Mamalaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) Kanda ya Ziwa Mashariki imewaonya wafamasia wanaokiuka sheria na taratibu za usimamizi na matumizi sahihi ya dawa tiba zenye asili ya kulevya kwa sababu vitendo vyao vinasababisha kuchepushwa na madhara kwa binadamu.
Onyo hilo limetolewa jijini Mwanza leo Novemba 13, 2023 na Meneja wa TMDA Kanda ya Ziwa Mashariki, Sophia Mziray wakati wa hafla ufunguzi wa mafunzo ya kuwajengea uwezo wafamasia wa vituo vya afya na hospitali za Mkoa wa Mwanza vyenye vibali vya kutumia dawa hizo.
‘’Lengo la mafunzo haya ni kuwajengea uwezo na kuwakumbusha wafamasia kuhusu uhifadhi, matumizi sahihi ya dawa zenye asili ya kulevya, utunzaji na uandaaji taarifa na kumbukumbu,’’ amesema Sophia
New Content Item (2)
Amesema dawa hizo zisipotumika kwa usahihi zinaweza kusababisha madhara; hivyo wafamasia ni lazima watimize wajibu na jukumu la kuzisimamia kkulingana na miongozo, kanuni na taratibu.
“Katika kaguzi tulizofanya kwenye vituo vya huduma, tumebaini uwepo wa changamoto za utunzaji wa taarifa, vyeti vya daktari kutoendana na aina ya dawa zinazotolewa, uhifadhi usio sahihi wa dawa na baadhi ya vituo kutotoa kwa wakati taarifa za matumizi na hivyo kuchelewesha upatikanaji wa vibali. Changamoto zote hizo huwaathiri wagonjwa,” amesema Sophia
Mtaalam huyo amesema kwenye baadhi ya vituo vya huduma, wafamasia wamebainika kutotoa ushirikiana wa kutosha kwa wauguzi na madaktari, hali inayoathiri huduma kwa wagonjwa.
‘’Wafamasia ndio wataalam wa dawa; ni lazima washirikiane na wataalam wengine wakiwemo wauguzi na madaktari kukamilisha huduma kwa wagonjwa ambao ndio wateja wetu sote,’’ amesema
Akizungumzia adhabu ya kufungia vibali vya matumizi ya dawa zenye kulevya, Sophia amesema hatua hiyo hufikiwa kulinda usalama na afya za wananchi pindi wahusika wanaposhindwa kutimiza wajibu wao kuanzia kwenye uhifadhi na matumizi ya dawa hizo.
Kamishna Msaidizi wa Oparesheni Mamlaka ya Kudhibiti na Kpambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA) Kanda ya Ziwa, Inspekta wa Polisi Wamba Msafiri amesema matumizi yasiyo sahihi ya dawa tiba zenye asili ya kulenya ni kosa kisheria kwa mujibu wa Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za kulevya ya mwaka 2015, Sura ya 95.
‘’Wanaotenda kosa hili waache mara moja kwa sababu wanatenda kosa kisheria na wakifikishwa mahakamani na ushahidi kuthibitisha makosa yao wanaweza kuhukumiwa kifungo cha maisha jela,’’ Inspekta Msafiri
Amesema kutokana na ukubwa wa tatizo la dawa za kulevya, DCEA imeanzisha ofisi za kanda huku akiwaomba wananchi wenye taarifa ya matumizi au biashara isiyo halali ya dawa tiba zenye asili ya kulevya kutoa taarifa kwa mamlaka husika ili kudhibiti matumizi yasiyo sahihi.
“Vitendo cha kutoa kiholela ama kuchepusha dawa tiba zenye kulevya vinaathiri afya za watumiaji sawa sawa na wanaotumia dawa zingine za kulevya ikiwemo Coccaine, heroine na bangi. Vitendo hivi vinaathiri siyo tu afya bali pia uchumi kwa sababu Taifa inakosa nguvu kazi,’’ amesema mkaguzi huyo wa Polisi
Theresa Lubasa, mmoja wa wafamasia wanaohudhuria mafunzo hayo amesema elimu wanayopata inawajengea uwezo kwa kuwakumbusha wajibu na majukumu yao ya usimamizi na udhibiti wa dawa.
Mfamasia kutoka Ofisi ya Mganga Mkuu Mkoa wa Mwanza, Baraka Kasase amewashauri wenzake kufuata miongozo ya uhifadhi, utoaji na udhibiti wa dawa ili zisiangukia kwenye mikono ya watu wasio na nia njema.