Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Taarifa za DNA za Watanzania wote kuhifadhiwa

86116 Pic+mkemia Taarifa za DNA za Watanzania wote kuhifadhiwa

Thu, 28 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali nchini Tanzania iko kwenye mchakato wa kutengeneza kanzi data ya vinasaba (DNA) vya Watanzania wote ili kurahisisha utoaji wa huduma ya vinasaba kwenye matukio ya ajali, uhalifu au masuala ya kijamii.

Mamlaka hiyo imejiwekea muda wa miaka miwili kuanzia sasa kuanzisha kanzi data hiyo ambayo inaelezwa itasaidia kutatua changamoto mbalimbali kwa urahisi na kwa muda mfupi.

Hayo yamebainishwa leo Jumatano Novemba 27, 2019  jijini Dar es Salaam, Mkemia Mkuu wa Serikali, Dk Fidelice Mafumiko wakati akizungumzia mafanikio ya mamlaka hiyo katika kipindi cha miaka minne ya serikali ya awamu ya tano iliyoingia madarakani Novemba 27, 2019.

Amesema kanzi data hiyo itasaidia utambuzi wa vinasaba vya watu waliopata ajali bila kuhitaji kuwapima ndugu zao. Pia, wahalifu wa matukio kama ubakaji wataweza kutambuliwa hata kabla hawajakamatwa.

"Kuna faida nyingi za kuwa na kanzi data, kwanza uchunguzi wa vinasaba utafanyika kwa haraka kwa kufanya ulinganifu wa sampuli iliyopatikana na ile inayopatikana kwenye kanzi data hiyo," amesema Dk Mafumiko.

Amesema mwamko wa uchunguzi wa vinasaba umeongezeka ambapo kwa wastani wanapokea sampuli tatu hadi nne kwa siku kutoka jeshi la polisi kwa mambo ya kihalifu au ustawi wa jamii kwa mambo ya kijamii kama vile utambuzi wa watoto.

"Database itarahisisha sana uchunguzi wa vinasaba, hata kama unataka kujua mzazi wa mtoto, tunachukua sampuli zake na kulinganisha na kwenye database yetu," amesema.

Mkemia Mkuu amesema mamlaka hiyo imefanikiwa kushiriki katika uchunguzi wa matukio ya ajali mbalimbali hapa nchini na kufanikisha utambuzi wa miili ya watu ambao haikutambuliwa na ndugu zao.

Pia, amesema katika kipindi cha miaka minne, tozo 17 zilizokuwa zinatozwa na mamlaka hiyo zimefutwa na tozo nane zimepunguzwa. Amesema lengo ni kuboresha mazingira ya biashara hapa nchini.

Chanzo: mwananchi.co.tz