Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Taarifa ya NIMR kuhusu chanjo ya COVID kugandisha damu

5bbe710ea5bfb0aa05458d98def84ad3.jpeg Chanjo ya COVID-19

Fri, 6 Aug 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

Mkuregenzi Mkuu wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Profesa Yunus Mgaya amesema hadi sasa hakuna mtu nchini aliyechomwa chanjo ya kinga ya corona na kukutwa na tatizo la kuganda damu au jingine lolote.

Profesa Mgaya alisema tukio la kuganda damu hutokea mara chache sana na hata Marekani ambako inasemekana kulikuwa na watu waliokutwa na changamoto hiyo ilikuwa ni watu wanne kati ya watu milioni moja.

Alisema hayo wakati wa kipindi maalumu kuhusu chanjo ya corona kilichorushwa na chaneli ya TBC1 ya Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).

Alisema chanjo inayochomwa nchini ya Johnson & Johnson ni salama na kama kuna changamoto baada ya kuchanjwa ni za kawaida.

“Hakuna taarifa za watu kudhurika kwa kiasi cha kupoteza maisha au kuganda damu ila ifahamike kuwa kama kuna changamoto ni zile za kawaida zinazoweza kutofautisha mtu na mtu. Mfano mimi nilichanjwa lakini sikusikia kichefuchefu kama wengine wala sikupata maumivu ya kichwa ila niliumwa kidogo mkono na kesho yake nikawa salama kabisa,” alisema Profesa Mgaya.

Alisema chanjo zinazotolewa nchini zilipimwa kwanza na zimethibitishwa zina ubora, hivyo changamoto ndogo za kawaida zisisababishe mtu aamue kutochanjwa.

“Chanjo siyo dawa ndugu zangu, ni kinga sasa mhakikishe kuwa mnachanja mapema Watanzania na siyo kungojea kupata ugonjwa huo na ndiyo kuanza kutafuta chanjo hivyo nawasihi watu wakachanje sasa na kisha kuendelea kuchukua tahadhari zinazotakiwa,” alisema Profesa Mgaya.

Daktari Bingwa wa Mapafu wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk Pauline Chale alisema dhana ya kuwa chanjo ya corona si salama haina nguvu kwa sasa kwani hata madaktari wanachanja chanjo hiyo ya Johnson & Johnson.

Dk Chale alisema wanaokataa kuchanja watajikuta wakiingia kwenye gharama zaidi hasa watakapoumwa na kulazimika kulazwa.

“Najua wapo watu ambao wanaodhania wakiumwa covid-19 ndiyo wataenda kuchanjwa hii siyo sawa kwa kuwa mtu akiumwa anapaswa kutochanjwa hadi akipona kabisa,” alisema na kuongeza:

“Hivyo muende kuchanja sasa hivi kwani itazuia au hata kupunguza nguvu ya ugonjwa kuingia mwilini, mimi nimefanya kazi muda mrefu kwenye huduma za mapafu ninajua hali inavyokuwa mbaya kwa mtu akipatwa na tatizo la kupumua, ndugu zangu mkachanje.”

Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Aifello Sichalwe jana alilieleza HabariLEO kuwa, suala la ugonjwa wa covid-19 si la wizara hiyo pekee, hivyo kama kuna dosari zikiwamo tuhuma za rushwa kwenye utoaji chanjo wananchi watoe taarifa.

"Taarifa za wahudumu wa afya kuchukua rushwa wakati wa utoaji chanjo hatujazipata, lakini cha msingi suala la covid-19 siyo la wizara ya afya pekee, ni la kila mtu, idara, taasisi na wizara mbalimbal,” alisema Dk Sichalwe na kuongeza:

"Pia wananchi watambue kuwa chanjo hii ni bure, hivyo kutoa rushwa siyo tu kujinyima haki yako ya msingi, bali utakuwa unatenda kosa la kutoa rushwa."

Alisema mikoa yote nchini imepokea chanjo ya covid-19 na kuna mwitikio mkubwa wa wananchi kupata kinga hiyo.

"Wizara kupitia MSD (Bohari ya Dawa) ilifanya usambazaji wa chanjo za Uviko-19 na vifaa katika mikoa yote nchini na mpaka jana (Agosti 3), mikoa yote 26 nchini ilikuwa imepokea chanjo.”

Alisema kazi ya kutoa chanjo ni endelevu hadi wananchi zaidi ya asilimia 60 watakapochanwa.

"Wizara pamoja wadau wote yakiwamo mashirika, NGO na makundi binafsi mbalimbali na mtu mmoja mmoja, wanaendelea kutoa elimu ya chanjo katika makundi mbalimbali na ngazi tofauti nchini,” alisema Dk Sichalwe.

Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Shedrack Mwaibambe aliwataka watumishi wa afya wenye tabia ya kuomba rushwa kwa wananchi wanaokwenda kupata chanjo waache mara moja.

Chanzo: www.habarileo.co.tz