Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TMDA ilivyojipanga kufanikisha chanjo dhidi ya corona

3402f6ca5a8be091cf05181fa482233a TMDA ilivyojipanga kufanikisha chanjo dhidi ya corona

Mon, 19 Jul 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MATUMIZI ya dawa zisizokuwa na ubora na usalama husababisha athari za kiafya na hata vifo kwa watumiaji. Ndivyo ilivyo pia kwa matumizi ya vitendanishi na vifaa tiba kwani visipokuwa bora na kukosa ufanisi huweza kusababisha kusambaa kwa maambukizi kwa watumiaji.

Katika kufanikisha usalama, ufanisi na ubora wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi, Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) imepewa jukumu la kudhibiti bidhaa hizo na moja ya njia inayotumika ni kuvichunguza kisayansi kwa kuvipima katika maabara zake.

Uchunguzi huo unajumuisha upimaji wa viambata hai katika dawa na uwezo wa kumlinda mtumiaji kwa vifaa tiba.

TMDA imeendelea kupata mafanikio katika kazi zake kwa jamii huku kukiwa na mabadiliko mengi chanya. Miongoni mwa mafanikio hayo ni namna ilivyojipanga katika kuhakikisha nchi inapata chanjo ya corona yenye ubora, ufanisi na usalama.

Upimaji na usajili

Nchi mbalimbali katika bara la Afrika wakiwemo majirani wa Tanzania; Kenya na Uganda, tayari zimeshaanza kuwapa wananchi wake chanjo ili kujikinga na ugonjwa unaosababishwa na virusi vya corona (Covid 19).

Wakati Zanzibar wameshaanza kutoa chanjo kwa baadhi ya makundi, Tanzania nayo inatarajia kuanza matumizi ya chanjo muda si mrefu, lengo ilikiwa ni kuwalinda wananchi na wimbi la tatu la virusi vya corona lijukanalo kama Delta.

Katika muktadha huo, ofisi za balozi za nje nchini tayari zimeruhusiwa kuchanja watu wao.

Hatua inazochukua Tanzania kuhusu ugonjwa wa corona zilianza kwa Rais Samia Suluhu Hassan kuunda kamati maalumu kwa ajili ya kutoa mapendekezo na ushauri wa namna ya kukabiliana na wimbi la ugonjwa huo.

Kamati hiyo ilikuja na mapendekezo 19, moja wapo likiwa ni kuruhusu matumizi ya chanjo ambayo ni bora na salama kwa wananchi kwa njia ya hiari.

Jukumu la kuhakikisha ubora, usalama na ufanisi wa chanjo zote ikiwemo hiyo ya corona ni la Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA).

Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Adam Fimbo anasema hadi sasa kuna aina nane za chanjo za Covid-19 zilizoainishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa matumizi ya dharura.

“Kwa suala la chanjo ya Covid-19 tunahusika katika kutoa vibali. Kwanza tunasajili na baada ya hapo tunatoa vibali kwa uingizaji. Tunatakiwa kuona ufanisi, usalama na ubora wa chanjo hata inapokuwa kwenye soko.

“Vilevile tunashiriki tathamini ya pamoja na Shirika la Afya Duniani (WHO), tunapeleka wataalamu, wanaenda kule kwa ajili ya kufanya tathmini ya ubora na ufanisi wa chanjo. Hata kwenye chanjo za corona tunashiriki,” anasema.

Anaongeza: “Ili kuweka sera ya kimataifa kwenye masuala ya chanjo tunashirikiana na wenzetu wanaosimamia masuala ya chanjo chini ya Wizara ya Afya. Pia kuna kamati ya kitaifa iliyoundwa inayohusika kupitia aina za chanjo zinazoruhusiwa ndani ya nchi na kutoa ushauri.”

Fimbo anasema TMDA inasubiri utaratibu rasmi utakaopitia kamati iliyoundwa na Rais kupitia Wizara ya Afya ili kutoa sera na mwelekeo wa chanjo hiyo.

“Muda sio mrefu chanjo iliyosajiliwa, yenye usalama itaanza kutumika nchini. Hii ni kazi kubwa ambayo tumejipanga kuifanya.

“Tuna mawasiliano ya karibu kila siku na WHO kufahamu kuna chanjo ngapi. Mfano hadi sasa chanjo zilizofanyiwa utafiti ni 200 na chanjo 60 ziko kwenye majaribio na bado watafiti wanafanya tafiti zaidi kwa ajili ya kuzuia ugonjwa huu,” anasema.

