrade kushirikiana na viwanda vya karatasi nchini kikiwamo cha Mgololo kilichopo Mufindi, kupata suluhisho la kupata karatasi zinazotakiwa na kwa viwango vinavyotakiwa vya TBS na WHO hapa nchini kuliko kuagizia nchi za nje kwani kufanya hivyo, kutawaongezea kipato na kuokosa fedha za kigeni ziende nje ya nchi.

“Itakuwa vyema mkishirikiana na viwanda hivyo ili mpate suluhisho la kupata karatasi zenye viwango vya ubora unaotakiwa hapa nchini, badala ya kuagiza nje ya nchi kwani kwa kufanya hivyo, mtajiongezea kipato na mtaokoa fedha zetu za kigeni zisiende nje ya nchi,” alisema.

Kaimu Mkurugenzi wa Nafunzo na Usimamizi wa Mikoa wa Sido, MacDonald Maganga, anasema Sido ipo tayari kuendelea kushirikiana na Technotrade, Mamlaka ya Mafunzo ya Ufundi Stadi (Veta) na wawekezaji wengine ili kukabili changamoto zinazojitokeza.

Naye Ofisa Biashara wa Mkoa wa Dar es Salaam, Thabiti Massa, anasema katika mazungumzo na HabariLEO kuwa, ni muhimu taasisi mbalimbali kuiga mfano wa Technotrade kuanzisha viwanda nchini ili kuongeza ajira, kuongeza thamani na kuokoa fedha na muda sambamba na kukuza ajira huku zikizingatia ubora.

Wakati wa tukio hilo, Technotrade ilitoa maboksi 200 ya kuhifadhia taka ngumu za hospitali zenye ncha kali kwa Wizara ya Viwanda na Biashara ili kuzikabidhi kwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

Chanzo: habarileo.co.tz