Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Taadhari kwa wauza nyama mabuchani

NYAMAS Taadhari kwa wauza nyama mabuchani

Thu, 10 Sep 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

OFISA Masoko wa Jiji la Dodoma, James Yuna amewataka wafanyabishara wa machinjio ya kuku na wauza nyama kwenye mabucha, kufanya kazi zao kwa umakini ili kuzuia mlipuko wa magonjwa.

Yuna alisema hayo juzi wakati akizungumza na wafanyabiashara hao kutokana na ukaguzi alioufanya kwenye machinjio ya kuku na mabucha ya kuuzia nyama yaliyopo katika masoko ya jiji hilo.

Aliwataka kuhakikisha machinjio hayo yanakuwa katika mazingira safi kwa muda wote. Alisema baadhi ya machinjio ya kuku na mabucha, yana mazingira ambayo siyo rafiki katika suala la usafi, hivyo ni muhimu wakajihadhari na milipuko ya magonjwa yanayoweza kujitokeza kutokana na suala hilo.

“Mjihadhari na magonjwa yanayoweza kujitokeza kutokana na mazingira mnayofanyia biashara zenu, hapa tatizo likitokea siyo nyinyi tu bali hata kwa wateja wenu pia wanaweza kujikuta wakikumbwa na ugonjwa,” alisema.

Alisema bado kuna changamoto kwa baadhi ya wafanyabiashara ndogo, kutozingatia usafi kwenye maeneo wanayofanyia biashara zao, hali ambayo imekuwa ikisababisha kuwepo kwa takataka na harufu kali ya uchafu.

Ofisa huyo wa masoko aliwataka wafanyabishara ndogo maarufu wamachinga, kufuata kanuni na sheria zinazoelekezwa na jiji kwa kutofanya biashara kwenye maeneo yasiyo rasmi, yanayohatarisha maisha na bidhaa zao.

. Akizungumza na wafanyabishara kwenye masoko yaliyovamiwa na wamachinga, aliwataka kutofanya shughuli katika sehemu ambayo siyo rafiki kwa upande wao.

Alisema bado kuna changamoto kwa baadhi ya wamachinga kupanga bidhaa zao maeneo yasiyo rafiki kwao na kwa wateja wao na kusababisha adhaa kubwa inayoweza kujitokeza.

“Wengi hukimbilia kupanga bidhaa kandokando ya barabara maeneo ambayo hutumika kupita magari na pikipiki, hali hii inaweza kusababisha ajali na pia uharibifu wa bidhaa zao na hata kwa maisha yao ikiwemo na wateja wanaonunua bidhaa hizo,”alisema.

Alisema jiji hilo halitakuwa tayari kuwaona baadhi ya wamachinga, wakikiuka maelekezo yaliyotolewa ya ufanyaji biashara. Alisema jiji hilo litaendelea kutoa elimu, ili sheria na utaratibu uweze kuzingatiwa na kuheshimiwa kwa pande zote mbili.

Aliwataka wafanyabiashara hao kushirikiana na halmashauri ya jiji pale wanapogudua kuna baadhi yao wamekiuka maelekezo kutoka ngazi husika, kama vile kuvamia maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya shughuli za kiserikali na kuweka vibanda vya biashara.

Chanzo: habarileo.co.tz