Anasema wanajiandaa pia kutoa elimu kwa umma kuhusiana na matumizi sahihi sambamba na ubora wa chanjo itakayotumika nchini.

“Tuna maabara yetu inayohusika na upimaji na kuweza kusoma taarifa za kisayansi na kitaalamu kabla ya kwenda kusajili chanjo,” anasisitiza.

Siku 100 za Rais Samia

Fimbo anasema kwamba katika siku 100 za Rais Samia Suluhu Hassan madarakani wamepokea maelekezo kadhaa ambayo utekelezaji wake umefanyika kwa ufanisi.

"Rais Samia ameanza kufanya kazi yake vizuri na sisi kama mamlaka ya udhibiti wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi kama sehemu ya Wizara ya Afya, majukumu yetu ni kufanya udhibiti ili kulinda afya ya jamii,” anasema.

Anatoa mfano wa moja ya maelekezo waliopata ndani ya siku 100 kuwa ni kupandisha watumishi vyeo na kwamba katika kutekeleza hilo na kuongeza ufanisi wa kazi wameeongeza watumishi 20.

Anasema kwa kuwa Rais Samia amekuwa akielekeza kusimamia masuala ya rushwa na kusisitiza uwajibikaji, TMDA imekuwa pia ikisisitiza sana uwajibikaji kwa kuweka mifumo unayofanya kazi.

“Tunasimamia vizuri uwajibikaji kwa wafanyakazi na taasisi inafanya vizuri. Tumefanyiwa tathmini na tumepata cheti na kuwa washindi wa pili kwa taasisi ambazo zinawakilisha serikali kwa kuwa na mifumo bora.

“Rais amesisitiza kutoa huduma kwa haraka na sisi tumefanikiwa kwa hilo. Kibali cha kuingiza bidhaa za dawa nchini kinapatikana ndani ya saa 24, hivyo huduma zinapatikana haraka.” anasema.

Anasema ili kurahisisha kazi za ukaguzi wameanzisha ofisi za kanda kwa nchi nzima na kwa sasa tayari wana ofisi nane nchini ambazo anasema wanahakikisha zinafanya kazi vizuri ikiwemo ukaguzi kwenye mipaka na kufika hadi vijijini.

Matumizi holela ya dawa

Fimbo anaiasa jamii kuacha matumizi holela ya dawa kwani ni bidhaa ambazo zina kemikali zenye sumu na kwamba zikitumika vibaya zina madhara makubwa kwa afya ya mwanadamu.

“Ni muhimu kwa jamii kwanza kabla ya kupata dawa wapate ushauri wa wataalamu wa afya au daktari, kufanya vipimo, kupata majibu na kutumia dawa iliyosahihi na wasitumie vibaya au tofauti na walivyoelekezwa na watalaamu.

“Na kama mtu utaona madhara yoyote kwa kuwa dawa pia zina madhara (side effects) toa taarifa kwa mamlaka ili tuweze kuchukua hatua.

“Kuna dawa bandia na vifaa tiba bandia na duni ambavyo pia vinapatikana kwenye soko kwa kuingizwa nchini kinyemela. Ukiona au ukihisi kuwa dawa fulani ni bandia toa taarifa itatusaidia kubaini wanaoingiza bidhaa hizo,” anasema.

Anasema kwamba kazi ya udhibiti inahitaji doria na wao wana wafanyakazi wachache ambao hawawezi kuwa katika dori kwa wakati wote na hivyo mtu akitoa taarifa inawasaidia kudhibiti dawa na vifaa tiba bandia nchini.

Mikakati zaidi

Fimbo anasema mpango mkakati wao ni kuhakikisha bidhaa zinazoingia nchini zinakuwa bora, salama na zenye ufanisi kwani wanalinda afya za watu.

“Kwa upande wa upimaji tunahakikisha tunafanya vizuri kwani ni moja ya kazi zetu kuanzia ukusanyaji wa sampuli na tuna maabara zinazotambulika kitaifa.

“Pia tunakazi ya kuelimisha jamii juu ya masula ya kujilinda na kujikinga na dhidi ya athari zinaweza kutokeza kwa matumizi ya yasiyofaa ya dawa na vifaa tiba,” anasema.

Chanzo: www.habarileo.co.tz