Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TMDA yakamata ghala 'bubu' la dawa za nguvu za kiume Dar

IMG 20220628 WA0018 1 TMDA yakamata ghala 'bubu' la dawa za nguvu za kiume Dar

Tue, 28 Jun 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Dawa za shinikizo la damu, za kuongeza nguvu za kiume, za kutoa ujauzito na dawa nyinginezo nyingi zisizosajiliwa zimekamatwa zikiwa zimehifadhiwa katika ghala ambalo nalo halijasajiliwa.

Pamoja na dawa hizo za binadamu ndani ya ghala hilo pia kumekutwa vifaa tiba mbalimbali ambapo vyote ni vya mamilioni ya fedha.

Maafisa wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) Kanda ya Mashariki, wamebaini ghala hilo katika Mtaa wa Kitumbini, uliopo Kata ya Mchafukoge katikati mwa Jiji la Dar es Salaam.

Akizungumza eneo la tukio, Meneja wa Kanda wa TMDA, Bw. Adonis Bitegeko amesema bidhaa hizo zimekamatwa katika ukaguzi maalum, zina thamani ya zaidi ya Tsh. Mil. 294.

Amesema ukaguzi huo umefanywa na timu ya TMDA Kanda ya Mashariki kufuatia taarifa za kiinteligensia zilizofuatiliwa kwa muda mrefu. "Tumebaini ghala hili linamilikiwa na mtanzania mwenye asili ya India Bw. Ramaiya Rijendra, limehifadhi dawa mbalimbali za binadamu ambazo hazijasajiliwa kwa hiyo ubora, usalama na ufanisi wake haujulikani," amesema.

Amesema hatua zilizochukuliwa hadi sasa ni pamoja na kuziorodhesha bidhaa hizo na kuziondoa.

"Hatua zaidi za kisheria zitachukuliwa ikiwemo kuwatoza faini isiyopungua Tsh. Mil. 85 na kuziteketeza kwa gharama zao," amebainisha.

Ameongeza "Tunatoa wito kwa wanaoendelea kufanya biashara hizo haramu kuacha mara moja laa sivyo watachukuliwa hatua kali za kisheria.

Ametoa onyo pia wataalamu wa dawa ambao wanajihusisha na biashara hizo haramu kuwa hawatosita kuwafutia leseni zao za kitaaluma. "Rai yetu ni kwamba wale wote wanaofanya biashara haramu adhabu ni kali na hatutomuacha mtu," amesisitiza.

Amesema ukaguzi huo maalum ulianza jana jioni na kufanyika usiku kucha hatimaye kuhitimika leo asubuhi.

"Mtuhumiwa aliyekutwa nazo alipohojiwa alikiri kuendesha ghala hilo bubu pasipo na kibali na kinyume na sheria kwa kile alichodai hakufahamu taratibu zinazohusika kusajili na kuendesha biashara hiyo," amesema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live