Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TMDA yapewa onyo kali

223f5dff91f7ffd6fc1f105a9753eeaa.png Mamlaka ya Dawa na Vifaa tiba nchini (TMDA)

Wed, 16 Feb 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mamlaka ya Dawa na Vifaa tiba nchini (TMDA) imetakiwa kuimarisha udhibiti wa uingizwaji wa dawa na vifaa tiba hafifu ili kuimarisha afya za wananchi na kuwalinda na madhara yatokanayo na matumizi ya bidhaa hizo.

Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Adam Malima wakati wa ziara ya Bodi ya Ushauri ya Wizara ya Afya kwa TMDA na menejimenti ya mamlaka hiyo.

Alisema ni muhimu mamlaka hiyo ikaongeza nguvu ya udhibiti wa dawa na vifaa tiba hafifu katika maeneo ya mipaka kabla ya kuwafikia watumiaji ili kulinda usalama wao.

"Muwe wakali na kuimarisha ukaguzi katika maeneo yote ya mipakani ili kudhibiti mianya ya uingiaji wa bidhaa za vyakula na dawa ambazo hazina viwango ili kulinda wananchi wetu," alisema.

Aidha, alitaka TMDA kushirikiana na kamati za usalama za wilaya na mikoa kwenye maeneo yote nchini badala ya kufanya jukumu la udhibiti na ukaguzi wa dawa na vifaa tiba hafifu na duni peke yao kwani wanaweza wasifikie lengo linalotarajiwa kwa haraka.

Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Adam Fimbo alisema kwa upande wa Kanda ya Mashariki wanakabiliwa na changamoto ya uchepushaji wa dawa za serikali zilizopo kwenye vituo vya afya, hali ambayo inasababisha uhaba wa dawa mara kwa mara kwenye vituo hivyo.

"Kwa utafiti mdogo ambao tumeweza kufanya tumebaini kuna uchepushwaji mkubwa wa dawa za serikali kwenda katika maduka binafsi ya dawa, huku wakiacha hospitali zinakosa dawa, hali ambayo ni kero kwa wananchi," alisema.

Alitaja changamoto nyingine kuwa ni uwepo wa dawa bandia za mifugo, hali ambayo inaleta usugu wa dawa kwa mifugo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live