Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TMDA yabaini dawa bandia sokoni

67156 Pic+dawa

Wed, 17 Jul 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) imeutahadharisha umma kuhusu kuwepo kwa dawa bandia sokoni aina ya Gentrisone Cream ambayo lebo yake inaonyesha namba GNTRO X030.

Dawa hiyo inaelezwa kufanana na dawa halisi isipokuwa zinatofautiana kwenye namba ya toleo.

Matoleo mengine ya dawa hiyo siyo bandia kwa kuwa yamesajiliwa na mamlaka hiyo na kuthibitika yanatibu magonjwa ya ngozi kama miwasho, upele, kuungua moto, fangasi za miguuni na maeneo mengine ya mwili.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Jumatano Julai 17, 2019  na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, uchunguzi uliofanywa na maabara ya mamlaka hiyo umethibitisha kuwa dawa hiyo bandia haina viambato hai ambavyo kwa kawaida vipo kwenye dawa halisi iliyosajiliwa, pia haina harufu ya dawa.

“Wananchi wote ambao wamenunua dawa hii kutoka kwenye maduka ya dawa wanashauriwa kuangalia kwenye lebo na ikiwa wataona namba ya toleo GNTRO X030 kwenye boksi la dawa husika warudishe waliponunua,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.

Pia, wauzaji wa jumla wenye dawa hiyo kwenye stoo zao wametakiwa kuacha kuzisambaza, badala yake wawasiliane na TMDA ili kupewa utaratibu wa wapi kwa kuzipeleka.

Pia Soma

Taarifa hiyo inaeleza kwamba tayari TMDA imechukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuondoa kwenye soko ya dawa (tube) 4,188 kutoka Mikoa ya Mwanza (1814), Dar es Salaam (931), Dodoma (591), Tabora (29), Arusha (6) na Mtwara (817).

“TMDA inaendelea kuwaomba wananchi wote kuendelea kutoa taarifa ikiwa watabaini kampuni, kikundi, mitandao au mtu yoyote anayejihusisha na utengenezaji, usambazaji na uuzaji wa dawa za dawa bandia ili hatua ziweze kuchukuliwa  kumkamata haraka na kumfikisha kwenye vyombo vya sheria” amesema kaimu mkurugenzi kwenye taarifa hiyo.

Chanzo: mwananchi.co.tz